“Jambo la kwanza, tunahitaji kumaliza vita. Kisha tuanzishe upya viwanda,” amesema Basher Abdullah, mshauri wa Waziri wa Viwanda na Biashara wa Sudan.

Kama ilivyo kwa nchi nyingi maskini, juhudi za Sudan kukuza uchumi wake zimezoroteshwa na migogoro. Hata hivyo, hata katikati ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda UNIDO linaendelea kutoa msaada wa kiuchumi na njia ya kuelekea katika ujenzi wa taifa.

Kauli hiyo ya “kwanza kumaliza vita, kisha kuanzisha upya viwanda” ilikuwa mbali kabisa na mandhari tulivu ya Kituo cha Mikutano cha Mfalme Abdul Aziz, mahali ambapo mawaziri kutoka mataifa mbalimbali walikutana Jumamosi kwa picha ya pamoja wakati wa Mkutano wa 11 wa Mawaziri wa Nchi Masikini Zaidi Duniani.

Wakifika kutoka Asia, Afrika na Karibea, mawaziri hawa wote wana sifa moja inayofanana, wanawakilisha nchi zilizo maskini zaidi na zilizo hatarini zaidi duniani, zinazotambuliwa rasmi na Umoja wa Matafa kama nchi zinazoendelea kwa kiwango cha chini sana (LDCs).

Wafanyakazi wanatekeleza jukumu lao katika kiwanda cha uzalishaji nchini Ethiopia.

ILO Photo/Marcel Crozet

Wafanyakazi wanatekeleza jukumu lao katika kiwanda cha uzalishaji nchini Ethiopia.

Ndiyo kwa mshikamano wa kimataifa

“Tunahitaji mabadiliko makubwa ya mwelekeo,” amesema Gerd Müller, Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO, katika hotuba yake ya ufunguzi, akiwakumbusha wanaohudhuria kuwa ujenzi wa viwanda ni “muhimu kwa kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na kujenga uthabiti dhidi ya misukosuko.”

Bw. Müller ameongeza kuwa “Tunahitaji kusema ndiyo kwa mshikamano wa kimataifa, ndiyo kwa mfumo wa kimataifa wa ushirikiano, ndiyo kwa kuzuia pengo kati ya matajiri na maskini kuongezeka zaidi.”

Amebainisha pia kuwa washindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel 500 na wachumi mashuhuri wanazitaka nchi tajiri 20 zijulikanazo kama G20, zinazokutana Afrika Kusini kuchukua hatua. Wataalam hao wameonesha kuwa kati ya mwaka 2000 na 2024, asilimia 1 ya nchi tajiri zaidi duniani zimeongeza utajiri wao kwa asilimia 41, huku nusu ya watu maskini zaidi duniani wakiongeza kwa asilimia 1 pekee.

Bwana. Müller ameonyesha wasiwasi kuwa nchi maskini zaidi duniani zinabaki kuwa dhaifu zaidi dhidi ya mishtuko ya kiuchumi, kuanzia mabadiliko ya tabianchi, ushuru wa biashara, hadi kupunguzwa kwa misaada kutoka mataifa tajiri.

“Kupotea kwa sekta muhimu,” ameonya, “kutakuwa kwa kiwango kikubwa katika maeneo kama nguo, ngozi, biashara ya chakula na vifaa sekta ambazo ni muhimu kwa maisha ya watu na uchumi wa ndani.”

Basher Abdel Rahman Youssef Abdullah mshauri wa vizara ya viwanda na biashara ya Sudan katika mkutano wa LDCMC11

Basher Abdel Rahman Youssef Abdullah mshauri wa vizara ya viwanda na biashara ya Sudan katika mkutano wa LDCMC11

Kujenga uthabiti kupitia viwanda

Dhamira ya UNIDO ni kusaidia nchi kustahimili mishtuko hii na kupitia ujenzi wa viwanda, kuboresha maisha. Nchini Bangladesh, mafunzo ya UNIDO yamewezesha kiwanda cha nguo kufikia viwango vya kimataifa na kutoa ajira kwa mamilioni ya wanawake, nchini Nepal, vijana wanapatiwa ujuzi wa kidijitali na wa upangaji programu, kupunguza pengo la teknolojia.

Wakati huo huo, Sudan inaendeleza sekta ya kilimo-biashara, ikiwalenga wakulima wadogo na wajasiriamali, na kuwawezesha wanawake na vijana kupata fedha ikiandaa sekta binafsi kwa siku za amani na utulivu.

Jumamosi, mafanikio mawili makubwa yalipatikana ambayo ni miongozo ya kuongeza msaada wa UNIDO ikilenga uhamishaji wa teknolojia na ujuzi iliidhinishwa, na mawaziri wakakubaliana kuboresha viwanda vyao, kupata fedha za kutekeleza mipango hiyo, na kuimarisha ushirikiano kulingana na malengo ya Umoja wa Mataifa.

Ahadi zilizotolewa Riyadh zinaashiria hatua muhimu kuelekea kuhakikisha mamilioni ya watu katika nchi zilizo hatarini zaidi duniani wanaweza kustawi katika uchumi wa dunia unaozidi kuunganishwa.

Mtazamo wa ukimbi wa mkkutano wa UNIDO 2025 Riyadhi Saudia

Mtazamo wa ukimbi wa mkkutano wa UNIDO 2025 Riyadhi Saudia

Matokeo ya Mkutano

Mkutano wa 11 wa Mawaziri wa nchi masikini zaidi LDCs umeandaliwa na Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Umoja wa Mataifa UNIDO kwa ushirikiano na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya mwakilishi wa juu wa nchi za LDCs, LLDCs na SIDS (OHRLLS).

  • Tamko la Mawaziri limepitishwa kuthibitisha upya dhamira ya ujenzi wa viwanda jumuishi na mnepo.
  • Mkakati wa Uendeshaji wa UNIDO umeidhinishwa kama ramani ya kuongeza msaada kwa LDCs hadi 2031.
  • Ushirikiano umeimarishwa ni ahadi mpya za ufadhili, kujenga uwezo na uhamishaji wa teknolojia.
  • Sera zimekubaliwa kama uwezeshaji wa vijana, usawa wa kijinsia na mabadiliko ya tabianchi vimetajwa kuwa vipaumbele.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *