Curacao, nchi yenye watu laki na elfu hamsini na nane (158,000) imefuzu Kombe la Dunia litakaloandaliwa kwa pamoja na nchi tatu za Kaskazini mwa Amerika, Marekani, Canada na Mexico.

Nchi hiyo ya visiwa vya bahari ya Caribbean Kusini eneo la Amerika ya kati, ni sehemu ya ufalme wa Uholanzi.

Iliangukia mikononi mwa Uholanzi tangu mwaka 1634 kutoka kwa Hispania ambayo iliitawala tangu mwaka 1499.

Hispania ilipoporwa visiwa hivyo na Uholanzi, vikaendelea kumilikiwa nao hadi sasa vinapofuzu kwa Kombe la Dunia.

Hata hivyo, Waholanzi walishawahi kuporwa mara mbili na Waingereza visiwa hivyo, lakini wakarudishwa.

Kuanzia mwaka 2010, visiwa hivyo vimekuwa na utawala wake wa ndani, chini ya ufalme wa Uholanzi kama sehemu ya Uholanzi iliyoko mbali na Uholanzi.

Mataifa makubwa yaliyojihusisha na ukoloni yanazo nchi za aina hii duniani kote kama ambavyo Ufaransa inamiliki visiwa vya Re Union barani Afrika.

Njia waliyopitia

Curacao iko chini ya shirikisho la soka la bara la Amerika ya Kaskazini, Kati na Caribbean, yaani CONCACAF.

Hili ndilo bara linaloandaa mashindano yajayo ya Kombe la Dunia kupitia wanachama wake watatu; Marekani, Canada na Mexico.

Wenyeji hawa wamepata nafasi ya kufuzu moja kwa moja kama waandaaji, hivyo hawakushiriki michezo ya kufuzu.

Kukosekana kwao kukatoa nafasi kwa nchi zilizobaki kupambania nafasi, ndio Curacao wakaipata.

Wakiwa chini ya kocha mkongwe, Dick Advocaat wa Uholanzi, Curacao wamefaidika sana na sera ya kuwarudisha nyumbani wachezaji wenye asili ya nchi hiyo waliozaliwa Ulaya.

Nahodha Leandro Bacuna na nduguye Juninho Bacuna, Jürgen Locadia, Tahith Chong, Sontje Hansen, na wengine wengi.

Tahith Chong aliwahi kuichezea Manchester United wakati fulani.

Uwepo wao na uwepo kocha mkubwa kama Advocaat kukafupisha safari yao kuelekea nchi ya ahadi.

Curaçao — alama 12

Haiti — alama 9

Saint Lucia — alama 4

Aruba — alama 2

Barbados — alama 1

Zanzibar iamke sasa

Kama tulivyoona hapo juu kwamba Curacao ni sehemu ya ufalme wa Uholanzi, na ilipata hadhi ya kuwa na utawala wake wa ndani kuanzia juzi tu, 2010.

Hadi sasa sio mwanachama wa umoja wa mataifa lakini ilipata uanachama wa FIFA tangu 1932.

Zanzibar ina hadhi ya utawala wake wa ndani tangu Aprili 26, 1964 baada ya Muungano lakini inanyimwa uanachama wa FIFA.

Sifa mojawapo ya kuwa mwanachama wa FIFA ni kuwa nchi huru na kutambuliwa na jumuiya za kimataifa.

Lakini mwaka 1932 wakati FIFA wanaipa uanachama Curacao, nchi ilikuwa bado haina hata utawala wake wa ndani hii sio sifa ya nchi kupata uanachama, lakini walipewa.

Zanzibar inayojitawala yenyewe tangu 1964, ilianza harakati za kutafuta uanachama wa FIFA mwanzoni mwa miaka ya 2000 lakini hadi sasa inahangaika bila mafanikio.

Ikiwa na ligi yake ya ndani, chama chake cha soka, timu yake ya taifa na sifa zote za kuwa mwanachama wa FIFA ikiwemo kuungwa mkono na taifa mama (Jamhuri ya Muungano), bado FIFA hawataki.

Hapa ndipo panapochanganya zaidi kwenye tafsiri ya kanuni za FIFA.

FIFA wamekuwa wakikataa kuipa uanachama Zanzibar kwa kigezo cha kwamba Zanzibar siyo ‘nchi huru’.

Hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 10 ya katiba ya FIFA kuhusu kupata uanachama.

Kanuni hii inaweka sharti kwamba ni lazima anayeomba uanachama atambuliwe na Jumuiya za Kimataifa.

Kipengele cha 6 cha kanuni hiyo kinatoa sharti la nchi hiyo kuungwa mkono na ‘nchi mama’ endapo nchi inayoomba uanachama haijawa nchi huru.

Pale kwenye kutambulika na Jumuiya za kimataifa ndiko kunachowakengeua wengi na kujikuta wakitafsiri tofauti, kwamba ni lazima hiyo nchi iwe mwanchama wa umoja wa mataifa.

Kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa siyo kigezo, Umoja wa Mataifa una wanachama 193 lakini FIFA ina wanachama 211.

Ukiziondoa nchi nne za England, Scotland, Ireland ya Kaskazini na Wales (British Home Nations) zinazolindwa na kipengele cha 5 cha kanuni hii kutokana na heshima ya kuwa waanzilishi wa mpira, FIFA ina wanachama wengine 18 ambao siyo ‘nchi huru’.

Nchi hizi zipo katika mabara yote wanachana wa FIFA kasoro CAF yaani Afrika na CONEMBOL yaani Amerika Kusini.

Nyingi ya nchi hizo zimepata uanachama huku zikiwa haziungwi mkono na ‘nchi mama’, tofauti na Zanzibar inavyoungwa mkono na ‘nchi mama’ Tanzania.

Nitazitolea mfano nchi mbili; Gibraltar na Kosoro, 1kutokana na mikasa yake kuwa ya kipekee na yenye ukakasi.

1. Gibraltar

-Taifa Mama: Uingereza/Hispania.

Tofauti na Zanzibar, Gibraltar ni nchi yenye utata zaidi. Nchi hii iliyopo ndani ya ardhi ya Hispania, ni mali ya Uingereza.

Mataifa haya yapo kwenye mzozo wa miaka na mikaka kuigombania.

Wananchi wake walipiga kura ya maoni 2002 na kuikataa Hispania ili wabaki chini ya Uingereza.

Wakati wa mashindano ya Euro 2024 ambayo England na Hispania zilikutana kwenye fainali, mzozo wa Gibraltar ulirudi tena.

Wachezaji wa Hispania kama nahodha Alvaro Morata na kiungo Jadidi Rodri, walisikika wakisema Gibraltar es Espagnol, kwamba Gibraltar ni ya Hispania.

Wakati wanaomba uanachama wa FIFA, Uingereza iliunga mkono, lakini Hispania ilipinga vikali kiasi cha kutishia kujitoa FIFA.

Hata hivyo, ilipata uanachama wa FIFA 2016.

– Taifa mama: Serbia.

Uanachama wa Kosovo ulipingwa mno na Serbia.

Nchi hii ilijitangazia uhuru wake kutoka Serbia mwaka 2008 huku Serbia ikipinga na kudai nchi bado ni sehemu yake…ilipata uanachama mwaka 2016.

UNAFIKI WA FIFA

FIFA wanasema hawawezi kutoa uanachama zaidi ya mara moja kwa nchi moja, lakini Uingereza imepewa uanachama mara 8 kupitia mataifa kadhaa inayoyamiliki, kutoka mabara tofauti duniani.

1. Gibraltar – ilipata uanachama 2016

AMERIKA KASKAZINI

1. Anguilla – Ilipata uanachama 1996.

2. Bermuda – Ilipata uanachama 1962

3. Visiwa vya Virgin – Vilipata uanachama 1996.

4. Visiwa vya Cayman – Vilipata uanachama 1992.

5. Montserrat – Ilipata uanachama 1996.

6. Visiwa vya Turks & Caicos – vilipata uanachama 1998.

1. Visiwa vya Cook – Vilipata Uluanachama 1994.

Nchi hizo zote zinatumia hati za kusafiria za Uingereza.

Nchi hizi zina mamlaka ya ndani kama Zanzibar lakini tofauti ni kwamba, Zanzibar ina mamlaka makubwa zaidi ya nchi nyingi hapo.

Kuhusu kutambuliwa na Jumuiya za Kimataifa, Zanzibar inatambuliwa vizuri tu.

a) Zanzibar imekaribisha viongozi wengi wa kimataifa wakipigiwa mizinga 21.

b) Zanzibar ina ofisi kadhaa za taasisi za kimataifa zikiwemo balozi za serikali ya kisultan ya Oman, Misri, China, Marekani, Msumbiji, Sweden, Brazil na Norway.

c) Taasisi nyingi za Umoja wa mataifa zina ofisi zake kuu Zanzibar; UNICEF, WHO, ILO na UNFPA.

d) Zanzibar ina mamlaka ya kufanya mahusiano ya kimataifa moja kwa moja kwa mambo yenye maslahi ya moja kwa moja na Zanzibar.

CAF WANAENDELEZA DHULMA

Mwaka 2016 Zanzibar ilipata uanachama wa kudumu wa Shirikisho la soka baranj Afrika, CAF.

Hii ilikuja baada ya kuwa mwanachama kivuli tangu 2004.

Lakini mwaka 2017, uanachama huo ukaondolewa na kurudi ule wa kivuli.

Sababu iliyotolewa ni eti Zanzibar inatakiwa kwanza iwe mwanachama wa FIFA kisha ipate uanachama wa CAF.

Lakini hii ilikuwa sababu ya hovyo na nyepesi sana.

Gibraltar tuliyoijadili hapo juu, ilikutana na chamamoto hizi hizi.

Iliomba uanachama wa UEFA..ikanyimwa. Ilaenda kufungua kesi kwenye mahakama ya usuluhishi wa michezo (CAS).

Wakashinda kesi yao na kupewa uanachama 2013.

Halafu wakaomba uanachama wa FIFA, wakanyimwa, huku Rais wa FIFA wa wakati huo, Sep Blatter, akisema hivi hivi wanavyoambiwa Zanzibar kwamba eti siyo nchi huru.

Wakarudi CAS na kuwashitaki FIFA, wakashinda kesi yao na kupata uanachama 2016.

Zanzibar itumie njia hii. Ipeleke tena maombi yake CAF ikikataliwa, ikafungue kesi CAS.

Halafu ipeleke maombi yake FIFA…ikikataliwa iende tena CAS.

Ni kwa njia hii tu ndio Zanzibar inaweza kupata haki yake ya kuwa mwanachama wa CAF na FIFA!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *