
Musab Abu Tuha ni mshairi na mwandishi wa Kipalestina aliyeshinda *Tuzo ya Pulitzer ya 2025 katika kipengele cha “Maoni ya Kiuandishi” kupitia mfululizo wa makala zenye nguvu zilizoonekana katika jarida la The New Yorker, ambazo ziliweka kumbukumbu ya kina kuhusu mateso ya kila siku ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza wakati wa vita.
Abu Tuha alishiriki katika hafla hiyo kama mwakilishi wa asasi za kiraia, akitoa ushuhuda wa kibinafsi kama mkimbizi aliyeokoka miezi ya mwanzo ya kile alichoeleza kama “mauaji ya halaiki yanayoendelea.” Amesema kwamba alitekwa nyara, kuteswa na kufanyiwa unyanyasaji wa kijinsia na vikosi vya Israeli.
Abu Tuha amesisitiza kuwa Wapalestina hawahitaji mpango mwingine wa amani, bali mpango wa haki unaohakikisha uwajibikaji na haki ya kujitawala. Amesoma mashairi yanayoeleza athari za vita, uharibifu wa nyumba, kupoteza wapendwa, na ukosefu wa mahali salama pa kukimbilia, akihimiza jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za kweli zinazozidi maneno matupu.
Sauti za waandishi wa habari wa Kipalestina
Katika hafla hiyo pia, mwandishi wa habari wa Kipalestina Shuruq Al-Aila mjane wa mwandishi Rushdi Al-Sarraj aliyeuawa Gaza ametoa ujumbe kwa njia ya video kutoka Ukanda wa Gaza ambao amezungumzia mateso anayopitia kama mwandishi wa habari na mama, na kuhusu binti yao aliyekuwa na miezi 11 wakati baba yake alipoawa, na jinsi alivyomwokoa kutoka chini ya vifusi mara mbili.
Ameeleza uhalisia mgumu wa Gaza: mashambulizi ya kila mara, ukosefu wa usalama, kulengwa kwa waandishi wa habari, kuishi kwenye mahema na kupoteza makazi.
Amesisitiza hitaji la haraka la waandishi wa habari wa kigeni kuingia Gaza kuripoti ukweli, akibainisha kuwa vizuizi vipo licha ya usitishaji mapigano. Amesema mateso ya Wapalestina yanaendelea, akitaka sauti yake isikike kama sehemu ya mamilioni ya Wapalestina. Shuruq Al-Aila anaongoza kampuni ya Ain Media, iliyoanzishwa na marehemu mumewe.
Kuuanzisha nchi ya Wapalestina ni haki ya msingi
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema: “Tumejumuika hapa leo kuthibitisha ukweli rahisi: Watu wa Palestina wana haki ya hadhi, haki, na kujitawala. Lakini katika miaka miwili iliyopita, haki hizi zimekiukwa kwa kiwango kisichoaminika.”
Katika ujumbe uliosomwa na mkuu wa ofisi yake, Courtenay Rattray, amesema kuwa makubaliano ya usitishaji mapigano yameleta mwanga wa tumaini. Alisema kupitishwa kwa azimio la Baraza la Usalama kuhusu Gaza ni hatua muhimu katika kuimarisha makubaliano hayo, na kwamba ni muhimu kugeuza kasi ya kidiplomasia kuwa maendeleo ya dharura na yanayoonekana ardhini.
Amesisitiza kuwa UNRWA bado ni njia muhimu ya kuokoa maisha ya mamilioni ya Wapalestina, akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuiunga mkono katika Ukingo wa Magharibi, Gaza, na katika kazi yake kwa wakimbizi wa Palestina katika eneo hilo.
Guterres amesisitiza kuwa kuundwa kwa nchi ya Palestina ni haki ya asili. Amerudia wito wake wa kukomesha uvamizi haramu wa maeneo ya Palestina na kufanya maendeleo yasiyoweza kurejeshwa nyuma kuelekea suluhisho la mataifa mawili, kwa mujibu wa sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa.
“Tusaidie mche wa mzeituni ustawi tena.”
Katibu Mkuu amezungumzia mashambulizi yaliyowakumba Wapalestina wakati wa mavuno ya mizeituni katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu: “Ni vigumu kupuuza kejeli hii: alama ya amani – mti unaotoka Mashariki ya Kati, unaojulikana duniani kote, na uliopo kwenye bendera ya Umoja wa Mataifa sasa unachafuliwa. Ni taswira inayoonyesha jinsi janga hili limezitikisa misingi iliyouongoza umoja wa kimataifa kwa miongo kadhaa. Tumaini linaweza kutimia. Tumaini kwamba watoto wa Kipalestina na Israeli siku moja wataamka katika dunia isiyo na hofu.”
Katika Siku hii ya Kimataifa, ameitaka dunia “kugeuza tumaini hili kuwa hatua, na kuusaidia mti wa mzeituni kustawi tena. Kwa ajili ya haki, utu, na amani.”
Tags: Siku za UN, Gaza, Palestina