Kwa mujibu wa mapendekezo ya mchakato wa uchaguzi, Baraza la Usalama linapaswa kupendekeza jina kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mnamo mwezi Julai mwaka ujao.

Nchi zihamasishe wagombea wanawake

Kanuni hizo zimo katika barua ya pamoja kutoka kwa Rais wa Baraza Kuu na Rais wa Baraza la Usalama, inayozialika Nchi Wanachama kuwasilisha majina ya wagombea. Mgombea atakayechaguliwa ataingia madarakani mwezi Januari 1, 2027.

Uchapishaji wa barua hiyo unaofanywa na chombo chenye wanachama 193, pamoja na Baraza la Usalama lenye wanachama 15, unafungua rasmi hatua ya kupokea uteuzi wa wagombea, na hivyo kuanza kwa mbio za kumtafuta mrithi wa Guterres.

Maandishi hayo yanasisitiza kuwa “kwa masikitiko imebainika kwamba hakuna mwanamke aliyewahi kushika wadhifa wa Katibu Mkuu” na kwamba, kutokana na haja ya kuhakikisha fursa sawa kwa wanawake na wanaume katika nafasi za juu za maamuzi, Nchi Wanachama zinahimizwa “kuzingatia kwa uzito kuwasilisha majina ya wanawake kama wagombea.”

Barua hiyo pia inasisitiza “umuhimu wa uwakilishi wa kikanda katika uteuzi wa makatibu wakuu.” Hadi sasa, kati ya makatibu wakuu tisa waliowahi kuongoza Umoja wa Mataifa, wanne wametoka Ulaya, wawili Asia, wawili Afrika na mmoja Amerika ya Kusini.

Wakati muhimu kwa Umoja wa Mataifa

Katika barua tofauti, Rais wa Baraza Kuu, Annalena Baerbock, amesisitiza kuwa uteuzi wa Katibu Mkuu ajaye unakuja katika kipindi muhimu sana kwa Umoja wa Mataifa na una umuhimu wa kipekee.

Ametaja kipindi cha “migogoro inayoongezeka, janga la tabianchi linalozidi kuwa baya kwa kasi, mahitaji ya kibinadamu yanayoongezeka kila siku, vikwazo vinavyoendelea katika utekelezaji wa Agenda 2030 na Malengo ya Maendeleo Endelevu, pamoja na kuongezeka kwa upinzani dhidi ya haki za binadamu.”

Kwa mujibu wa Baerbock, mfumo wa ushirikiano wa kimataifa “uko katika shinikizo kubwa la kifedha na kisiasa” wakati ambapo dunia “inahitaji zaidi kuliko wakati mwingine wowote” shirika ambalo ndilo pekee linaloweza kuyakusanya mataifa yote, kuchukua hatua katika kiwango cha kimataifa na kwa uhalali wa kisiasa na mamlaka ya kimaadili duniani.

Wagombea waliokwisha jitangaza

Miongoni mwa waliokwisha kutangaza nia ya kugombea ni rais wa zamani wa Chile, Michelle Bachelet; makamu wa rais wa zamani wa Costa Rica, Rebeca Grynspan; na mwanadiplomasia wa Argentina, Rafael Grossi.

Grynspan na Grossi kwa sasa wanafanya kazi ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa. Grynspan anaongoza Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo UNCTAD. Naye Grossi ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, IAEA.

Bachelet aliwahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake, UN Women na pia Rais wa Chile mara mbili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *