Mwanaharakati huyo mwenye umri wa miaka 26 raia wa Zimbabwe, Namatai Kwekweza mshindi wa mwaka huu wa Tuzo ya Afrika inayotolewa na Ujerumani alipokea Tuzo hiyo mbele ya hadhira teule iliyokusanyika mjini Berlin siku ya Jumatano.
Jopo huru la wanachama 20 limesema harakati za Kwekweza zinatoa ujumbe mkubwa wa kujiamini kuelekea kuifufua demokrasia. Binti huyo aliibuka kidedea kutoka kwa zaidi ya wateule 28 waliofanikiwa kuingia kwenye kinyang’anyiro cha mwisho cha kumsaka mshindi.
Katika hotuba yake kwenye sherehe hiyo, Rais wa Bunge la Ujerumani, Julia Klöckner alimsifu Kwekweza kwa kuchochea demokrasia na utawala wa sheria nchini mwake.
Akiwa na umri wa miaka 18, Namatai Kwekweza alianzisha shirika la WELEAD Trust, linalowafunza viongozi vijana na linawashirikisha katika michakato ya kufanya maamuzi ya kisiasa.
Mwakilishi wa kizazi kipya
Alipoulizwa jinsi alivyojihisi baada ya kupokea tuzo hiyo ya heshima kubwa, Kwekweza aliisifu jamii yake na wenzake wa shirika la WELEAD Africa ambao amesema ndio nguvu kubwa iliyo nyuma yake.
Kwekweza amesema tuzo yake ni kwa ajili ya vijana wote wanaosimama imara na wanaolipa gharama kubwa kwa kutetea demokrasia.
Katika hali ya ukandamizaji inayozidi kuongezeka nchini Zimbabwe, Kwekweza anapigania utawala wa sheria na ushiriki sawa wa kisiasa. Amejihatarisha kwingi kwa ajili ya hili: Amekamatwa mara kadhaa na ameripoti juu ya mateso na vitisho dhidi yake lakini amesema havunjiki moyo kwa sababu kila mafanikio yana gharama yake.
Mwenyekiti wa baraza la majaji kwenye Jopo huru, Claus Stäcker, ambaye ni Mkurugenzi wa Idhaa za Afrika za Deutsche Welle, ameelezea kwamba kasi ya hivi karibuni katika uanaharakati wa vijana barani Afrika imechochea maamuzi ya baraza hilo la majaji.
“Kote barani Afrika, vijana wamejitolea kushiriki, kuhakikisha uwazi, na mabadiliko ya kijamii, kama vile harakati za hivi karibuni za maandamano ya Kizazi cha GenZ nchini Kenya, Madagasca, Cameroon na Tanzania, zinavyoonyesha. Na binti huyi Namatai Kwekweza ni mfano mkubwa wa kizazi hicho kipya cha wanademokrasia ambao sio tu wanapinga jambo fulani bali kwa ujasiri wanachukua majukumu ambayo yanaunda mustakabali wa nchi zao.”
Majaji wa Jopo huru la Tuzo ya Ujerumani kwa Afrika, Namatai Kwekweza, ni mfano wa kuigwa na kizazi kipya cha wanademokrasia, wanaochukua majukumu kwa ujasiri na hivyo kusaidia kujenga mustakabali mzuri wa nchi zao.
Tuzo hiyo ni utambuzi wa juu zaidi wa Wajerumani kwa Waafrika. Inatolewa na Wakfu wa German Africa – wakfu usioegemea upande wowote uliojitolea kukuza taswira bora bora ya bara la Afrika kwenye uwanja wa kisiasa miongoni mwa umma wa Wajerumani.
Tangu mwaka 1993, imewatunukia Tuzo hiyo watu kutoka bara la Afrika ambao wametoa mchango wa kipekee kwa demokrasia, amani, haki za binadamu, maendeleo endelevu, utafiti, sanaa, utamaduni, na pia masuala ya kijamii barani Afrika.
Mwaka jana, Meya wa mji mkuu wa Sierra Leone, Freetown, Yvonne Aki-Sawyerr, alipokea tuzo hiyo. Wapokeaji wengine ni pamoja na watafiti wa COVID, Tulio de Oliveira na Sikhulile Moyo, Rais wa zamani wa Botswana Ketumile Masire na wanaharakati wa Somalia Waris Dirie na Ilwad Elman.