Wajumbe hao wapya  wa tume ni Srinivasan Muralidhar kutoka India, Florence Mumba kutoka Zambia, na Chris Sidoti kutoka Australia ambao wanakuja na uzoefu mpana wa sheria na haki za binadamu.

Jaji Muralidhar atakuwa Mwenyekiti wa Tume, huku Sidoti akiteuliwa tena baada ya kuhudumu hapo awali. “Hawa ni watu wenye uadilifu wa kipekee na uzoefu mkubwa,” amesema Lauber. “Uongozi wao utakuwa muhimu wakati Tume ikiendelea na kazi yake muhimu.”

Wajibu wa Tume hiyo

Tume ilianzishwa kupitia azimio S-30/1 la Baraza la Haki za Binadamu mwaka 2021, lililotaka “kuanzishwa kwa dharura kwa tume huru, ya kimataifa na endelevu ya uchunguzi” ili kuchunguza madai ya ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu katika eneo hilo tangu tarehe 13 Aprili 2021. Wakati huo, Baraza liliweka wazi umuhimu wa kuchunguza wahusika wote katika mgogoro huo.

“Jumuiya ya kimataifa lazima ikabili ukiukaji popote pale unapofanyika,” limesema Baraza la Haki za Binadamu katika azimio lake la awali.

Kuchunguza sababu za msingi, ubaguzi na ukandamizaji

Zaidi ya kuweka kumbukumbu za madai ya ukiukaji, Tume pia imepewa jukumu la kuchunguza sababu za msingi za mivutano ya mara kwa mara katika eneo hilo. Majukumu yake yanajumuisha uchunguzi wa “ubaguzi na ukandamizaji wa kimfumo unaotokana na utambulisho wa kitaifa, kikabila, rangi au dini.”

Tume inatakiwa kuwasilisha ripoti kila mwaka kwa Baraza la Haki za Binadamu na kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

“Kuelewa chanzo cha mgogoro ni muhimu katika kujenga njia ya kuelekea amani endelevu,” amesema afisa mmoja wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa.

Majukumu yalioongezwa baada ya machafuko ya Gaza

Baraza la Haki za Binadamu lilipanua wigo wa Tume kupitia maazimio ya ziada mwaka 2024, likiielekeza kuandaa ripoti kuhusu walowezi wa Kiyahudi na kuhusu uuzaji wa silaha ikijumuisha zile zilizotumika katika operesheni ya kijeshi ya Israel huko Gaza baada ya 7 Oktoba 2023.

Katika ripoti yake ya hivi karibuni, iliyotolewa Septemba 2025, Tume ilihitimisha kwamba Israel ilitenda makosa ya jinai ya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza ikiwa ni mara ya kwanza kwa chombo cha Umoja wa Mataifa kutoa hitimisho kama hilo.

“Haya ni matokeo mazito na yenye athari kubwa,” amesema Chris Sidoti baada ya kuteuliwa tena. “Wajibu wetu ni kuendelea kuweka kumbukumbu za ukweli kwa kujitegemea na kwa weledi.”

Wasifu wa wajumbe wapya wa Tume ya Uchunguzi

Jaji Srinivasan Muralidhar, aliyewahi kuwa Jaji Mkuu wa Mahakama Kuu ya Orissa, ana historia ndefu ya utetezi wa haki za binadamu na mageuzi ya mahakama nchini India, ikiwemo kufanya kazi na Tume ya Haki za Binadamu ya India na Tume ya Sheria ya India.

Jaji Florence Mumba wa Zambia ana uzoefu wa miongo kadhaa katika mahakama za kitaifa na kimataifa, ikijumuisha kazi muhimu katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kwa Yugoslavia ya zamani, ambako alichangia jitihada za kutambua ubakaji kama uhalifu wa kivita.

Chris Sidoti, wakili wa haki za binadamu kutoka Australia, ametoa ushauri kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa zaidi ya miaka ishirini na ni mwanzilishi mwenza wa Baraza Maalum la Ushauri kuhusu Myanmar.

“Kila mmoja wetu amejitolea kutetea sheria bila woga wala upendeleo,” amesema Mumba. “Haki inahitaji tusimame imara.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *