
Katika hali ambayo imeibua sintofahamu katika soka la Afrika, timu ya taifa ya Cameroon imewaweka kando nyota wake wawili wenye uzoefu, André Onana na Vincent Aboubakar, katika kikosi cha mwisho kilichotangazwa kwa ajili ya Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.
Uamuzi huo unaashiria mtikisiko mkubwa kwa Cameroon, kabla ya mashindano hayo makubwa ya soka barani Afrika.
Kukosekana kwa Onana, kipa ambaye amecheza katika klabu kubwa za Ulaya na Aboubakar, mkongwe anayecheza katika nafasi ya ushambuliaji na nahodha wa muda mrefu, kunaashiria mwelekeo mpya chini ya uongozi wa timu uliorekebishwa.
Orodha ya kikosi hicho cha Cameroon pia inaonyesha mabadiliko makubwa ya vizazi huku wachezaji wachanga na ambao hawajaimarika zaidi wakipewa nafasi ya kuhusika kabla ya michuano hiyo nchini Morocco.
Kikosi hicho cha Cameroon katika Fainali za AFCON kitakuwa chini ya Kocha Mkuu, David Pagou ambaye amechukua nafasi hiyo kutoka kwa Marc Brys aliyetimuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Cameroon (FECAFOOT).
Cameroon pia haijamjumuisha nyota wa Napoli, Zambo Anguissa ambaye alikosa mechi za mwezi uliopita za kuwania kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Cameroon na Nigeria kutokana na majeraha.
Kikosi cha Cameroon kwa ajili ya AFCON 2025 kinaundwa na makipa Devis Epassy (Dinamo Bucharest), Simon Omossola (St Eloi Lupopo), Simon Ngapandouetnbu (Montpellier) na Edouard Sombang (Colombe Du Dja).
Mabeki ni Samuel Kotto (Gent), Gerzino Nyamsi (Lokomotiv Moscow), Jean-Charles Castelletto (Al-Duhail), Nouhou Tolo (Seattle Sounders), Flavien Enzo Boyomo (Osasuna), Mahamadou Nagida (Rennes), Christopher Wooh (Spartak Moscow), Junior Tchamadeu (Stoke City) na Darlin Yongwa (FC Lorient).
Katika eneo la kiungo walioitwa ni Martin Ndzie (Rapid Vienna), Carlos Baleba (Brighton), Arthur Avom (FC Lorient), Eric-Junior Dina Ebimbe (Brest), Brice Ambina (Valerenga), Jean Junior Onana (Genoa) na Olivier Kemen (Istanbul B.B).
Washambuliaji ni Bryan Mbeumo (Manchester United), Christian Bassogog (Al-Okhdood), George-Kevin N’koudou (Al-Diriyah), Danny Namaso (Auxerre), Frank Magri (Toulouse), Karl Etta Eyong (Levante), Christian Kofane (Bayer Leverkusen) ma Patrick Soko (Almeria).
Salah kuongoza jahazi Misri
Kwa upande mwingine, Misri imetangaza kikosi chake kwa ajili ya AFCON 2025 ambacho kitaongozwa na nyota wa Liverpool, Mohamed Salah.
Kocha Hossam Hassan ameteua washambuliaji watatu tu asilia wa kati ambao wataongozwa na nyota wa Nantes, Mostafa Mohamed.
Wanaounda kikosi cha Misri ni makipa Mohamed El Shenawy (Al Ahly), Ahmed El Shenawy (Pyramids), Mostafa Shobeir (Al Ahly) na Mohamed Sobhi (Zamalek).
Kuna mabeki tisa katika kikosi hicho ambao ni Mohamed Hany (Al Ahly), Ahmed Eid (Al Masry), Ramy Rabia (Al Ain), Khaled Sobhi (Al Masry), Yasser Ibrahim (Al Ahly), Mohamed Ismail (Zamalek), Hossam Abdel-Maguid (Zamalek), Mohamed Hamdy (Pyramids) na Ahmed Fatouh (Zamalek).
Viungo ni Marwan Attia (Al Ahly), Hamdi Fathi (Al Wakrah, Qatar), Mohannad Lasheen (Pyramids), Mahmoud Saber (Zed), Mohamed Shehata (Zamalek), Emam Ashour (Al Ahly), Ahmed Mostafa Zizo (Al Ahly), Mahmoud Hassan Trezeguet (Al Ahly), Ibrahim Adel (Al Jazira), Mostafa Fathi (Pyramids), Omar Marmoush (Manchester City) na Mohamed Salah (Liverpool).
Wachezaji wa nafasi ya ushambuliaji ni Mostafa Mohamed (Nantes), Salah Mohsen (Al Masry) na Osama Faisal (Al Ahly Bank).