Katika ripoti yake, Amnesty International imesema, mashambulizi ya siku nyingi ya RSF dhidi ya kambi ya Zamzam yalihusisha mauaji ya kiraia, utekaji nyara na uharibifu wa misikiti, shule na kliniki za afya, na kwamba lazima uharibifu huo uchunguzwe kama uhalifu wa kivita.

Katibu mkuu wa shirika hilo la Amnesty International Agnès Callamard, amesema mashambulizi hayo ya makusudi na ya kutisha ya RSF dhidi ya raia waliokata tamaa na wenye njaa katika kambi ya Zamzam yalifichua kwa mara nyingine tena hali ya kutojali maisha ya binadamu.

Ameongeza kusema shambulizi hilo halikuwa la kipekee.

Ripoti hiyo ya Amnesty ni ya hivi karibuni zaidi ya shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu kushtumu ukatili uliofanywa na kundi la RSF katika vita hivyo vya takriban miezi 30.

Ukatili huo umejumuisha mauaji ya watu na ubakaji katika miji na vijiji hasa Darfur.

Jeshi la Sudan pia limeshtumiwa kwa ukatili katika vita hivyo.

Amnesty International yaikosoa UAE

Amnesty pia imeukosoa Umoja wa Falme za Kiarabu, kama ilivyofanya awali, juu ya madai ya kuliunga mkono kundi hilo la RSF. Callamard, ameiambia AP kwamba Amnesty ilirekodi kuwa Umoja huo wa Falme za Kiarabu uliendelea kuiunga mkono RSF ikijuwa wazi kwamba kundi hilo la wanamgambo lilikuwa likifanya uhalifu wa kivita.

DW- Mahojiano | Carl Skau
Naibu mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP Carl Skau katika mahojiano na DW mnamo Mei 6, 2024 mjini BerlinPicha: DW

RSF haikujibu mara moja ombi la tamko kuhusu matukio hayo lakini kufuatia shambulio hilo, kundi hilo lilidai kuwa kambi hiyo ya Zamzam ilitumiwa na jeshi pamoja na wanamgambo washirika wake, na kuongeza kuwa wapiganaji wake pia hawakuwalenga raia.

WFP yaonya kuhusu uhaba wa chakula Sudan

Naibu mkurugenzi mtendaji wa WFP Carl Skau, amesema changamoto ya kufikia baadhi ya maeneo, kama vile el-Fasher, jiji kubwa katika eneo la magharibi la Darfur, bado ni suala kuu linapaswa kuangaziwa ili kuwashughulikia wakimbizi.

”Tunapoweza kuyafikia, tunafanikiwa kuwashughulikia na kuokoa maisha. Lakini maeneo mawili karibu na Kadugli huko Kordofan na el-Fasher ni maeneo mawili ambayo hatujaweza kufikia, kwa hivyo ufikiaji ndio suala kuu.”

Skau pia amesema kwasasa wanatumaini kwamba hatua ambazo wamekuwa wakipiga kuwafikia watu katika kipindi cha mwaka uliopita, hazitafifia kwasababu ya mabadiliko katika mgogoro huo na siasa kwasasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *