
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Leo XIV amesema, chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) barani Ulaya mara nyingi huchochewa na wale wanaotaka kuwatenga watu wa imani na mbari tofauti na zao.
Akizungumza na waandishi wa habari ndani ya ndege, wakati anarejea Vatican jana Jumanne kutoka kwenye ziara yake ya kwanza rasmi nje ya nchi ya kuzitembelea Uturuki na Lebanon, Papa Leo amesisitiza kuwa, kuishi pamoja kwa masikilizano Wakristo na Waislamu nchini Lebanon kunatoa masomo kwa Ulaya na Amerika Kaskazini, na kwamba, kuwa na mazungumzo ya dhati na ya kuheshimiana ndiyo njia inayopasa kufuatwa.
Alipoulizwa na mwandishi mmoja wa habari kuhusu imani waliyonayo baadhi ya Wakatoliki kwamba Uislamu unatishia utambulisho wa Kikristo wa ulimwengu wa Magharibi, kiongozi huyo wa kanisa katoliki amesema:
“Ninajua kwamba wakati mwingine, hofu hizo zipo barani Ulaya, lakini mara nyingi huchochewa na wale wanaopinga uhamiaji na wanaojaribu kuwatenga watu wanaotoka nchi nyingine, wa dini nyingine, au asili nyingine ya kimbari.”
Amesisitiza kuwa, bila shaka yoyote mazungumzo na urafiki kati ya Waislamu na Wakristo ni mambo yanayowezekana.
“Nadhani moja ya masomo makubwa ambayo Lebanon inaweza kuufundisha ulimwengu ni kwamba, hiyo ni nchi ambayo Uislamu na Ukristo zipo na zinaheshimiwa, ambapo kuishi pamoja na urafiki vinawezekana.”
Papa Leo ameendelea kueleza: “simulizi tulizozisikia katika siku mbili zilizopita, ushuhuda wa Waislamu na Wakristo wanaosaidiana hata katika vijiji vilivyoharibiwa, ni masomo muhimu ambayo inapasa yasikike pia Ulaya au Amerika Kaskazini. Pengine tungepaswa tupunguze hofu kidogo na kutafuta njia za kukuza mazungumzo ya kweli na kuheshimiana baina ya pande mbili”…/