Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio linalotangaza kuwa, kuendelea Israel kuikalia kwa mabavu na kuiunganisha na upande wake Miinuko ya Golan ya Syria ni “kinyume cha sheria” na limeutaka utawala huo uondoke kikamilifu katika eneo hilo hadi kwenye mstari wa mpaka wa Juni 4, 1967.

Rasimu ya azimio hilo ambayo iliwasilishwa na Misri, ilipitishwa jana Jumanne kwa kura 123 zilizounga mkono, saba zilizopinga na 41 za nchi zilizojizuia kupiga kura.

Azimio hilo linasema, uamuzi wa Israel wa Desemba 14, 1981 wa kuweka “sheria, mamlaka ya mahakama na utawala wa kiuendeshaji” kwenye Miinuko ya Golan ya Syria inayokaliwa kwa mabavu “ni batili na hauna uhalali wa namna yoyote.”

Azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa “limeitaka tena Israel iondoke kwenye Miinuko yote ya Golan ya Syria inayoikalia kwa mabavu hadi kwenye mstari wa Juni 4, 1967 ukiwa ni utekelezaji wa maazimio husika ya Baraza la Usalama,” na kuongeza kuwa, kuendelea uvamizi na ukaliaji wa ardhi kwa mabavu unaofanywa na Israel na kuliunganisha eneo hilo na upande wake kwa hakika ni “kizuizi kinachokwamisha kufikiwa amani kamili, ya haki, na ya kudumu katika eneo”.

Mwakilishi wa Syria katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Ibrahim Alali, alisisitiza jana hiyohiyo kwamba, Miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu ni eneo la Syria, na akatilia mkazo haki ya nchi yake kurejesha kikamilifu udhibiti wake kutoka kwa Israel.

Utawala wa kizayuni wa Israel umekuwa ukiikalia kwa mabavu Miinuko ya Golan tangu mwaka 1967, na sasa ulipanua zaidi wigo wa ukaliaji kwa mabavu wa ardhi ya Syria hadi kwenye eneo la kizuizi cha baina ya pande mbili na Mlima Hermon huko kusini mwa nchi hiyo baada ya kuanguka utawala wa Bashar al Assad.

Baadaye utawala huo ghasibu ulitangaza kuwa, makubaliano ya mwaka 1967 yaliyofikiwa kati ya pande hizo mbili yalivunjika kwa kuangushwa utawala wa Assad…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *