MOROGORO: SERIKALI kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) kupitia ufadhili wa Pandemic Fund imeendelea kutoa mafunzo maalumu ya kuijengea uwezo timu ya kitaifa ya magonjwa ya dharura na maafa kwa ajili ya utayari wa kukabiliana nayo.
Mkurugenzi wa Huduma za Dharura na Maafa, Dk Erasto Sylvanus, amesema hayo mjini Morogoro wakati akifunga mafunzo ya kujenga uwezo wa timu ya kitaifa itakayotoa matibabu ya magonjwa ya kipindi cha dharura na maafa (EMT 10 Steps and EMTCC).

Dk Sylvanus amesema ni muhimu kwa wataalamu waliopata mafunzo hayo kutumia maarifa na ujuzi walioupata kuimarisha taasisi walizotoka na kuhakikisha wanaendelea kuzingatia viwango, miongozo na taratibu za kitaifa na kimataifa, kupanga, kutekeleza na mwitikio wa huduma za dharura na maafa.
Amewataka wataalamu hao kuwa tayari wakati wote kuitumikia nchi pale watakapohitajika ndani na nje ya nchi wakizingatia uzalendo, nidhamu, weledi na kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa kama timu.
“Mnatakiwa kutambua kuwa wanapokuwa katika majukumu ya dharura wanaiwakilisha Tanzania pamoja na Wizara ya Afya , hivyo mnapaswa kulinda heshima na taswira yake,” amesisitiza Dk Sylvanus.
Dk Sylvanus pia amewataka waratibu wa mafunzo kuanzisha na kuhuisha kanzidata ya wataalamu wa timu za dharura za afya ili kusaidia kupanga na kuratibu rasilimali watu kwa ufanisi wakati wa matukio ya dharura.
Naye Ofisa wa WHO hapa nchini, Dk Janeth Masuma, amesema WHO kupitia ufadhili wa Pandemic Fund ikishirikiana na Serikali ya Tanzania pamoja na wadau wengine wakiwemo Centre of disease Control (US CDC), Center for International Health , Education and Biosecurity- Tanzania (CIHEB) na Medecins sans Frontieres (MSF) ambao ni Madaktari Wasio na Mikapa wamefwezakufanikisha mafunzo hayo muhumu.
Hivyo ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuimarisha mifumo ya utayari na mwitikio wa dharura za afya nchini kupitia uwekezaji wa kujenga uwezo wa wataalamu wake wa sekta ya afya .
Dk Masuma amesema Tanzania ni nchi ya 27 Afrika kuanzisha timu ya kitaifa ya magonjwa ya dharura na maafa, ambayo kwa sasa ipo thabiti ,uwezo na utayari wakati wowote wa kukabiliana na magonjwa ya dharura na maafa kwa haraka na kuwezesha kupunguza vifo.

“Kipindi hiki ambacho kumekuwa na matishio ya ugonjwa wa Ebora katika nchi za jirani, Tanzania ipo tayari kukabiliana na ugonjwa huo na magonjwa mengine ya dharura na maafa,” amesema Dk Masuma.
Kwa upande wake Mratibu wa mafunzo hayo kutoka kitengo cha dharura na maafa katika Wizara hiyo, Dk Erick Richard amesema mafunzo hayo yalianza kutolewa mwaka 2025 kwa awamu tatu tofauti.
“Kutokana na utaratibu uliowekwa na WHO katika utoaji wa huduma za dharura timu hii haitakuwa ya kitaifa tu bali inaweza kutumika hata nje ya nchi endapo itahitajika,” amesema Dk Erick.