Utawala wa nchi, unaundwa na mihimili mitatu rasmi ya Serikali, Bunge na Mahakama na mhimili wa nne usio rasmi, huu ni mhimili wa vyombo vya habari, kwa lugha ya kisasa ni media.

Ile mihimili mitatu rasmi inaheshimiwa, inaangaliwa, inajaliwa, inatunzwa na kulipana mishahara minono na posho za kueleweka huku huu mhimili wa nne, wa media, tukiachwa kupambana na hali yake kama mtoto yatima, na siku tukilipwa posho ni viposho fulani kiduchu, tena hulipwa kama huruma ama hisani na sio stahiki. 

Siku zote viongozi wetu wakiwemo viongozi wakuu wakihutubia, hutusifu sana sisi media na kuelezewa jinsi tulivyo sekta muhimu, na kutueleza kwa kauli nzuri nzuri jinsi tunavyothaminiwa, ila kuthaminiwa huko ni kwa maneno matupu. Tushukuru Mungu, angalau dalili za kuthaminiwa zimeanza kuonekana.

Mhimili huu wa nne ndio kiungo muhimu cha upashanaji habari kati ya mihimili ile mitatu na wananchi. Mihimili hiyo mitatu, ya Serikali, Bunge na Mahakama, kazi yake ni kutoa tu habari na sisi wanahabari tunazitangaza, hivyo zinawafikia wananchi. 

Umuhimu wa mhimili wa nne ni sisi, ndio tunaongea na wananchi, wanatueleza shida zao, mahitaji yao na wanataka nini, na sisi tunaandika au tunatangaza na kuifikishia ile mihimili mitatu ili wazifanyie kazi hoja za wananchi.

Lakini kwa kilichotokea Oktoba 29, kinaonyesha Serikali na viongozi hawatusomi au hawatusikilizi na kama wanasoma na kutusikiliza, basi wanatupuuza, na kile kilichotokea October 29 ni matokeo ya mapuuza hayo.

Laiti kama ngazi za uamuzi, zingetusikiliza, wananchi ambao ndiyo wenye nchi, wanataka nini, naamini kabisa tusingelifika hapa tulipofika kwa sababu sisi media tulisema kila kitu, nikiwemo mimi kupitia kalamu yangu, kwa kutoa ushauri wangu wa kifanyike nini katika uchaguzi mkuu wetu ili uchaguzi huo uwe huru, kweli na wa haki, lakini hatukusikilizwa.

Karibu watu wote wanajadili tu matokeo ya kilichotokea badala ya kujadili chanzo na kisababishi. 

Tanzania kama nchi, tumejikwaa mahali, tukaanguka chini, badala ya kuangalia tulipojikwaa, tunaishia kuangalia tulipoangukia tu, hivyo kuna hatari, tukifika tena pale tulipojikwaa kwa tishio la maandamano mengine ya tisa Desemba, tusije tukajikwaa tena tukaanguka tena.

Angalau sasa, baada ya kutokea kilichotokea Oktoba 29, 2025, sasa serikali yetu imeamka usingizini na kutukumbuka media kwa kutupa umuhimu stahiki ili kuzuia kilichotokea kisije kujirudia. 

Nianze na pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua mwanahabari nguli, Tido Mhando kuwa mshauri wake wa habari, hivyo sasa Rais atashauriwa kuhusu habari, Rais akisikia ni Serikali imesikia.

Pia, nimpongeze kwa kumteua mwanahabari nguli mwingine, Bakari Machumu kuongoza Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu na kitu cha kwanza ni Bakari Machumu kutuita wahariri Ikulu na kusemezana nasi na Alhamdidulahi, alituangalia vizuri.

Tunamuomba Machumu, kupitia kwa Katibu Mkuu Kiongozi, kuandika waraka kwa taasisi zote za umma kutoa maelekezo ya jinsi ya kuwaangalia wanahabari kama tulivyoangaliwa pale Ikulu. 

Nisiache kumshukuru Rais Samia kuturudishia Profesa Palamagamba Kabudi kuendelea na Waziri wa Habari na kututeulia manaibu waziri wawili, Hamis Mwinjuma ‘MwanaFA’ na Paul Makonda, hawa ni vipenzi vya wanahabari. 

Pia, nimpongeze Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba kuanza na sisi sekta ya habari, tuwaelimishe Watanzania na hasa Gen Z kuwa Tanzania ni mali ya Watanzania wote wala si ya Serikali au chama cha siasa na hivyo kila mmoja anapaswa kuilinda.

“Tanzania si mali ya Serikali, Tanzania si mali ya chama cha siasa na vyama vya siasa vipo kwa sababu nchi ipo. Tuilinde nchi yetu. Mungu ametupa nchi nzuri na kila mmoja ana wajibu wa kuilinda,” amesisitiza.

Waziri Mkuu aliyasema hayo Novemba 25, 2025 wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari nchini katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam. 

Amesema fedha zinazotumika kujenga miundombinu ya barabara, zahanati, vituo vya afya, miradi ya maji ni za Watanzania na wala si za Serikali. “Hakuna fedha ya Serikali kwenye miradi. Fedha yote inayotekeleza miradi ni yako Mtanzania isipokuwa inasimamiwa na Serikali.”

Amesema kila Mtanzania anachangia pato la Taifa na anajinyima aina fulani ya maisha ili kujenga barabara au zahanati kwenye eneo lake. “Ukinunua shati kuna sehemu unapeleka kujenga barabara, unakuwa umetenga sehemu ya kutumia na sehemu umejinyima ili kuchangia maendeleo ya nchi.”

Mkutano huo ulihudhuriwa na mawaziri na naibu mawaziri kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja viongozi wa Jukwaa la Wahariri (TEF).

Kama serikali ingesoma media tulichoshauri kuhusu uchaguzi, ikatekeleza ushauri wetu, yaliyotokea yasinge tokea. Maji yameishamwagika, yaliyopita si ndwele, tugange yaliyopo na yajayo.

Ilmradi sasa Serikali imeonyesha kutujali, itujali kweli kama vyama vya siasa ambavyo kazi yake ni kupiga siasa, vinapewa ruzuku, nini kinashindikana kwa media pia lupewa ruzuku na kulipwa posho nene na nono kama ile mihimili mitatu ambayo ni rasmi?

Media tukisikilizwa, mkitujali, tutalisaidia taifa na kutimiza majukumu yetu kikamilifu kama mhimili wa nne usio rasmi. 

Tukiamua tunaweza. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *