Ndani ya kauli iliyojipatia sifa mbaya kupitia mitandao ya kijamii katika siku zile za joto kali a Julai 2021, Ngizwe Mchunu aliyekuwa ameondolewa kazini kama DJ wa redio, alirusha bomu la kisiasa lililoacha alama isiyofutika katika maisha yake.

Kwa kiwango kikubwa kauli hiyo ikabadilisha mwelekeo wa mazungumzo ya taifa la Afrika Kusini lililokuwa tayari limegawanyika vipande vipande.

Machafuko hayo ya Julai 2021 yalikuwa miongoni mwa matukio ya vurugu kubwa zaidi katika historia ya Afrika Kusini, baada ya kumalizika kwa enzi ya ubaguzi wa rangi.

Yalianza kama mlipuko wa hasira kutokana na kufungwa jela kwa Jacob Zuma, Rais wa zamani wa Afrika Kusini kwa kosa la kudharau mahakama.

Rais huyo wa zamani alikuwa amekaidi agizo la Mahakama ya Kikatiba la kufika mbele ya Tume ya Zondo iliyokuwa ikichunguza matumizi mabaya ya madaraka.

Wafuasi wake, wengi wao wakitoka KwaZulu-Natal na Gauteng walimiminika mitaani. Kilichofuata hakikuwa maandamano ya kawaida bali kuvunjika kwa utaratibu wa kijamii. Maduka makubwa yakaporwa, maghala yakavunjwa na kuachwa tupu. Mnyororo mzima wa usambazaji huduma na bidhaa ukaharibiwa.

Katikati ya hali hyo, ndipo Mchunu, mwanaharakati aliyejijengea taswira ya ‘mlinzi wa utamaduni’ na mfuasi wa karibu wa Rais wa zamani, Jacob Zuma alilipua bomu hilo.

Takribani watu 354 walipoteza maisha. Uchumi wa Afrika Kusini ulipata hasara iliyokadiriwa kufikia Rand 50 bilioni (Sh7.8 trilioni) na takribani ajira 150,000 zilipotea, nyingi miongoni mwa hizo hazikurudi tena.

Kabla ya mlipuko wa vurugu, Mchunu alikuwa amechapisha mfululizo wa video mitandaoni akimpa Rais Cyril Ramaphosa amri ya mwisho ambayo ni kali; amwachie huru Zuma kutoka gerezani, la sivyo nchi ikabiliane na matokeo yake.

Video hizo hazikuwa za mafumbo. Zilisemwa kwa ukali wa mtu aliyekuwa ameishi maisha ya utangazaji kwa miaka mingi na anayejua jinsi ya kuvuta usikivu wa umma.

Mchunu kabla ya kukamatwa kwa Zuma, alionekana akipiga kambi nje ya makazi ya Nkandla, KwaZulu-Natal, akisisitiza kwamba Zuma hatafungwa kamwe. Lakini alipofungwa, hasira ya Mchunu ilivuka mipaka.

Julai 19, 2021, Mchunu alijisalimisha kwa polisi wa KwaZulu-Natal. Alishtakiwa kwa kuchochea vurugu za umma na kuvunja Sheria ya Usimamizi wa Majanga.

Awali, alinyimwa dhamana kwa hoja kwamba alikuwa na uwezekano wa kutoroka na akanyang’anywa pasi yake ya kusafiria. Baadaye Mahakama ya Hakimu Mkazi Randburg ikaona ana kesi ya kujibu.

Akawa miongoni mwa majina makubwa yaliyoangaziwa katika tuhuma za kuchochea machafuko, akishtakiwa pamoja na wengine kadhaa, akiwamo mwanaharakati wa Fees Must Fall, Bonginkosi Khanyile na diwani wa African National Congress (ANC), Clarence Tabane.

Kukamatwa kwake kulizaa uhusiano usiotarajiwa kati yake na Khanyile. Siku Mchunu alipofika mahakamani Randburg, Khanyile ambaye wakati huo alikuwa kiongozi wa MK Party Youth League, alisimama nje na kuzungumza na vyombo vya habari kwa niaba ya familia ya Mchunu, akisisitiza kuwa Mamlaka ya Taifa ya Mashtaka (NPA) haina msingi wa mashtaka dhidi yake.

Safari ya kisheria ilikuwa ndefu, kesi ilivutwa mahakamani kwa miaka, ikiahirishwa mara kwa mara, tarehe za kusikilizwa zikibadilishwa na kupangwa upya.

Hakimu aliyemwachia Mchunu kwa dhamana alibainisha wazi kuwa ushahidi dhidi yake ulikuwa dhaifu. Hatimaye, akaachiwa huru.

Lakini uzoefu huo wa kukamatwa, kufungwa na miaka ya kusubiri hatima mahakamani haukumfanya awe mnyenyekevu; badala yake ulizidishia msimamo wake mkali.

Mwaka 2024 na 2025, Mchunu akakutana na sababu mpya; uhamiaji usio halali. Nchi ilikuwa ikikabiliana na siasa za uhamiaji kwa miongo kadhaa. Vurugu za kibaguzi dhidi ya wageni mwaka 2008 zilisababisha vifo vya watu 62. Kulifuatia milipuko mingine mwaka 2015 na 2019. Kila mara serikali iliahidi kuchukua hatua, ahadi zilizopotea hewani.

Mamilioni ya Waafrika Kusini wakiangalia ukosefu wa ajira ukifikia takriban asilimia 40, wakiangalia biashara nyingi zikiendeshwa na raia wa kigeni na fursa zao za kiuchumi zikizidi kupungua, walijikuta katika hasira isiyo na mahali pa kwenda wala mtu wa kuzieleza. Mchunu akawa sauti yao.

Chombo chake kilikuwa ‘Amabhinca Nation’ harakati iliyojikita katika utambulisho wa kitamaduni wa Kizulu. Akijiita Rais wa Amabhinca, Mchunu aligeuza harakati dhidi ya wahamiaji kuwa zaidi ya siasa.

Akaiweka kama harakati ya kulinda utamaduni, ‘mapambano ya mwisho’ ya wanaume wa Kizulu na Waafrika Kusini kwa ujumla dhidi ya kufutwa kwa urithi wao na kile alichokiita wizi wa fursa za kiuchumi.

Ujumbe huo ulikuwa mkali na wenye kuvutia. Uligusa hisia za wanaume waliohisi kupuuzwa, kunyimwa mamlaka na kuachwa nyuma na mfumo wa kidemokrasia, uliotoa ahadi nyingi lakini chache kutimizwa.

Aliungana na harakati ya ‘March and March’ ambayo ni taasisi ya kitaifa inayoongozwa na Jacinta Ngobese-Zuma, iliyojijenga kama sauti ya kiraia ikitumia alama na mbinu za historia ya maandamano ya kiraia nchini humo.

Matakwa yao yalikuwa bayana: Udhibiti mkali wa visa, mapitio ya sera za hifadhi na hatua kali dhidi ya biashara zinazoajiri wahamiaji wasio na vibali. Harakati iliweka tarehe ya mwisho yenye msisimko: “Wahamiaji wote wasio halali waondoke Afrika Kusini ifikapo Juni 30, 2026.”

Maandamano yaliyofuata kuanzia Aprili hadi Mei 2026 yalikuwa makubwa. Durban, Mary Fitzgerald Square Johannesburg, Pretoria, KuGompo City harakati hizo zilisambaa nchi nzima kama dhoruba inayokua. Mchunu alitembea mstari wa mbele, sauti yake ikisikika kwa vipaza sauti na hotuba zake zisizozuilika.

Katika maandamano ya Durban Aprili 2026, Mchunu aliongoza wafuasi na mvutano uliongezeka zikazuka vurugu kati ya waandamanaji na walinzi binafsi wa biashara zinazomilikiwa na wageni.

Johannesburg hali ilikuwa ya kutisha zaidi. Waandishi wa habari walishuhudia mkimbizi kutoka Cameroon akipigwa, pamoja na matukio kadhaa ya vitisho na mashambulizi ya makundi ya waandamanaji.

Zaidi ya suala la uhamiaji, orodha ya matukio tata ya Mchunu ilizidi kupanuka. Tume ya Haki za Binadamu ya Afrika Kusini ilibaini Oktoba 2025 kwamba kauli zake za chuki dhidi ya wapenzi wa jinsia moja zilikuwa na uwezekano mkubwa wa kukiuka Sheria ya Usawa. Aliamriwa kuondoa maudhui yake, kuacha kabisa matamshi ya chuki na kuomba msamaha hadharani. Alikataa waziwazi kufanya hilo.

“Ningependa kwenda jela kuliko kuomba msamaha kwa LGBTQIA+,” alisema, kauli iliyowafurahisha wafuasi wake na kuishtua jamii ya kiraia.

Mwishoni mwa Aprili 2026, akizungumza katika maandamano ya ‘March and March’ mjini Pretoria, na baadaye kwenye mahojiano ya televisheni, Mchunu alimshambulia kiongozi wa EFF Julius Malema.

Alidai kwamba Malema amepokea Dola 60 milioni (takriban Sh156 bilioni) kutoka kwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya wa Nigeria. Kwamba anawalinda wahamiaji wasio halali kwa masilahi binafsi na anapokea fedha hizo kutoka kwa wageni haramu.

Alimwita Malema ‘nyoka aliyekufa,’ ‘shetani wa siasa’ na mwanasiasa aliyepitwa na wakati anayepaswa kwenda jela.

Malema alijibu kupitia timu yake ya mawakili, akitaka kulipwa fidia, kuombwa msamaha hadharani na kupeleka suala hilo Mahakama Kuu ya Gauteng. Jaji Mncedisi Khumalo aliamua kwamba kauli hizo ni za kashfa na zisizo halali, akamzuia Mchunu kuzitoa tena lakini alikataa kutii amri hiyo.

Hata akiwa amesimama nje ya mabaki ya nyumba yake iliyochomwa moto, akiendelea kukabiliwa na hali ya kisiasa na kisheria, aliendelea kumshambulia Malema hadharani.

Huyu ni mtu aliyesababisha machafuko. Mtu aliyeshinda kesi ya uchochezi. Mtu ambaye nyumba yake iliteketezwa. Na mtu aliye chini ya amri ya mahakama lakini bado anaonekana kuipuuza.

Hii inamaanisha nini, wakati mtu aliyepoteza kila kitu bado anaendelea kupambana? Ina maana gani kwa taifa linalopasuka katika misingi ya uhamiaji, utambulisho na ukosefu wa usawa, wakati mtu huyo anakataa kutii amri?

Soma sehemu ya tatu na ya mwisho kesho

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *