Mwanamfalme William pamoja na mkewe Catherine anayejulikana kama Kate walionekana wakimpokea Rais Frank-Walter Steinmier na mkewe Elke Büdenbender, walipowasili katika uwanja wa ndege wa Heathrow.
Baadae wageni hao waliokaribishwa kwa kutandikiwa zulia jekundu, walipelekwa moja kwa moja katika kasri la Winsor walikopokewa na Mfalme Charles III na mkewe Camila, kukifuatiwa na sherehe za kifalme ambazo kwa kawaida, ufalme huo wa Uingereza huwafanyia wageni wake mashuhuri ikiwemo karamu ya kifahari.
Rais Steinmeier, ndio rais wa kwanza wa ujerumani, kufanya ziara rasmi ya kiserikali nchini Uingereza ndani ya miaka 27. Ujerumani na Uingereza zinania ya kuimarisha ushirikiano zaidi, wakati wanapokumbana na changamoto za vita vya Ukraine na sera za rais wa Marekani Donald Trump za “Marekani Kwanza” zinazotishia kuharibu uhusiano wa muda mrefu wa biashara na usalama.
Ziara hiyo itaendeleza kauli ya Mfalme Charles alipokuwa ziarani nchini Ujeruman mwaka 2023, ambako alisisitiza uhusiano mwema kati ya mataifa hayo na umuhimu wa ushirikiano zaidi kwa siku za baadae, jambo lililoungwa mkono pia na Steinmeier kabla ya kuondoka Ujerumani.
Akizungumza na waandishi habari mjini Berlin, muda mfupi kabla ya kuanza safari yake ya Uingereza, Steinmeier alisema nchi hizo zipo kwenye njia ya kurekebisha mahusiano hayo baada ya uamuzi mkubwa uliochukuliwa na Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya maarufu kama Brexit.
Steinmeier kulihutubia bunge la Uingereza
Rais huyo wa Ujerumani anatarajiwa kulihutubia bunge katika ziara yake hiyo na hii leo jioni anatarajiwa pia kukutana na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, kwa mazungumzo yatakayojikita juu ya uungwaji mkono wa mataifa hayo mawili kwa Ukraine katika vita vyake na Urusi.
Ziara hii imejiri wakati serikali za mataifa yote mawili, zikipambana na shinikizo kutoka vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia vinavyopinga uhamiaji, chama cha Alternative for Germany (AfD) na chama cha Reform nchini Uingereza kinachoongozwa na Nigel Farage.
Siku ya Ijumaa Steinmeier, pamoja na mkewe wamepangiwa kutembelea kanisa kuu la Coventry kukumbuka mashambulizi ya mabomu yaliyofanywa na Manazi mjini London, yaliyosababisha mauaji ya watu 568 na kuharibu nusu ya majumba ya mji huo mnamo Novemba 14 mwaka 1940.
Mauaji hayo yalitokea wakati wa vita vya pili vya dunia. Ujerumani hata hivyo imeshaomba radhi zaidi ya mara mbili kufutia ukatili wa utawala wa Nazi.