Vita wakati mwingine huweka wazi washindi wake wa kweli na walioshindwa sio kwenye uwanja wa vita, bali katika vyumba vya kifikra na vituo vya kimkakati.

Katika kutathmini shambulio la Marekani dhidi ya Iran, jarida la Foreign Policy limeashiria wasiwasi unaozidi kuongezeka miongoni mwa wasomi na wanafikra wa Marekani kuhusu tofauti kubwa iliyopo kati ya ubabe wa vita wa Washington katika upeo wa kimataifa na uwezo wake halisi wa kufikia malengo yanayofuatiliwa katika ubabe huo. Hal Brands, mhadhiri wa taaluma ya mahusiano ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, ametahadharisha katika ripoti hiyo kwamba vita na Iran vimekuwa mtihani mkubwa wa kutathmini nguvu za kijeshi za Marekani; mtihani ambao umeonyesha kwamba hata nguvu kubwa zaidi ya kijeshi duniani inakabiliwa na vizuizi vya rasilimali, kudhoofika uwezo wa kupambana, na changamoto za kusimamia migogoro kadhaa kwa wakati mmoja. Tathmini hii, kwa kweli, ni nyongeza ya maonyo yale yale ambayo yamekuwa yakikaririwa mara kwa mara katika taasisi za kifikra za Marekani katika miaka ya hivi karibuni. Shirika la RAND limesisitiza katika ripoti kadhaa kuhusu ushindani mkali uliopo kati ya nguvu kubwa ulimwenguni na kwamba Marekani haiwezi tena kuchukua hatua kwa wakati mmoja kwenye nyanja kadhaa kuu za kijeshi kama ilivyokuwa katika zama za baada ya Vita Baridi. Kwa mtazamo wa watafiti wa taasisi hiyo, vita vya kuchosha Asia Magharibi, ushindani na Uchina Asia Mashariki, na uungaji mkono kwa Ukraine yote hayo yana msingi mmoja. Kuhusu suala la silaha, kushugulishwa Marekani katika Nyanja kadhaa za vita kunaonyesha wazi  kuwa hifadhi ya silaha na uwezo wa viwandani haitoshi kukidhi mahitaji ya ushindani wa kijeshi wa muda mrefu kimataifa.

Wasiwasi huo pia unaonekana wazi katika tathmini za Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati na Kimataifa (CSIS). Wataalam wa kituo hicho awali walikuwa wameonya kwamba kukiibuka mzozo kuhusu Taiwan, Marekani itakabiliwa na uhaba wa makombora ya masafa marefu, mifumo ya ulinzi wa anga na silaha makini za ulengaji shabaha. Vita dhidi ya Iran vimeondoa wasiwasi huu kutoka mazingira ya kinadharia hadi kwenye uwanja wa vitendo katika medani ya vita. Matumizi makubwa ya makombora ya Tomahawk, kuharibiwa mifumo ya ulinzi wa anga ya SM-3, THAAD, na Patriot, yote hayo yamethibitisha kuwa hata operesheni ndogo pia zinaweza kuathiri pakubwa nguvu za kijeshi za Marekani katika maeneo mengine ya dunia.

Paul Kennedy, mwanahistoria mashuhuri wa Uingereza, alisema katika kitabu chake maarufu cha “The Rise and Fall of Great Powers” miongo kadhaa iliyopita kwamba madola ambayo hutoa ahadi za kutekeleza majukumu ya kigeni kuliko uwezo wao wa kiuchumi na kijeshi huingia hatua kwa hatua kwenye njia ya mmomonyoko wa kimkakati. Leo, wachambuzi wengi wanaamini kwamba Marekani inakabiliwa na hatari hiyo hiyo. Suala hili ni muhimu sana hasa tukizingatia ushindani wake mkubwa na China. Eli Ratner, afisa wa zamani wa Pentagon, ameonya mara kwa mara kwamba changamoto kuu kwa Marekani katika karne ya 21 ni kudhibiti nguvu inayokua kwa kasi ya Beijing. Ukweli mwingine mchungu kwa Marekani ni kwamba Asia Magharibi inaendelea kuirudisha nyuma Washington. Kuanzia Iraq na Afghanistan hadi vita vya Gaza, mgogoro wa Bahari Nyekundu, na sasa makabiliano na Iran, hakuna hata moja ya migogoro hii imeirihusu Marekani kutekeleza mpango wake wa eti mhimili kuelekea Asia au kwa maneno mengine “pivot to Asia.”

Matukio haya pia yanafuatiliwa kwa wasiwasi mkubwa katika eneo la Asia Mashariki. Baadhi ya viongozi wa Japan na Korea Kusini wameelezea wasiwasi wao kuhusu kuhamishiwa mifumo ya ulinzi ya Marekani katika eneo la Asia Magharibi. Huko Taiwan pia, swali hili muhimu linaulizwa kwamba je, ikiwa mizozo ya wakati mmoja itaibuka barani Asia, Washington itaweza kweli kutimiza majukumu yake ya kiulinzi na kiusalama? Picha hii, kwa kweli haina maana kuwa nguvu ya kijeshi ya Marekani imepungua kabisa kimataifa. Marekani bado ina bajeti kubwa zaidi ya kijeshi duniani, mtandao mpana zaidi wa miungano ya kijeshi, na uwezo mkubwa zaidi wa kiteknolojia, lakini pamoja na hayo haina uwezo wa kijeshi wa moja kwa moja ilivyokuwa nao katika miaka ya nyuma. Vita na Iran vimeonyesha kwamba hata mataifa makubwa yanapaswa kufanya machaguo; machaguo kati ya vipaumbele, medani za vita, na gharama ambazo sasa zina kikomo, kinyume na ilivyokuwa zamani. Wakati huo huo, vita hivi pia vimetoa somo muhimu kuhusu namna vita vya baadaye vitakavyokuwa. Nafasi ya ndege zisizo na rubani, mifumo mahiri, vita vinavyotegemea mitandao na akili mnemba vimethibitisha kuwa ubora wa kijeshi hautegemei tu idadi ya manowari na ndege za kivita. Nguvu za kati pia zinaweza kuwatwisha gharama kubwa za kijeshi wachezaji wakuu kwa kutumia teknolojia za kisasa vitani. Moja ya matokeo muhimu zaidi ya vita hivi ni kwamba Iran imeweza kuweka kioo mbele ya sera za nje za Marekani, kioo ambacho mbali na kuakisi uwezo wake wa kijeshi pia unaakisi mapungufu yake makubwa katika uwanja huo. Sasa swali la msingi kwa Washington sio tena kama inaweza kuingilia kati au la; bali ni vita gani vinafaa kupiganwa katika ulimwengu uliojaa mizozo ya wakati mmoja, na ni kwa kiwango gani Marekani inaweza kuendelea kumudu kulipa gharama ya kuongoza dunia?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *