Umoja wa mataifa umelaani kuongezeka kwa matukio ya ukandamizaji dhidi ya upinzani na vyombo vya habari kuelekea uchaguzi mkuu nchini Uganda, UN ikitoa wito wa kufanyika uchunguzi huru kuhusu matukio ya kukamatwa kiholela na mateso dhidi ya wapinzani.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Ofisi ya haki za binadamu ya umoja wa mataifa imeainisha ripoti za kuaminika zinazoonesha kuwa takriba watu 550, wakiwemo wanachama na wafuasi wa chama cha upinzani NUP chake mgombea wa urais Bobi Wine, walikamatwa na kuzuiliwa tangu mwanzoni mwa mwaka huu.
Zaidi ya watu 300 kati yao, wamekamatwa tangu kuanza kwa kampeni za uchaguzi mwezi Septemba kuelekea uchaguzi wa Januari15 mwaka ujao, wengi wao wakikabiliwa na mashtaka mbalimbali ikiwemo kutoheshimu sheria na kuchochea vurugu.

Ofisi hiyo aidha, imeelezea namna vikosi vya usalama vilivyojihami vimetumwa katika maeneo ambapo chama cha upinzani NUP kinaendesha kampeni zake, huku ripoti zikieleza kuongezeka kwa matukio ya mateso dhidi ya wafuasi wa upinzani na wanaharakati.
Taarifa hiyo pia imekosoa kiminywa kwa uhuru wa vyombo vya habari, kufuatia visa vya hivi karibuni ambapo zoezi la kuwaidhinisha waandishi wa habari liliondolewa, huku makumi ya wanahabari wakikandamizwa na wengine vifaa vyao vya kazi kuchukuliwa.

Mkuu wa tume ya haki ya UN Volker Turk amezitaka mamlaka za Uganda kukomesha ukandamizaji wote dhidi ya vyombo vya habari na upinzani, na kuheshimu sheria za kimataifa za haki za binadamu.