
Press TV ya Iran imezindua kitengo cha lugha ya Kiebrania jambo ambalo limezua hofu katika duru za vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni wa Israel kwani hatua hiyo inaonekana kama sehemu ya juhudi za kimkakati za Iran kuathiri maoni ya Waisraeli huku kukiwa na vita vya simulizi vinavyozidi kupamba moto.
Tangu uzinduzi wake rasmi mwishoni mwa mwezi uliopita, huduma ya lugha ya Kiebrania ya Press TV imeibua gumzo katika vyombo vya habari vya Kizayuni, huku wachambuzi wengi wakitoa maoni yanayoonyesha hofu na wasiwasi. Huduma hii, inayotolewa na Press TV ambayo ni sehemu ya Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB World Service), ilianzishwa ili kufikia wanaozungumza Kiebrania kote duniani.
Huduma hii inapatikana kupitia akaunti ya X (@PresstvHebrew) na kituo maalum cha Telegram (@PresstvHebrew), huku tovuti kamili ikitarajiwa kuzinduliwa katika miezi ijayo.
Kwa mujibu wa Dkt. Ahmad Noroozi, mkurugenzi wa IRIB World Service, jukumu kuu la kituo hiki ni kufichua ukweli ambao vyombo vya habari vya Kizayuni vinajaribu kuficha, hasa kutokana na udhibiti mkali uliowekwa kwa vyombo vya habari vya Kiebrania katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu wakati wa vita vya siku 12.
Uzinduzi wa huduma ya Kiebrania ulifuatia azimio la Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni la Iran, lililoelekeza IRIB kuanzisha televisheni ya kimataifa ya lugha ya Kiebrania. Baraza hilo, likiongozwa na Rais Masoud Pezeshkian, limesema mpango huu unalenga kukabiliana na propaganda za utawala wa Kizayuni na vyombo vyake, kuimarisha diplomasia ya vyombo vya habari vya Iran, na kutoa taswira sahihi zaidi ya matukio ya kieneo.
Tangu uzinduzi wake, vyombo vya habari vya Kizayuni vimekuwa na taharuki, vikilieleza kuwa hiyo ni sehemu ya “vita vya simulizi” na jaribio la moja kwa moja la vyombo vya habari vya Iran kushawishi jamii ya walowezi wa Kizayuni.
Kwa mfano, tovuti ya habari ya Kizayuni Walla ilichapisha ripoti yenye kichwa: “Iran Yazindua Kituo cha Televisheni cha Kiebrania, ikimpita Netanyahu na Kuzungumza Moja kwa Moja na Waisraeli.” Ripoti hiyo ilieleza kituo cha Kiebrania kama sehemu ya “juhudi za propaganda za Tehran” zilizoundwa kuingiza simulizi za Iran moja kwa moja katika anga ya vyombo vya habari vya Kiebrania bila wapatanishi.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa vyombo vya habari, ripoti hizi zinadhihirisha hofu na wasiwasi katika duru za kisiasa na za habari za utawala wa Kizayuni wa Israel, ambazo kwa muda mrefu zimefuata sera ya kuficha habari na uchambuzi unaoonyesha udhaifu wa utawala huo, hata katikati ya vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza.