
Amesema wasiwasi huo unaongezeka wakati ambapo mapigano kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF yanazidi kushika kasi katika jimbo la Kordofan.
Türk ametoa wito wa kusitishwa haraka kwa machafuko ili kuruhusu misaada kufikishwa katika miji iliyo katika hatari ya kushambuliwa.
Watu 269 wauawa
Katika taarifa yake, Türk amesema kuwa tangu RSF ilipouteka mji wa Bara huko Kordofan mnamo Oktoba 25, ofisi yake imerekodi vifo takribani 269 vilivyosababishwa na mashambulizi ya anga, makombora na mauaji holela.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, pia kumekuwepo taarifa za mauaji ya kulipiza kisasi, watu kukamatwa kiholela, utekaji nyara, unyanyasaji wa kijinsia na ajira ya lazima, ikiwemo kwa watoto.
Türk amesema ni jambo la kusikitisha kuona historia ikijirudia Kordofan, muda mfupi tu baada ya matukio ya kushtua yaliyoshuhudiwa huko El-Fasher.