Simba kama kawaida imeendeleza moto wake kwenye Ligi Kuu Bara, baada ya kuichapa Mbeya City kwa mabao 3-0 lakini utamu wa ushindi huo ni kiungo Mohammed Bajaber.

Ushindi huo wa nne kwenye mechi nne unaifanya Simba kufikisha pointi 12 ikipaa kutoka nafasi ya nane mpaka ya nne ikiishusha Namungo kwa nafasi moja.

Mapema tu Mbeya City ndio walioilainisha mechi  baada ya mshambuliaji wake Vitalis Mayanga kupewa kadi nyekundu ya Moja kwa Moja dakika ya 23 baada ya kumpiga kiwiko beki wa Simba Antony Mligo na mwamuzi Nassoro Mwinchui kutoa kadi hiyo.

Kadi hiyo ikafungulia mabao ambapo kiungo Morris Abraham akafungua ukurasa wa mabao dakika ya 27 akimalizia kazi nzuri ya Ellie Mpanzu.

Wakati City inatafuta utulivu ikajikuta inaruhusu bao la pili mfungaji akiwa Jonathan Sowah akifunga kirahisi akinufaika na makosa ya mabeki wa wageni waliokuwa wanagongeana pasi eneo la nyuma na mshambuliaji huyo kwenda kumfunga kipa Benno Kakolanya kirahisi.

Mabao hayo yakadumu mpaka kipindi cha kwanza huku Simba iliyo chini ya kocha wa muda Seleman Matola ikionekana kutulia na kucheza kwa kasi.

Kipindi cha pili Simba kama ingetulia ingeongeza mabao mengi lakini washambuliaji wake wakajikuta wanapoteza nafasi nyingi.

Majukwaa ya Uwanja wa Meja Jeneali Isamuhyo yakalipuka kwa furaha dakika ya 84 wakati kiungo wao Bajaber akiingia Uwanjani ikiwa ni mchezo wake wa kwanza tangu asajiliwe na wekundu hao akitokea Polisi ya Kenya, akichukua nafasi ya Mpanzu.

Mapokezi hayo yakalipa dakika ya 85 baada ya Bajaber mpira wake wa kwanza kugusa uwanjani akaifungia Simba bao la tatu akipokea pasi ya Steven Mukwala.

Bao hilo likaumaliza mchezo huo ukiisha kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 huku City ikizidi kuandamwa na matokeo mabaya, ikifikisha michezo minne bila kushinda au kupata sare.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *