
Mataifa zaidi ya 17 ya umoja wa Ulaya ikiwemo ujumbe wa umoja wa Ulaya nchini Tanzania, wametoa taarifa ya pamoja kuhusu vurugu za uchaguzi wa Octoba 29 nchini humo.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Mataifa ya Uingereza, Canada, Norway, Uswizi, Ubelgiji, Denmark, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Poland, Slovakia, Uhispania na Sweden, kwenye taarifa yao, wameeleza kuguswa na taarifa za vifo na majeruhi wakati na baada ya uchaguzi wa mwaka huu.
Nchi hizo zimeitaka serikali ya Tanzania waliyosema imejipambanua kama kisiwa cha amani, kulinda uhuru wa watu kutoa maoni na kwa vyombo vya usalama kujiepusha dhidi ya matumizi ya nguvu kwa waandamanaji.
Aidha nchi hizo zimesisitiza wito wao kwa Serikali ya Tanzania kuheshimu mikataba ya kimataifa ikiwemo ya uhuru wa kisiasa na maoni.
Kwa mujibu wa taarifa yao, wamepokea ushahidi usio na shaka kutoka kwa mashirika ya ndani na yale ya kimataifa kuhusu kufanyika kwa mauaji ya kupangwa, watu kutoweka, kukamatwa kiholela na kufichwa kwa miili ya watu waliouawa wakati wa maandamano.
Tunazitaka mamlaka kwa haraka sana kukabidhi miili ya watu waliouawa kwa familia zao, kuwaachia wafungwa wote wa kisiasa na kuruhusu washukiwa kupata msaada wa kisheria”, ilisema taarifa hiyo.
Aidha, tunaitaka Serikali kushughulikia mapendekezo yaliyotolewa na ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Afrika na SADC, ambao walionesha wazi kuwa uchaguzi ulikuwa na mapungufu makubwa”.
Taarifa yao iliongeza kuwa wanakaribisha hatua ya Serikali kutaka kufahamu kiini cha vurugu na mazingora yaliyopelekea vifo ili kupata haki kwa wahanga.
“Uchunguzi wowote lazima uwe huru, wa wazi na shirikishi kwa kuyahusisha mashirika ya kiraia, taasisi za dini na wadau wengine wa kisiasa”. Taarifa ilisema.
Taarifa yao imekuja siku moja kupita tangu Marekani kupitia kwa wizara ya mambo ya nje, itoe taarifa kusema kuwa inatathmini upya uhusiano wake na Tanzania, ikionesha kutofurahishwa na yaliyotokea Tanzania wakati wa uchaguzi.
Pamoja na Marekani, hapo jana pia wataalamu kutoka tume ya haki za binadamu ya umoja wa Mataifa, walilaani kile walichosema ripoti za matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu kufuatia uchaguzi wa Octoba 29.
Serikali lazima itoe taarifa kuhusu hatima na mahali walipo watu wote waliotoweka na kuhakikisha utambuzi na urejeshaji wa maiti kwa familia zao kwa heshima,” wataalamu hao walisema.
“Vikwazo vyote kwa vyombo vya habari lazima viondolewe, kwani haviendani na majukumu ya kimataifa ya Tanzania.” Ilisema taarifa ya wataalamu hao.
Kuelekea maandamano yaliyopangwa kufanyika tarehe 9 Desemba 2025, wataalamu hao wamezitaka mamlaka za Tanzania na vikosi vya usalama kuzuia ukiukwaji zaidi na kulinda haki ya watu ya kukusanyika kwa amani.