“Tunarudia kueleza wazi kwamba tunaunga mkono suala la uhuru, umoja, na uadilifu wa eneo la Syria,” balozi wa Slovenia kwenye Umoja wa Mataifa Samuel Zbogar aliuambia mkutano na waandishi wa habari mjini Damascus Alhamisi.
“Ujumbe wetu ulikuwa mwepesi na wa wazi: Tunatambua matamanio na changamoto ya nchi yenu, na njia ya kuelekea kupata mustakabali bora wa Syria mpya itakayoongozwa na Wasyria wenyewe,” alisema mwanadiplomasia huyo ambaye nchi yake ndio rais wa sasa wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
“Jumuiya ya kimataifa inasimama nanyi na iko tayari kuwasaidia kwa chochote mnachoamini kwamba kinaweza kuwasaidia,” alisema na kuongeza: “Tunataka kuwasaidia kujenga daraja kuelekea kwenye mustakabali huo mpya kwa ajili ya Wasyria.”
Ujumbe huo ulikutana na Rais wa mpito wa Syria Ahmed al-Sharaa imesema taarifa ya ofisi ya rais, iliyochapisha pia picha za mkutano huo.
Wakati Umoja wa Mataifa ukiangazia kujiimarisha tena nchini Syria, Baraza la Usalama hivi karibuni lilimuondolea vikwazo Sharaa mwanamgambo wa zamani wa jihadi ambaye vikosi vyake viliongoza harakati zilizomuondoa madarakani Assad mnamo Disemba 8, 2024.
Uchumi waimarika haraka
Katika hatua nyingine, uchumi wa taifa hilo umeripotiwa kupanda haraka zaidi ya makadirio yaliyowekwa na Benki ya Dunia ya wastani wa asilimia 1, kwa mwaka 2025, wakati wakimbizi wakirejea nchini humo kwa wingi baada ya kumalizika kwa vita vya miaka 14 vya wenyewe kwa wenyewe.
Benki ya Dunia mnamo Julai ilikadiria kwamba pato la ndani la Syria lingekua kwa asilimia 1 mwaka 2025 baada ya kudhoofika kwa asilimia 1.5 mwaka 2024, huku kukiwa na changamoto za usalama, vikwazo vya ukwasi na kusimamishwa kwa misaada ya kigeni.
Kuimarika huko kwa uchumi kunachochea mipango ya kuzindua upya sarafu ya nchi hiyo pamoja na juhudi za kujenga kitovu kipya cha fedha cha eneo la Mashariki ya Kati, Gavana wa Benki Kuu AbdulKader Husrieh alisema Alhamisi. “Sarafu mpya itakuwa ishara ya ukombozi wa kifedha,” Husrieh alisema
Kuondolewa kwa vikwazo ni “miujiza”
Akizungumza kwa njia ya video na shirika la habari la Reuters kwenye mkutano wa NEXT mjini New York, Husrieh amesema pia kwamba anayakaribisha makubaliano na kampuni ya Visa ya kuanzisha mifumo ya malipo ya kidijitali nchini humo na kuongeza kuwa taifa hilo linashirikiana na Shirika la Fedha Ulimwenguni, IMF kutengeneza mbinu za kupima kwa usahihi takwimu zitakazoakisi ukuaji huo mpya.
Mkuu huyo wa Benki Kuu ya Syria ambaye anasaidia juhudi za taifa hilo kuungana tena baada ya kuangushwa kwa utawala wa Bashar al-Assad yapata mwaka mmoja uliopita, alielezea pia hatua ya kufutwa kwa vikwazo vingi vya Marekani dhidi ya Syria kama “muujiza”.
Husrieh pia alisema Syria inafanya kazi ya kurekebisha kanuni za kupambana na utakatishaji fedha haramu na ufadhili wa ugaidi, jambo ambalo alisema litatoa uhakika zaidi kwa wakopeshaji wa kimataifa.
