
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, ametambua kuwa mamlaka za mpito zimeanza kujenga misingi ya haki ya mpito kwa kuunda kamisheni za kitaifa za haki ya mpito na watu waliopotea, pamoja na kuanzisha vyombo vya uchunguzi katika maeneo ya pwani na Suweida.
“Hizi ni hatua za kutia moyo, lakini ni mwanzo tu wa yale yanayohitajika kufanyika,” kwa mujibu wa msemaji wa OHCHR, Thameen Al-Keethan.
Kesi dhidi ya watuhumiwa wa ghasia katika ukanda wa pwani pia zimeanza, na rasimu ya sheria ya haki ya mpito imetangazwa.
Mauaji, utekaji na unyama bado vinatamalaki
Licha ya maendeleo hayo, OHCHR inasema inaendelea kupokea “taarifa za kusikitisha za mauaji ya bila kufuata taratibu, mauaji ya kiholela na utekaji nyara katika maeneo mbalimbali ya nchi.”
Ukatili huo umewalenga wajumbe wa jamii mbalimbali na watu wanaoshukiwa kuwa na uhusiano na serikali ya zamani.
Ofisi hiyo imesema Mamía ya watu wameuawa katika kipindi cha mwaka uliopita kwa risasi, visu, kupigwa mawe, mashambulizi ya mabomu ya kutupa kwa mkono, na mashambulizi ya makombora.
Kwa mujibu wa OHCHR, waliotekeleza ukatili huo ni pamoja na vikosi vya usalama vya mamlaka za mpito, makundi yanayohusishwa nayo, mabaki ya vikosi vya serikali ya zamani, makundi yenye silaha ya kienyeji na watu wenye silaha wasiojulikana.
“Tumerekodi pia vifo vinavyotokana na mabaki ya vilipuzi vya vita,” ameongeza Al-Keethan.
Ukatili wa Kijinsia, unyang’anyi na kufurushwa
OHCHR pia imebaini ukiukaji mwingine kadhaa, ikiwemo ukatili wa kijinsia, kukamatwa kiholela, uporaji, uharibifu wa nyumba, kufukuzwa kwa nguvu na kunyang’anywa mali za watu.
Vikwazo dhidi ya uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa amani pia vimeibua mashaka.
Ukiukaji mwingi umeathiri zaidi jamii za Waalawite, Wadrusi, Wakristo na Mabedui.
OHCHR inasema ukatili huu una “chochewa na kauli za chuki, mtandaoni na mitaani.”
Operesheni za kijeshi za Israel zinachochea maumivu kwa raia
Mwaka uliopita pia kumeonekana mashambulizi ya mara kwa mara ya kijeshi ya Israel ndani ya Syria, ikiwa ni pamoja na uvamizi na kuongeza maeneo waliyoyateka imesema ofisi hiyo ya haki za binadamu.
“Tumepewa taarifa za vifo vya raia, ikiwemo katika operesheni ya hivi karibuni ya Israel karibu na Damascus, pamoja na kukamatwa na upekuzi wa nyumba,” amesema Al-Keethan.
Ukosefu wa uhakiki katika vikosi vya usalama wazua hofu
Moja ya masuala makuu yanayowatisha wataalamu wa haki za binadamu ni muunganisho wa haraka wa makundi ya zamani ya waasi ndani ya vikosi vipya vya usalama bila kufanyiwa uchunguzi makini wa kuheshimu haki za binadamu.
“Marekebisho ya sekta ya usalama ni muhimu ili kuhakikisha kwamba waliokiuka sheria za kimataifa hawajumuishwi katika miundo mipya,” Al-Keethan ameonya.
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Volker Türk ametoa wito kwa mamlaka za Syria kushughulikia mizizi ya ukiukaji unaoendelea.
“Uwajibikaji, haki na usalama wa Wasyria wote ni masharti ya msingi kwa mafanikio ya uongozi wa mpito,” amesema. “Haki za waathiriwa kupata tiba, fidia na marekebisho lazima zitimizwe.”
UN yaendelea kutoa msaada
OHCHR inasema timu yake mjini Damascus inaunga mkono juhudi za Syria kuunda mfumo jumuishi wa haki ya mpito na kuimarisha utawala wa sheria.
“Ukiukaji wote wa zamani na wa sasa lazima uchunguzwe kwa uhuru, kwa kina na kwa uwazi, na wahusika wawajibishwe,” amesisitiza Türk.