Njia ya kuelekea Kombe la Dunia la FIFA 2026 sasa imewekwa wazi kwa Iran baada ya droo ya Ijumaa usiku mjini Washington, D.C. kuipanga Timu ya Taifa ya Soka ya Iran maarufu kama, Team Melli, katika Kundi G lenye mvuto na msisimko, pamoja na Ubelgiji, Misri na New Zealand.
Sherehe hiyo ilifanyika katika Kituo cha John F. Kennedy na kuhudhuriwa na Rais wa FIFA Gianni Infantino, nyota wa zamani wa soka duniani na wajumbe kutoka mataifa yote yaliyofuzu. Kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran walihudhuria kocha mkuu Amir Ghalenoei, meneja wa timu Mehdi Mohammad-Nabi, na Omid Jamali wa idara ya kimataifa ya Shirikisho la Soka la Iran, huku nyota wa zamani Mehdi Mahdavikia pia akialikwa na FIFA.
Toleo la 2026 linaweka historia kwa kupanua mashindano hadi timu 48, zikigawanywa katika makundi 12 ya timu nne. Kila timu itacheza mechi tatu, na mbili bora kutoka kila kundi pamoja na nane bora waliomaliza nafasi ya tatu kuingia hatua mpya ya timu 32. Kuanzia hapo, mashindano yatakuwa ya mchujo wa moja kwa moja. Droo ilifanywa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya FIFA, huku wenyeji Marekani, Kanada na Mexico wakipangwa moja kwa moja katika Pot ya Kwanza. Infantino aliwaalika maafisa kutoka nchi zote tatu wenyeji jukwaani, na kwa ishara ya kipekee, kila mmoja alichukua mpira ulioamua kundi lao.
Iran iliingia droo kutoka Pot ya Pili, sambamba na Morocco, Uruguay, Uswisi, Japan na Senegal. Nyota wa zamani Rio Ferdinand na gwiji wa mpira wa vikapu Shaquille O’Neal walishiriki katika kuendesha droo hiyo. Wachambuzi wamesema nafasi ya Iran katika Kundi G ni ngumu lakini ina njia ya kupenya hadi hatua ya mchujo. Ratiba ya mechi za Iran tayari imeshajulikana ambapo Juni 15, 2026 itacheza dhidi ya New Zealand, Juni 21 dhidi ya Ubelgiji na Juni 26 dhidi ya Egypt. Mechi hizi tatu za hatari kubwa zinaweza kuandika moja ya kampeni zenye matumaini makubwa kwa Team Melli katika miaka ya karibuni.

Hata hivyo, kivutio cha droo kiligeuka kuwa mjadala pale Rais wa Marekani Donald Trump alipopewa nafasi kubwa jukwaani, jambo lililowafanya mashabiki wengi kuliona tukio hilo kuwa la aibu na lisilovutia. Sherehe ambayo ilikusudiwa kuwa sherehe ya mashindano ya timu 48 katika kombe hilo ambalo linaandaliwa kwa pamoja na Marekani, Kanada na Mexico, iligeuka kuwa maonyesho yaliyotawaliwa na Trump na Infantino. Infantino alikosolewa vikali kwa kumpa Trump tuzo mpya ya FIFA ya “Amani,” hatua iliyochochea mjadala mkali mitandaoni na kuonekana kama kujipendekeza.
Mashabiki walitumia mitandao ya kijamii kulalamika, wakisema droo hiyo imegeuka kuwa ya kusikitisha na ya aibu. Mmoja aliandika: “Droo ya Kombe la Dunia inanifanya nihisi aibu.” Mwingine akaongeza: “Tuzo ya amani iliyobuniwa kwa ajili ya Trump ni ya kusikitisha kabisa.” Sherehe hiyo, iliyohusisha pia nyota wa Marekani kama Tom Brady na Aaron Judge, ilikosolewa kwa utangulizi mrefu na maonyesho yaliyopitiliza.