
Rais Masoud Pezeshkian amesema taifa la Iran limejifunza kutokubali kudhalilishwa kutoka kwa Kiongozi aliyeuawa shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.
Rais Pezeshkian ameyasema hayo katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X, akiashiria urithi wa Kiongozi aliyeuawa shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ambaye alikuwa akilihimiza taifa kulinda hadhi na heshima yake na kukataa matakwa ya kuchupa mipaka ya maadui wake.
Amesisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu imejiandaa kwa matukio yote yanayowezekana huku juhudi zikiendelea kwa ajili ya kukomesha mzunguko sasa wa uchokozi usio na sababu wa Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Akizungumzia hati ya makubaliano iliyopangwa kusainiwa kati ya Iran na Marekani nchini Uswisi siku ya Ijumaa, Rais Masoud Pezeshkian amesema: “Maelewano hayo ni hatua muhimu kuelekea upande wa kusimamisha vita na kuanza mazungumzo,” akikumbusha kwamba hata hivyo makubaliano ya mwisho bado hayajapata sura.
Kabla ya hapo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi alisema mazungumzo yanayolenga kufikia makubaliano kamili yataanza baada ya mchakato wa kusainiwa hati ya maelewano kukamilika.
Rais Pezeshkian amesema Jamhuri ya Kiislamu inaendelea kuwa tayari “kwa machaguo yote,” licha ya mchakato wa kidiplomasia unaoendelea.
Wakati huo huo, Rais amesisitiza kwamba kipaumbele cha serikali ni kuendelea kuhudumia umma bila kujali kama mazungumzo hatimaye yatazaa matunda na kufikiwa makubaliano au la.