Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa idadi kubwa ya raia wa Marekani wanapinga mashambulizi ya kijeshi yaliyofanywa na serikali ya Rais Donald Trump dhidi ya Iran.
Mnamo tarehe 5 Desemba 2025, tovuti ya takwimu Statista ilichapisha matokeo ya utafiti wa maoni kuhusu shambulio hilo. Kulingana na utafiti huo, Wamarekani wengi walionyesha kutoridhishwa na hatua ya kijeshi ya Marekani, wakiona kuwa inaweza kuongeza mivutano ya kimataifa na kuathiri usalama wa ndani.
Kwa mujibu wa tovuti hiyo, kuendelea kwa mivutano kati ya Marekani na Iran mwishoni mwa mwaka 2025 kumesababisha mgawanyiko mkubwa ndani ya jamii ya Marekani. Uchunguzi wa maoni uliofanywa na televisheni ya CNN mnamo tarehe 22 na 23 Juni 2025, kabla ya majibu ya Iran na tangazo la kusitisha mapigano na Rais Trump, ulionesha kuwa Wamarekani wengi (asilimia 56) walipinga uamuzi wa Rais Trump kuanzisha mashambulizi ya kijeshi.
Asilimia 82 ya Warepublican waliunga mkono mashambulizi ya kijeshi, ilhali asilimia 60 ya wapiga kura huru na asilimia 88 ya wafuasi wa chama cha Democrat walipinga vikali hatua hiyo. Hata hivyo, ni muhimu kutambua kuwa sehemu kubwa ya wapiga kura wa chama cha Republican, takribani mmoja kati ya kila watano, pia walikuwa wapinzani wa mashambulizi hayo.
Kuna sababu kadhaa za msingi za upinzani huu.
Kwanza, kutokuwapo kwa imani ya umma katika maamuzi ya Trump kuhusu matumizi ya nguvu za kijeshi. Wengi wa washiriki katika utafiti wa maoni uliofanywa na CNN walieleza wazi kuwa hawana imani na uamuzi wa Trump kuanzisha vita. Walihisi kuwa rais hakuzingatia maslahi ya kitaifa kwa dhati, bali alichochewa zaidi na shinikizo za kisiasa na ushawishi wa makundi ya kigeni yenye nguvu.
Sababu ya pili ni hofu ya kuongezeka kwa vitisho dhidi ya Marekani. Takribani asilimia 60 ya washiriki katika tafiti za maoni walisema kuwa shambulio la Marekani dhidi ya Iran linaweza kuongeza hatari ya hatua za kulipiza kisasi kutoka Iran. Hofu hii ilionekana zaidi miongoni mwa vijana na wapiga kura huru, ambao walihisi kuwa kuingia katika vita vipya hakutaimarisha usalama wa Marekani, bali kutaweka taifa hilo katika hatari mpya.
Sababu ya tatu ni kuwa ni mgongano na ahadi za kampeni za Trump. Katika kampeni zake za uchaguzi, Trump mara nyingi alisisitiza kuwa ataweka kikomo kwa “vita visivyo na mwisho” na kuiepusha Marekani na migogoro ya nje. Lakini hatua ya kijeshi dhidi ya Iran ilikuwa kinyume kabisa na ahadi hiyo. Wapiga kura wengi, walichukulia shambulio hilo kama usaliti wa kauli zake za kupinga vita.

Katika tafiti za maoni, ni asilimia 9 pekee ya Wamarekani waliounga mkono kupelekwa kwa vikosi vya nchi kavu nchini Iran, huku asilimia 68 wakipinga vikali hatua hiyo. Hii inaonyesha kuwa hata wale waliokubali mashambulizi ya anga hawako tayari kubeba gharama nzito za vita vya nchi kavu. Wamarekani wanatambua vyema kwamba vita vya nje huweka mzigo mkubwa kwa walipa kodi, na waathirika wakuu huwa wananchi wa kawaida, si wanasiasa au makampuni ya kijeshi na viwanda.
Ingawa asilimia 82 ya Warepublican waliunga mkono mashambulizi ya anga dhidi ya Iran, ni asilimia 44 pekee walio oneysha kuunga mkono kikamilifu hatua hiyo, jambo linaloonyesha mashaka ndani ya sehemu ya wafuasi wa Trump. Aidha, vijana walio na umri chini ya miaka 35 walipinga hatua hiyo kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko makundi mengine ya umri, huku kiwango cha imani yao kwa Trump kikiwa cha chini. Hii inaonyesha kuwa kizazi kipya cha Wamarekani kina mwelekeo mkubwa zaidi kuelekea diplomasia na kuepuka vita.
Kwa hivyo, upinzani mpana wa hujuma ya kijeshi ya utawala wa Trump dhidi ya Iran unaweza kuelezwa kama mchanganyiko wa kutokuwa na imani kwa uongozi wa kisiasa, hofu ya athari za kiusalama, mgongano na ahadi za kampeni za uchaguzi, wasiwasi kuhusu gharama za vita, na mgawanyiko wa kijamii.
Sababu hizi ziliungana na kusababisha Wamarekani wengi, hata sehemu ya wafuasi wa chama tawala cha Republican, kukataa hatua ya kijeshi dhidi ya Iran. Kwa hivyo, shambulio la Trump halikuweza kuunda mwafaka wa ndani, bali liliendeleza na kuzidisha mgawanyiko wa kisiasa na kijamii uliokuwepo Marekani. Tukio hili tena lilidhihirisha kwamba maoni ya umma nchini humo hayana hamu ya kuingia katika vita vipya.