
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Mkakati mpya wa Usalama wa Taifa wa Marekani (NSS) unaobainisha misingi na vipaumbele vya Washington katika sera za nje kimsingi ni hati ya usalama kwa ajili ya utawala wa kizayuni wa Israel.
Esmaeil Baghaei ameeleza hayo katika mkutano na waandishi wa habari jana Jumapili, siku mbili baada ya serikali ya Rais wa Marekani Donald Trump kuzindua NSS ya 2025.
Baghaei amesema NSS imeweka wazi malengo ambayo serikali moja baada ya nyingine ya Marekani imekuwa ikiyafuatilia kwa muda mrefu kwa kutumia ulaghai wa haki za binadamu na demokrasia.
Waraka huo wa kurasa 33 umesema Asia Magharibi si kipaumbele tena cha juu cha kimkakati cha Washington, ukiielezea akiba ya nishati ya eneo hili kama “sababu ya kihistoria” inayoifanya Marekani ilitilie maanani.
Baghaei amebainisha pia kwamba, kuhakikisha Marekani inazitia mkononi rasilimali za nishati za eneo la Asia Magharibi na kudhamini usalama wa utawala wa Kizayuni ni masuala mawili ya msingi yaliyotajwa katika waraka huo kuhusiana na eneo hili.
“Kimsingi, muhtawa wa waraka huo unaonyesha kwamba Marekani inachukua nafasi ya jaji juu ya nchi zote, jambo ambalo hakuna upande wowote katika ulimwengu wa leo unaokubaliana nalo” ameeleza Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran.
Baghaei amefafanua kwa kusema, lakini mbali na hayo, kutoashiriwa chochote kuhusu haki za Palestina kunathibitisha ukweli kwamba hati hiyo, badala ya zaidi kuwa ni Mkakati wa Usalama wa Taifa wa Marekani, inazingatia zaidi – kwa uchache kuhusiana na Asia Magharibi – mkakati wa usalama wa taifa wa utawala wa Kizayuni…/