
Mapigano yanaendelea mashariki mwa DRC licha ya kusainiwa kwa makubaliano ya amani kati ya Kinshasa na Kigali chini ya usimamizi wa Rais wa Marekani Donald Trump siku ya Alhamisi, Desemba 4. Mwishoni mwa wiki hii, mapigano yalikuwa makali sana huko Kivu Kusini, katika eneo la Uvira.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Licha ya kusainiwa kwa makubaliano ya amani kati ya Kigali na Kinshasa siku ya Alhamisi, Desemba 4, huko Washington chini ya usimamizi wa Rais wa Marekani Donald Trump, mapigano yanaendelea mashariki mwa DRC. Siku ya Jumapili, Desemba 7, mapigano kati ya AFC/M23 inayoungwa mkono na Rwanda na jeshi la Kongo, likisaidiwa na wanajeshi wa Burundi na wanamgambo wa Wazalendo, yaliripotiwa katika mkoa wa Kivu Kusini.
Mapigano makali zaidi yaliripotiwa kaskazini mwa jiji la Uvira, katika uwanda wa Mto Ruzizi, ambapo wapiganaji wa AFC/M23 waliingia katika kijiji cha Luvungi, ambapo wakazi wake waliondoka mapema. Askari wa Kongo au wa Burundi, wala wapiganaji wowote wa Wazalendo hawakuepo katika mji huo, jambo lililomshangaza mwakilishi wa mashirika ya kiraia wa eneo hilo ambaye alijiuliza kwa nini “watu wote waliondoka katika mji huo.” Ili kuonyesha uwepo wao huko Luvungi, waasi walirusha picha zao kwenye mitandao ya kijamii kutoka maeneo mbalimbali kote mjini humo.
Wakati mabomu yakiendelea kuanguka, wakazi wa vijiji vya Bwegera, Luberizi, na Mutarule, vilivyoko kusini mwa Luvungi, walikimbilia Sange, mwanamume mmoja ambaye aliwapoteza wanawe wawili ameambia RFI. Hali hii inayafanya mashirika ya kiraia ya Uvira kuwa na hofu ya kutokea kwa janga la kibinadamu kutokana na idadi kubwa ya watu waliokimbia makazi yao.
ICRC inasikitishwa kutoweza kuvuka mstari wa mbele
Hata hivyo, huko Uvira, hali bado ni shwari kwa sasa, huku gavana wa mkoa wa Kivu Kusini, Jean-Jacques Purusi Sadiki, akiwataka raia wenzake kuwa watulivu, na jeshi la Kongo linakanusha kukamatwa kwa maeneo kadhaa yanayozunguka mji huo, pia likionya dhidi ya uvumi unaoenezwa “na maadui wa amani” kwenye mitandao ya kijamii.
Katika taarifa, Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) inalaani mapigano yanayoendelea, ambayo yanazuia uhamishaji wa waliojeruhiwa hadi Uvira, ambapo shirika hilo linasema limeweza kusafirisha raia 21 pekee, wakiwemo watoto 7. “Kutokana na mapigano makubwa katika mstari wa mbele, ni vigumu sana kwa timu za ICRC kuvuka ili kurahisisha upatikanaji wa huduma na matibabu kwa raia,” anabainisha Djibril Mamadou Diallo, mkuu wa ofisi ya ICRC huko Uvira, ambaye ameoneza: “Leo, changamoto kuu inabaki kuwa na uwezo wa kuvuka mistari hii ili kuwahamisha waliojeruhiwa, lakini pia kutoa msaada muhimu wa kibinadamu kwa utendaji kazi wa vituo vya afya.”