
Rais wa Marekani Donald Trump amesema Jumapili jioni kwamba “anasikitishwa” kuona mwenzake wa Ukraine “bado hajasoma” pendekezo la Marekani lililofichuliwa wiki tatu zilizopita kwa ajili ya kutatua mgogoro nchini Ukraine. Kwa upande wake, Volodymyr Zelensky anatarajia kukutana na washirika wake wa Ulaya Keir Starmer, Emmanuel Macron, na Friedrich Merz jijini London leo Jumatatu.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Siku ya Jumapili, Desemba 7, Donald Trump amemkosoa mwenzake wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, kwa kutosoma pendekezo la amani kwa Ukraine lililofichuliwa wiki tatu zilizopita na Washington, ambalo ni mada ya mazungumzo tofauti na Moscow na Kyiv.
“Kwa hivyo tulizungumza na Rais (wa Urusi) Vladimir Putin, tulizungumza na vongozi wa Ukraine—akiwemo rais Zelensky—na lazima niseme nimesikitishwa kuona rais Zelensky bado hajasoma pendekezo la Marekani” kwa ajili ya suluhu nchini Ukraine, rais wa Marekani amesema, akihojiwa na waandishi wa habari katika sherehe huko Washington. “Haya ni matakwa ya Urusi, unajua, nadhani Urusi ingependelea kuwa na nchi nzima,” lakini “Sina uhakika kama hii itamridhisha Zelensky,” Donald Trump ameongeza.
Tangu kuwasilishwa kwa mpango wa Marekani karibu wiki tatu zilizopita, mazungumzo kadhaa yamefanyika na wajulbe wa Ukraine huko Geneva na Florida kujaribu kurekebisha maandishi kwa niaba ya Kyiv. Hati hiyo pia iliwasilishwa kwa Vladimir Putin siku ya Jumanne wakati wa ziara ya mjumbe wa Marekani Steve Witkoff na Jared Kushner, mkwe wa rais wa Marekani na mpatanishi asiye rasmi, huko Moscow.
Maelezo machache yameibuka kuhusu mpango huu uliorekebishwa, baada ya toleo la awali kuonekana na Kyiv na nchi za Ulaya kama linaloipendelea Urusi kwa kiasi kikubwa.
Volodymyr Zelensky jijini London
Volodymyr Zelensky anatarajia kukutana na washirika wake wa Ulaya Keir Starmer, Emmanuel Macron, na Friedrich Merz jijini London leo Jumatatu. Rais wa Ukraine atapokelewa na Waziri Mkuu wa Uingereza, pamoja na Rais wa Ufaransa na Kansela wa Ujerumani.
Mkutano huo unakusudiwa kupitia “mazungumzo yanayoendelea ndani ya mfumo wa upatanishi wa Marekani,” Emmanuel Macron aliandika Jumamosi kwenye mtandao wa kijamii wa X, akiahidi “kuendelea kuiwekea shinikizo Urusi ili kuilazimisha kufanya amani.”
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Yvette Cooper anatarajiwa mjini Washington kukutana na mwenzake wa Marekani, Marco Rubio, kama sehemu ya juhudi kubwa za kidiplomasia za kujaribu kukomesha vita nchini Ukraine vilivyosababishwa na mashambulizi ya Urusi ya Februari 24, 2022.
Uingereza na Marekani zinatarajiwa kuthibitisha tena “ahadi yao ya kufikia makubaliano ya amani nchini Ukraine,” Wizara ya Mambo ya Nje imetangaza, ikiongeza kuwa London inaunga mkono “juhudi zinazoendelea za Rais Trump za kuhakikisha amani ya haki na ya kudumu.”