Netanyahu aliyazungumza hayo wakati wa mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, aliyemtembelea na alisisitiza kwamba awamu ya pili, ambayo itashughulikia kuwapokonya silaha wapiganaji wa Hamas na kuondolewa kwa wanajeshi wa Israel kutoka Gaza, inaweza kuanza mwisho wa mwezi huu.

Hamas bado haijakabidhi mabaki ya mateka mmoja anayeitwa Ran Gvili, aliyekuwa afisa wa polisi mwenye umri wa miaka 24 na amabye aliuawa katika mashambulio ya Hamas yaliyofanyika Oktoba 7, mwaka 2023 na mwili wake ulipelekwa Gaza.

Israel Jerusalem 2025 | Friedrich Merz na Benjamin Netanyahu
Kushoto: Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz. Kulia: Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Hatua hiyo ya pili ya kusitisha mapigano pia itajumuisha kupelekwa kwa kikosi cha kimataifa ili kuulinda Ukanda wa Gaza na kusimamia kuundwa kwa serikali ya muda ya Palestina itakayoendesha mambo ya kila siku chini ya usimamizi wa bodi ya kimataifa itakayoongozwa na Rais wa Marekani Donald Trump.

Hamas yasemaje?

Afisa mkuu wa Hamas, Bassem Naim, aliye katika ofisi ya kisiasa inayohusika na kufanya maamuzi ya Hamas ameliambia shirika la Habari la The Associated Press, kwamba kundi hilo liko tayari kujadili juu ya kuweka silaha zao chini kama sehemu ya kusitisha mapigano, hiyo ikiwa ni hatua mojawapo kati ya masuala magumu zaidi yaliyo mbele ya pande hio mbili za Israel na Hamas.

Tangu makubaliano ya kusitisha mapigano yaanze, Hamas imewarejesha mateka wote 20 walio hai na miili 27 kwa kubadilishana na wafungwa wapatao 2,000 wa Kipalestina.

Israel Jerusalem 2023 | Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Abir Sultan/AP Photo/picture alliance

Netanyahu kwenye mkutano na waandishi wa Habari pamoja na Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, mjini Jerusalem alibainisha kuwa baadaye mwezi huu, atakutana na Rais wa Marekani Donald Trump kujadili maendeleo ya awamu ya pili na alisisitiza msimamo wa Israel kwamba haitakubali kuanzishwa kwa taifa la Palestina.

Kwa upande wake Kansela Merz alisema Ujerumani inaunga mkono haki ya Israel ya kuwepo na usalama wake lakini pia alionyesha wazi mtazamo wa Ujerumani kuhusu kuunga mkono kuanzishwa kwa taifa huru la Palestina huku akipinga vitendo vya Israel vya kuuvamia na kutwaa kwa nguvu maeneo ya Ukingo wa Magharibi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *