Syria: Mwaka mmoja tangu kuanguka utawala wa AssadSyria: Mwaka mmoja tangu kuanguka utawala wa Assad

Akizungumza mjini Damascus, Rais Ahmed al-Sharaa amewataka Wasyria kuunganisha nguvu kujenga nchi yao, akiweka msisitizo kwenye umoja, uthabiti na kulinda mamlaka ya taifa katika hatua mpya ya kulijenga upya.

Rais huyo aliyeonekana kwenye mavazi ya kijeshi kama alivyofanya alipoingia Damascus mwaka mmoja uliopita, alitumia hotuba yake kusifu “ushujaa na kujitolea” kwa wapiganaji waliouangusha utawala wa  Assad baada ya vita vilivyodumu takribani miaka 14.

Katika uwanja wa Umayyad na maeneo mengine ya Damascus, maelfu ya wananchi wamejitokeza kuadhimisha kumbukumbu hiyo, huku gwaride la kijeshi likipamba kilele cha sherehe. Sherehe hizi zimekuja wakati serikali ikiwa imepata uungwaji mkono mpya kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwa vikwazo vingi vya nchi za Magharibi na kuboresha mahusiano na mataifa ya Ghuba, Marekani na Uturuki.

Serikali mpya yakabiliwa na changamoto lukuki

Hata hivyo, licha ya mafanikio hayo ya kidiplomasia, changamoto nzito zimeendelea kuikumba nchi hiyo. Matukio ya umwagaji damu katika maeneo ya jamii za Alawi na Druze yameibua mashaka kuhusu uthabiti wa taifa, huku operesheni za kijeshi za Israel zikiendelea kutikisa kipindi cha mpito.

Syrien Damaskus 2025 | Gwaride la kijeshi
Maelfu ya wananchi wamejitokeza kuadhimisha mwaka mmoja tangu kuondolewa utawala wa Assad huku gwaride la kijeshi likipamba kilele cha sherehe. Picha: Omar Sanadiki/AP Photo/picture alliance

Wananchi wengi, hasa wa jamii za walio wachache, bado wana wasiwasi juu ya uwezo wa serikali mpya kulinda usalama na haki zao.  Familia za waliopoteza wapendwa wao wakati wa utawala wa Assad pia bado zinatafuta majibu. Mkuu wa Amnesty International Agnes Callamard, anasema serikali inapaswa kuwasikiliza watu hao:

“Jambo muhimu zaidi ambalo serikali na tume za kitaifa zinaweza kufanya kwa sasa ni kuhakikisha kwamba familia zinahisi zinasikilizwa na zinaungwa mkono.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amesisitiza kuwa safari ya Syria kuelekea maridhiano na ustawi ni ndefu kuliko mabadiliko ya kisiasa pekee. Kwenye taarifa yake alisema kuwa nchi hiyo ina nafasi ya “kujenga upya jamii zilizovunjika na kuponya migawanyiko ya muda mrefu,” akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuisaidia Syria katika juhudi hizo za mpito.

Upinzani waipinga serikali ya Sharaa

Mbali na hilo, sauti za upinzani zimeonekana katika baadhi ya makundi ya wachache. Kiongozi mmoja mashuhuri wa kiroho wa jamii ya Alawi aliwataka wafuasi wake kususia sherehe hizo, akipinga kile alichokiita uonevu wa utawala mpya. Wakati huohuo, utawala wa Kikurdi unaodhibiti maeneo ya kaskazini mashariki umetangaza marufuku ya mikusanyiko kutokana na hofu za kiusalama, licha ya makubaliano maalum ya kuunganishwa na serikali kuu kabla ya mwisho wa mwaka kuendelea kusuasua.

Syrien Damaskus 2025 | Rais Ahmad al-Sharaa
Rais Ahmed al -Sharaa alionekana kwenye mavazi ya kijeshi kama alivyofanya alipoingia Damascus mwaka mmoja uliopita.Picha: Syrian Presidency/Handout/Anadolu/picture alliance

Kiongozi wa Kikurdi, Mazloum Abdi, kupitia mtandao wa X, amesisitiza kuwa makubaliano hayo ndiyo msingi wa kujenga Syria “ya kidemokrasia na iliyogatuliwa madaraka,” akibainisha kuwa bado wapo tayari kushirikiana na Damascus, licha ya changamoto za kisiasa na kiusalama zinazoendelea.

Sharaa kuendeleza kipindi cha mpito kwa miaka minne ijayo 

Katika upande mwingine wa mpito, Rais Ahmed al-Sharaa ametoa ahadi ya kuendeleza kipindi cha mpito kwa miaka minne ijayo ili kuweka misingi ya taasisi mpya, kuandika katiba inayotarajiwa kupigiwa kura na kuandaa uchaguzi wa taifa. Hata hivyo, serikali yake inakabiliwa na changamoto za kusimamia mchakato huo, ikiwemo kukamilisha uteuzi wa theluthi ya wabunge 210 kama ilivyoainishwa kwenye katiba ya muda.

Zaidi ya watu laki moja wameuawa katika vita, huku mamilioni wakiyakimbia makazi yao ndani na nje ya Syria tangu 2011. Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi linaripoti kuwa raia zaidi ya milioni 1.2 wamerejea nyumbani tangu Assad aangushwe, lakini wafadhili wa kimataifa wanapunguza misaada, hatua inayoweza kuathiri mustakabali wa wakimbizi na waliohamishwa.

Hali ya kibinadamu bado ni mbaya, na takwimu za Shirika la kiutu la Umoja wa Mataifa, OCHA zinaonesha kuwa watu milioni 16.5 wanahitaji msaada mwaka 2025. Hata hivyo, serikali inasema kurejea kwa takriban wakimbizi milioni 1.5 kumeanza kuutoa uchumi kwenye hali ya kukwama na kutoa matumaini ya kufufuka kwa taifa lililojeruhiwa na vita.

Mzozo wa Sweida na sura zake kijamii, kisiasa na kimataifa

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *