Kordofan, inayojumuisha majimbo ya Kordofan Kaskazini, Kati na Kusini, ni eneo lenye umuhimu mkubwa kimkakati kwa sababu linatenganisha Darfur inayodhibitiwa na RSF na maeneo ya kati na mashariki yanayoshikiliwa na jeshi.
Kupotea au kushikiliwa kwa mkoa huu kunaweza kubadili mwelekeo wa vita. Zaidi ya hayo, Kordofan ni kituo cha utajiri wa mafuta, dhahabu na mazao muhimu ya kilimo, rasilimali ambazo sasa zimegeuka kuwa chanzo cha mapigano makali kutokana na umuhimu wake katika kufadhili vita vya pande zote mbili.
Katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita, mapigano yameripotiwa kuongezeka katika miji kama El-Obeid, Kadugli, Babanusa na Dilling, ambapo maelfu ya wakazi wanaripotiwa kukwama bila chakula, dawa na huduma za msingi kutokana na mizingiro na mashambulizi ya mara kwa mara.
Wasiwasi watanda kufuatia RSF kudhibiti maeneo mengi
Ushindi wa RSF katika baadhi ya maeneo ya Kordofan umeanza kuiweka hatarini miji ya katikati ya Sudan, na kuzua hofu kuwa Khartoum inaweza kuwa shabaha ya mwisho la mashambulizi hayo.
Katikati ya wasiwasi huo, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, ametahadharisha juu ya dalili za ukatili unaoongezeka na hatari ya kurudiwa kwa mauaji ya kimbari. Ametoa kauli kali akisema:
“Nahofia kutokea wimbi jipya la madhila na ukatili Sudan wakati mapambano makali yanaendelea kwenye eneo la Kordofan. Kamwe tusiruhusu yaliyojiri El Fasher kushuhudiwa Kordofan. Tangu tarehe 25 Oktoba pale wapiganaji wa RSF walipoudhibiti mji wa Bara ulioko Kaskazini ya Kordofan,afisi yangu imenakili mauaji yasiyopungua 269 ya Raia wa kawaida… yaliyotokana na mashambulizi ya angani , makombora na mauaji ya kikatili.”
Athari za kibinadamu zimefikia kiwango cha kutisha
Kauli yake imeongeza uzito kwa onyo la kimataifa kuhusu kuzama kwa Sudan kwenye mgogoro mpya na mkubwa zaidi.
Kwa upande wa vikosi vinavyopambana, Jeshi la Sudan chini ya Abdel Fattah al-Burhan linategemea zana nzito za Kichina, ndege za zamani na droni zinazotolewa na Iran na Uturuki.
RSF ya Mohamed Hamdan Daglo (Hemedti), ikiwa na mizizi katika kundi la wanamgambo la Janjaweed, imepanua ushawishi wake kwa kuungana na kundi la SPLM-N la Abdel Aziz al-Hilu katika Milima ya Nuba na Blue Nile, hatua inayoiimarisha katika maeneo yaliyokuwa ngome za waasi.
Wakati huo huo, athari za kibinadamu zimefikia kiwango cha kutisha. Umoja wa Mataifa umetangaza njaa kali mjini Kadugli na kutoa onyo la hali ile ile katika eneo la Dilling. Mashambulizi ya droni na makombora yameua raia wengi, wakiwemo watoto waliokuwa chekechea huko Kalogi na zaidi ya watu 45 waliouawa kwenye hafla ya mazishi mjini El-Obeid.
Aidha, mashambulizi ya jeshi huko Kauda mwezi uliopita yameongeza idadi ya vifo, yakionyesha kiwango cha hatari kwa raia katika maeneo yote ya Kordofan. Jumla ya watu 45,000 wamekimbia makazi yao katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita pekee, na kuongeza kwenye idadi inayokaribia watu milioni 12 waliotawanywa tangu vita kuanza.
Mashirika ya kimataifa yapo katika hali ya tahadhari, yakihofia kuwa Kordofan inaweza kuwa kitovu kipya cha vita vya muda mrefu na mauaji ya kinyama, ikiwa juhudi za kusimamisha mapigano hazitachukuliwa haraka.