Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya mwaka ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), mashirika zaidi 10 na kaunti zinachunguzwa kwa ufisadi wa mabilioni ya fedha.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Shirika la Maendeleo ya Ngozi nchini Kenya ndilo linaongoza kwa kukiuka sheria za ununuzi baada ya kutajwa katika zabuni ya Shilingi bilioni 2.5 ya ujenzi wa mtambo wa majitaka. Katika kipindi hicho, tume ilichunguza visa 838 vya ufisadi na uhalifu wa kiuchumi unaoendelea, na iliwasilisha faili 175 zilizokamilika kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka ya Umma.
EACC pia iliongeza juhudi za kurejesha mali kama anavyosema Afisa Mkuu Mtendaji wa tume ya EACC Abdi Mohammed. “Kupitia kesi hizi, tume inanuia kurejesha mali iliyopatikana kwa njia haramu yenye kima cha thamani ya shilingi bilioni 4.8 za Kenya, katika kipindi hicho tume ilirejesha mali yenye thamani ya shilingi bilioni 3.4.”
Kuchunguzwa kwa aliyekuwa gavana wa jimbo la Mandera
Katika jimbo la Mandera, aliyekuwa gavana anachunguzwa kwa tuhuma za mgongano wa maslahi kutokana na malipo yasiyo ya kawaida kwa kampuni 10 zilizofanya biashara na kaunti hiyo kati ya mwaka 2013 na 2020, zikihusisha Shilingi bilioni moja. Majimbo mengine yanayochunguzwa ni Kajiado, Wajir, Kiambu, Turkana, Trans Nzoia, Bomet, Embu, Garissa, Trans Nzoia na Siaya, ambayo yanahusishwa na kutengeneza zabuni za bei ya juu kupita kiasi, mgongano wa maslahi na malipo ya udanganyifu yanayohusishwa na maafisa wa umma.
Aidha udanganyifu wa vyeti miongoni mwa maafisa wa serikali wa Kenya umekithiri kama anavyosema mwenyekiti wa Tume ya EACC David Oginde.”Uadilifu lazimi uzingatiwe katika kila kiwango cha maendeleo yetu, inasikitisha sana kuwa hata maafisa wakuu serikalini wanatumia nyaraka ghushi.”
Utoaji wa kiwango cha juu wa zabuni ya shilingi bilioni 1.3
Miongoni mwa kesi za kiwango cha juu ni uchunguzi kuhusu utoaji usio wa kawaida wa zabuni wa Shilingi bilioni 1.3 na Baraza la Madaktari na Madaktari wa Meno nchini kwa ujenzi wa kituo cha mafunzo pamoja na ubadhirifu wa Shilingi bilioni 1.3 na Shirika la Umeme la Kenya katika ujenzi wa mtambo wa nishati ya upepo eneo la Lamu West.
Serikali ya Kenya imekuwa ikipambana na ufisadi kupitia uchunguzi wa EACC, kufikishwa kortini kwa washukiwa na kuimarisha mifumo ya kidijitali ili kufuatilia matumizi ya fedha. Pia imeweka sheria kali zaidi za ununuzi, kufanya ukaguzi wa mali za maafisa na kupambana na utakatishaji fedha kupitia uchunguzi wa kibenki. Hata hivyo, juhudi hizi mara nyingi hukwamishwa na ushawishi wa kisiasa, ucheleweshaji wa kesi mahakamani na ufisadi uliokita mizizi katika taasisi za umma.
DW, Nairobi