
Ripoti kutoka Kenya zinasema, washirika wa Rais William Ruto wa nchi hiyo katika eneo la Mlima Kenya wamebuni mpango kabambe unaolenga kuhakikisha atapata angalau kura milioni mbili kumwezesha kurejea Ikulu katika uchaguzi wa 2027.
Mpango huo unahusisha kugawa eneo la Mlima Kenya katika makundi kadhaa ya wapiga kura ili kuzuia ushawishi wa Muungano wa Upinzani katika eneo hilo.
Takwimu zinaonyesha kuwa, mwaka 2022, Rais Ruto alipata asilimia 87 ya kura za eneo la Mlima Kenya, takriban nusu ya kura zote zilizompa ushindi.
Hata hivyo, tangu wakati huo uhusiano kati yake na eneo hilo umekuwa ukivurugika, hali ambayo imesababisha uhasama na migawanyiko ndani ya chama tawala cha UDA kilichowahi kushinda zaidi ya asilimia 95 ya viti katika eneo hilo.
Chanzo kikuu cha mvutano huo ni kutimuliwa aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua, mnamo Oktoba mwaka jana baada ya kuhudumu kwa miaka miwili.
Gachagua, aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, alitimuliwa na Bunge la Seneti miezi kadhaa iliyopita kwa mashtaka matano kati ya 11 yaliyowasilishwa dhidi yake, yakiwemo kuchochea migawanyiko ya kikabila na kuhujumu Idara ya Mahakama.
Mwanasiasa huyo ameanzisha chama kipya cha siasa, Democracy for Citizens Party (DCP), akikitaja kama chombo maalum cha Mlima Kenya kuzuia kuchaguliwa tena kwa Rais Ruto mnamo 2027.
Vilevile ameungana na viongozi wa upinzani akiwemo kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa DAP-Kenya Eugene Wamalwa, Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, Naibu Kiongozi wa Jubilee Fred Matiang’i na Seneta wa Kajiado Kerrar Seki kuanzisha vuguvugu la ‘Wantam’.