Ripoti ya Shirika la Kitaifa la Uchunguzi wa Ubaguzi la serikali ya Ujerumani imefichua kwamba Waislamu na watu weusi wanaoishi nchini humo wanasumbuliwa na “ubaguzi wa kimfumo” kuhusu hali ya makazi.

Matokeo ya ripoti hiyo, yenye kichwa cha habari “Kukosekana kwa Usawa katika Maisha, Ubaguzi wa Rangi na Hali ya Makazi,” yalitangazwa katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika mji mkuu, Berlin, Jumatatu iliyopita.

Ripoti hiyo, ambayo imetokana na utafiti wa maoni kwa watu 9,512, imehitimisha kwamba watu weusi, Waislamu na wengine wasio Wajerumani wanasumbuliwa na “ubaguzi wa kimfumo” katika sekta ya makazi.

Imeeleza kwamba watu weusi na Waislamu wanaishi katika “mazingira magumu na maskini zaidi kuliko Wajerumani, wana mikataba ya kukodisha nyumba isiyo salama na mara nyingi hubaguliwa katika vitongoji vyao.”

Ripoti ya Shirika la Kitaifa la Uchunguzi wa Ubaguzi la serikali ya Ujerumani imeongeza kuwa karibu 50% ya Waislamu na watu weusi wanasema nafasi zao za kupata makazi ni ndogo ikilinganishwa na watu wa dini na mbari nyingine.

Awali, ripoti ya kila mwaka iliyotolewa na mtandao wa “Klem”, unaofuatilia ubaguzi wa rangi dhidi ya Waislamu nchini Ujerumani, ilifichua ongezeko kubwa la idadi ya visa vya ubaguzi dhidi ya Waislamu katika mwaka uliopita wa 2024.

Ripoti hiyo ilionyesha kuwa waathiriwa hujiepusha kwenda kwenye vyombo rasmi kutoa taarifa au kuomba msaada, hasa katika mazingira ya shule, ambapo wazazi wanaogopa kwamba watoto wao watachukuliwa hatua za kulipiza kisasi.

Josine Jehan, mwakilishi wa mtandao wa “Klem”, ameyataja baadhi ya matukio hayo kuwa ni “ya kikatili sana na yanaonyesha dharau kwa utu wa binadamu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *