Tangu mwaka 2006, Mfuko wa Dharura wa Umoja wa Mataifa (CERF) umetenga karibu dola bilioni 10 kwa zaidi ya nchi 110 kupitia ufadhili wa haraka na wa kimkakati, mara nyingi ukipatikana kabla ya vyanzo vingine vya misaada, na kuokoa maisha mengi.

Lakini kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya kibinadamu kunakosababishwa na kuongezeka kwa migogoro, “rasilimali zimekaribia kuisha, mamilioni ya maisha yako hatarini,” amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, akiwahimiza washiriki kufikia lengo la kuchangia dola bilioni moja kwa ajili ya CERF.

“Miaka ishirini iliyopita, wakati CERF ilipoanzishwa, jamii ya kimataifa ilitoa ahadi rahisi: ikitokea janga, msaada ungefika,” amesema. “Leo, nawaomba mhuishe ahadi hiyo.”

Athari inayonekana

Mkutano wa wafadhili umefanyika siku moja baada ya Umoja wa Mataifa kuzindua mpango wake wa kibinadamu wa kimataifa wa mwaka 2026, unaolenga kuwasaidia watu milioni 87 wenye mazingira magumu kupita kiasi katika nchi 50.

“Kama sehemu ya juhudi hizi za kimataifa, CERF ni mfuko wetu wa dharura unaochukua hatua kwa haraka na kwa kubadilika,” amebainisha Katibu Mkuu. “Katika maeneo mengi, CERF ndiyo hutofautisha kati ya kupata msaada wa kuokoa maisha na kutopata msaada kabisa.”

Wakati upatikanaji wa kibinadamu uliporejeshwa Gaza, CERF ilisaidia kuhakikisha upatikanaji wa mafuta yaliyohitajika kuendesha hospitali, mitandao ya maji, na huduma nyingine muhimu. Mfuko huo ulikuwepo wakati vita ilipoanza Ukraine mwaka 2022 na uliweza kuingilia ndani ya saa chache.

Zaidi ya dola milioni 110 zimetolewa mwaka huu kwa dharura zilizopuuzwa na kufadhiliwa kidogo, ikiwemo Afghanistan na Somalia. Pia nchi za Karibiani zilipokea ufadhili, msaada wa uokoaji, na mahitaji ya dharura baada ya Kimbunga Melissa mnamo Oktoba.

Kengele ya hatari

CERF hupokea msaada kutoka kwa nchi wanachama, serikali za kikanda, mashirika ya kimataifa, sekta binafsi, watu binafsi na wafadhili wengine.

Hata hivyo, michango imepungua kwa kiwango kikubwa mwaka huu na inatarajiwa kufikia kiwango cha chini zaidi katika kipindi cha miaka kumi, alionya Tom Fletcher, Mratibu wa Misaada ya Dharura wa Umoja wa Mataifa.

“Tunapohitajika kufanya kazi kwa uwezo kamili, kengele za hatari hupiga,” alisema. “Hili sio tu suala la ukosefu wa fedha. Ni dharura ya kiutendaji. Ikiwa CERF itadhoofika, mfumo wa kimataifa wa kukabiliana na dharura utayumba, na watu wanaotegemea msaada wetu watateseka.”

Kuimarisha rasilimali

Bwana Fletcher ametangaza mfuko wa dola milioni 100 kwa ajili ya hali za dharura zinazofadhiliwa kidogo zaidi duniani, ambao ni takriban robo ya mapato yanayotarajiwa kwa mwaka 2025.

Ireland na Ufilipino wameandaa kwa pamoja tukio la leo, na serikali zote mbili zilikazia umuhimu wa kuunga mkono CERF.

Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Ireland, Neale Richmond, amesema nchi yake italipa nyongeza ya euro milioni 1 mwaka 2026, na kupeleka jumla ya mchango hadi euro milioni 21.5.

Huku akikiri kuwa “ufadhili sio suluhisho pekee” kwa migogoro ya kibinadamu, kwa sababu “suluhisho sahihi za kisiasa zinahitajika,” aliongeza kuwa suluhisho hizo bado hazijapatikana.

“Wajibu wa maadili”

“Wakati huohuo, tuna wajibu wa kimaadili kuhakikisha kwamba watu waliokwama katika migogoro ambayo haipewi uzito kwenye vyombo vya habari, au ambayo haijawahi kupewa, hawasahauliki,” amesema katika ujumbe wa video.

Tangu kuanzishwa kwake, Ufilipino imetoa takriban dola milioni 1 kwa CERF, ikiongezeka kutoka michango ya dola 5,000 hadi 10,000 mwanzoni hadi karibu dola 250,000 mwaka huu. Dola 200,000 zaidi zitatolewa mwaka 2026.

Waziri wa Mambo ya Nje Theresa Lazaro amebainisha kuwa CERF ilitoa haraka karibu dola milioni 6 siku chache kabla ya Kimbunga Kikubwa Fung-wong kupiga mwezi Novemba, pamoja na msaada wake muhimu katika majanga yaliyotangulia.

“Kwa kuwezesha mashirika ya Umoja wa Mataifa kutoa huduma muhimu kama chakula, malazi, na matibabu, CERF imekuwa mwanga wa matumaini kwa watu waliokumbwa na majanga,” alisema katika ujumbe wa video.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *