Kenya. Mwaka 2011, Judy Wanyoike raia wa Kenya, alianza kupata maumivu ya mgongo na kutokwa na damu ukeni, dalili ambazo hapo awali hakuweza kuzifafanua.
Hali hii iliendelea kwa miezi kadhaa hadi mwaka wa 2012 alipoambiwa kuwa alikuwa na saratani ya shingo ya kizazi.
“Nilikua nimeenda kwenye semina ya kanisa ya wiki moja huko Naivasha, ambapo mojawapo ya shughuli ilikuwa uchunguzi wa Pap Smear,” anakumbuka.
Kwa mshangao wake, madaktari waligundua hitilafu wakati wa uchunguzi huo, na bila kupoteza muda akashauriwa kwenda katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta KNH kwa vipimo zaidi.
“Baadaye ilithibitishwa kuwa nilikuwa na saratani ya mlango wa uzazi ya hatua ya 2B.”
Ili kukabiliana na hali hii, Wanyoike alifanyiwa upasuaji wa kuondoa mfuko wa uzazi, utaratibu uliondamana na matibabu ya tibakemia, tibaredio na utaratibu wa brachytherapy, ambapo baadaye alianza kupata nafuu.
Hata hivyo, mwaka wa 2019, saratani hii ilirudi. “Sikuweza kwenda kwenda haja kubwa,” anasema.
Kufika Septemba mwaka huo, hali yake ilikuwa imezidi kuwa mbaya kiasi kwamba hakuweza hata kupitisha hewa tumboni.
“Uchunguzi zaidi ulionyesha kuwa nilikuwa na uvimbe, ambao ulitolewa kupitia upasuaji na kuonyesha kwamba ulikuwa na saratani.”
Wanyoike alianza matibabu ya tibakemia na tibaredio ambapo mwezi Aprili mwaka wa 2020, alikamilisha taratibu hizi zote.
Shida mpya
Lakini masaibu yake hayakuwa yamekwisha, kwani mwaka wa 2022, alianza kupata maumivu ya mgongo ambayo yalikuwa yamesambaa hadi shingoni.
“Nililazimika kufanyiwa tena vipindi vinne vya tibakemia na uchunguzi wa PET scan Agosti mwaka huu.”
Kulingana na wataalam, uwezekano wa saratani ya mlango wa kizazi kurudi hutegemea hatua ya saratani, aina ya matibabu na hali ya mgonjwa.
“Saratani hurudi pale seli za saratani zinapobaki mwilini baada ya matibabu na kuanza kukua tena,” anaeleza Dk Catherine Nyongesa, mtaalamu wa matibabu ya saratani jijini Nairobi.
Sababu kuu ya saratani kurejea, anasema, ni seli ndogo za saratani kubaki mwilini baada ya taratibu kama vile upasuaji, tibaredio na tibakemia.
Aidha, iwapo saratani itagundulika ikiwa tayari iko katika hatua ya juu, basi uwezekani wa kurejea huongezeka.
“Wakati huu, uwezekano wa maradhi haya kusambaa kwenye tishu au tezi za limfu huwa uko juu,”anaeleza Dk Nyongesa.
Tafiti za kitabibu zinaonyesha kuwa katika hatua za awali (Stage I) za saratani, uwezekano wa saratani ya mlango wa uzazi kurejea huwa kati ya asilimia tano na 15, na mara nyingi hujirudia katika kipindi cha kati ya miaka miwili na mitatu baada ya matibabu.
Kwa upande mwingine, aina hii ya saratani ikitambulika katika hatua ya pili au ya tatu (Stage II–III), uwezekano wa kurejea huongezeka na kuwa kati ya asilimia 30 na 40, huku iwapo ugonjwa huu utagundulika katika hatua za mwisho (Stage IV), hatari ya kurejea tena huwa imeongezeka pakubwa na kufikia asilimia 50.
“Katika hatua hii, ni vigumu kuondoa saratani yote kabisa,” anaeleza.
Kwa mujibu wa DkNyongesa, tatizo ni kwamba wanawake wengi huchelewa kwenda kufanyiwa uchunguzi, hivyo maradhi haya yanapogundulika, tayari huwa yamesambaa.
“Kwa bahati mbaya, hakuna ishara za mapema za maradhi haya, kumaanisha kuwa sio rahisi kwa mgonjwa kutambua kuwa ana tatizo. Tatizo ni kwamba wanawake wengi huenda hospitalini wakiwa wamechelewa ambapo mara nyingi saratani hii huwa imeenea katika sehemu zingine, na hivyo kufanya iwe ngumu kupokea matibabu na kuokoa maisha ya mgonjwa,” anaeleza.
Kwa nini hurejea?
Kwa mujibu wa wataalamu, maambukizi sugu ya HPV (hasa aina 16 na 18) yanaweza kuchangia saratani kuzuka tena, au ikiwa baadhi ya seli sugu za saratani ambazo hazikuangamizwa kupitia tibakemia na mionzi, zilisalia.
Mbali na hayo, maradhi haya yanaweza kurejea ikiwa mfumo wa kingamwili ni dhaifu, au kulingana na mtindo wa maisha kama vile vutaji sigara, lishe duni, msongo wa mawazo na kutofuatilia matibabu ipaswavyo.
Kulingana na Dk Nyongesa, dalili zinazoweza kuashiria kurejea kwa saratani hiyo ni pamoja na maumivu ya nyonga au mgongo, kutokwa na damu au ute usio wa kawaida, ugumu wa kwenda haja ndogo au kubwa, kuumwa miguu au miguu kuvimba, na kupungua uzani bila sababu.
Njia bora ya kudhibiti maradhi haya, anasema, ni kufanya utambuzi wa mapema ambao hasa hufanywa kupitia uchunguzi wa pap smear unaosaidia madaktari kugundua vidonda au seli zisizo za kawaida kwenye lango la uzazi, na ambazo zinaweza kutibiwa kabla ya kugeuka na kuwa na uwezo wa kusababisha saratani.
Kwa mujibu wa mtaalam huyu, kupimwa ndio mbinu ya kutambua maradhi haya kwani inaweza kusaidia kuzuia aina nyingi za saratani ya mlango wa uzazi kwa kutambua mabadiliko yasiyo ya kawaida kwenye seli za mlango wa uzazi ili ziweze kutibiwa.
Kurejea kwa aina nyingine za saratani
Sio tu saratani ya mlango wa kizazi inayoweza kuzuka tena hata baada ya kupona.Wataalam wa afya kutoka vyanzo mbalimbali vya kimtandao, wanaeleza kuwa uwezekano wa saratani kurudi hutegemea kwa kiwango kikubwa aina ya saratani.
Baadhi ya saratani, kama ile ya matiti, koo, koloni, ovari na ubongo, zina tabia ya kurudi baada ya muda, hata pale mgonjwa anapoonekana amepona kabisa.
Katika baadhi ya matukio, seli za saratani huonekana zimemalizika kupitia tiba mbalimbali, lakini baadhi yake huenda zikabaki mwilini pasipo kugundulika na baadaye kuanza kukua tena.
Kuhusu sababu za kurudi wanasema ni pamoja na hatua ambayo saratani iligunduliwa. Madaktari hutumia neno “stage” kueleza kiwango ambacho saratani imefika.
Saratani zikigunduliwa mapema, hasa zikiwa katika hatua ya kwanza au ya pili, huwa na nafasi kubwa ya kuponywa bila kurudi.
Hata hivyo, zinapogunduliwa zikiwa tayari zimesambaa kwenye sehemu nyingine za mwili, hatari ya kurejea huwa kubwa zaidi. Hii ndiyo sababu kampeni za uchunguzi wa mapema zimekuwa zikipigiwa debe kwa nguvu na wataalamu wa afya.
Pili aina ya matibabu yaliyotolewa hutofautiana kulingana na mahali saratani ilipo, ukubwa wake, na afya ya mgonjwa. Matibabu kama upasuaji, mionzi, chemotherapy na immunotherapy hutumika ama kwa pamoja au kwa mfululizo ili kuhakikisha seli za saratani zinatokomezwa. Pamoja na jitihada hizi, bado uwezekano wa kurudi upo endapo seli chache zitabaki.
Mara nyingi, seli hizi hubadilika na kuwa sugu zaidi, jambo linaloweza kufanya matibabu ya mara ya pili kuwa changamoto.
Tatu, hali ya mwili wa mgonjwa pia ina athari kubwa. Mfumo wa kinga, umri, lishe na magonjwa mengine yanaweza kuathiri namna mwili unavyopambana na seli za saratani. Mgonjwa mwenye kinga imara huwa na nafasi nzuri zaidi ya kudhibiti uwezekano wa kurudi kwa ugonjwa.
Kwa kawaida, saratani inaporudi, inaweza kurudi katika namna tatu: sehemu ile ile, maeneo ya karibu, au sehemu za mbali zaidi kama mapafu, ini na mifupa. Kila aina ya kurudi huwa na mkakati wake wa matibabu na tathmini ya kitaalamu.
Habari njema ni kwamba, hata ikirudi, saratani mara nyingi inaweza kutibiwa tena. Madaktari huchunguza mabadiliko ya ugonjwa, hutumia vipimo maalumu na kupendekeza mbinu mpya za tiba kulingana na hatua na nguvu za mgonjwa. Wakati mwingine matibabu ya awali hurudiwa, na wakati mwingine tiba mpya hutumiwa.
Hata hivyo, msingi wa yote unabaki kuwa uchunguzi wa mapema, ufuatiliaji wa mara kwa mara na ushauri wa kitabibu.
Saratani inaweza kupona na ikarudi, lakini kwa mwamko sahihi wa kiafya, wagonjwa wengi wameendelea kuishi maisha marefu na yenye ubora mzuri, hata baada ya kukabiliana na ugonjwa huu mara kadhaa.