
PAMBA Jiji kwa sasa ipo katika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, lakini hiyo haina maana kama benchi la ufundi la timu hiyo limeridhika, kwani limesema lipo katika msako wa beki wa kati na linapanga kuwatema nyota kadhaa ili kuimarisha kikosi kwa ngwe inayofuata.
Timu hiyo iliyorejea Ligi Kuu msimu uliopita baada ya kuisotea kwa miaka karibu 23 tangu iliposhuka mwaka 2001, imekusanya pointi 16 kama ilizonazo Yanga ila zimetofautiana mabao ya kufunga na kufungwa, baada ya kucheza mechi tisa ikishinda nne, sare nne na kufungwa moja. Yanga imecheza mechi sita.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha mkuu wa timu hiyo, Francis Baraza amesema hana mpango wa kuongeza wachezaji wengi katika dirisha lijalo linalotarajia kufunguliwa Januari mosi kutokana na idadi kubwa aliyonayo.
“Sitaki kuongeza wachezaji wengi kwa sababu wachezaji nilionao naona wana kitu tayari na wameonyesha utayari wa kuipambania timu hivyo nilichopanga ni kupunguza kwa kuwatoa kwa mkopo baadhi,” amesema Baraza ambaye ni raia wa Kenya akiongeza;
“Natoa kwa mkopo kwa sababu namba ni kubwa na sehemu ambayo nitaipigania sana kuongeza ni beki wa kati tu ni eneo ambalo linahitajika kuongeza nguvu ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya ushindani.”
Baraza amesema hawajaanza vibaya na upungufu alioona anaweza kuufanyia kazi kwa kutumia wachezaji alionao bila kuongeza idadi kubwa ya wachezaji.
“Siwezi kufanya maboresho kwa sababu wapinzani wanafanya hivyo nimekaa na timu na kubaini kuwa nina wachezaji wengi wazuri na wanafanya kazi kwa usahihi.”