Ajenda ya mkutano huu imejumuisha masuala muhimu kuanzia kuokoa barafu za milimani zinazoendelea kuyeyuka, kudhibiti milipuko mikubwa ya mwani baharini, hadi kupunguza athari za kimazingira za teknolojia ya akili mnemba. Lakini ujumbe wa msingi ni mmoja mabadiliko ya tabianchi, kupotea kwa bioanuai, na uchafuzi wa mazingira vinaongezeka kwa kasi isiyowahi kushuhudiwa.

Ngamia akiwa amesimama katika bustani ya mashine za upepo nje kidogo ya Nouakchott, Mauritania.

© UNDP Mauritania/Freya Morales

Ngamia akiwa amesimama katika bustani ya mashine za upepo nje kidogo ya Nouakchott, Mauritania.

Tuwekeze katika mustakabali usio na uchafuzi: Mkuu wa UNEP

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP, Inger Andersen, alifungua kikao hicho kwa ujumbe mzito kwamba dunia inakaribia kuvuka mstari wa hatari lakini bado ina uwezo wa kujiokoa iwapo hatua Madhubuti zitachukuliwa sasa.

“Tukiwekeza katika tabianchi tulivu, tukiwekeza katika asili yenye afya, katika ardhi yenye rutuba, katika dunia isiyo na uchafuzi,” Andersen amesema, “basi dunia inaweza kupata faida kubwa kiuchumi, kuepusha vifo vya mapema kwa mamilioni ya watu, kuwaondoa mamilioni ya watu kwenye umasikini na njaa, na kuleta usawa na haki ya tabianchi.”

Amesisitiza kuwa hakuna taifa linaloweza kukabiliana na changamoto hizi peke yake.

“Kwa sababu hakuna serikali inayoweza kushughulikia janga hili peke yake, na hakuna nchi inayoweza kulifanya hili kwa nguvu zake pekee, hatua lazima zibebe ushirikiano wa kimataifa, sekta kwa sekta, mipaka kwa mipaka,” amesema.

Andersen ameongeza kuwa UNEP na UNEA zimeonesha kwa vitendo kwamba ushirikiano wa kimataifa huleta matokeo halisi.
“Nawaomba leo mtazame mbali zaidi ya dhoruba na kuelekeza macho kwenye upeo. Kwa kufanya kazi pamoja, tunaweza kuhakikisha tabianchi thabiti, mazingira safi na endelevu, na dunia isiyo na uchafuzi kwa manufaa ya kila taifa, kila mtu na kila mtoto ambaye bado hajazaliwa.”

Paneli za Solar zikiwa katika ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Nairobi, Kenya. Kote duniani, nishati ya jua imethibitika kuwa nishati nafuu na rafiki kwa mazingira.

UN Kenya/Neil Thomas

Paneli za Solar zikiwa katika ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Nairobi, Kenya. Kote duniani, nishati ya jua imethibitika kuwa nishati nafuu na rafiki kwa mazingira.

Ruto: Afrika inalipa gharama ya janga ambalo haikulisababisha

Rais wa Kenya William Ruto, mwenyeji wa mkutano huo, ametoa wito wa kutafsiri matamko ya kimataifa kuwa hatua za vitendo.

“Kazi yetu hapa Nairobi ni kuzigeuza ishara hizi kuwa matokeo halisi na yanayotekelezeka dhidi ya majanga matatu ya kimazingira, mabadiliko ya tabianchi, kupotea kwa bioanuai, na uchafuzi wa mazingira,” amesema.

Rais Ruto amesisitiza kuwa kwa Afrika, athari za tabianchi si mjadala wa kinadharia au jambo la kufikirika.

“Kwa Afrika, mabadiliko ya tabianchi si hoja ya kubishaniwa. Ni uhalisia wa kila siku. Barani kote kuanzia kwenye mazao kushindwa kuvunwa shambani hadi mafuriko ya uharibifu mkubwa, kutoka kwenye dhoruba kali hadi migogoro inayochochewa na upungufu wa rasilimali, Waafrika wanalipa gharama ya janga  ambao hawakulianzisha.”

Amesema kuwa bara hili linahitaji hatua zinazojumuisha maendeleo, ulinzi wa mazingira na mnepo.

“Kazi yetu ni kuhakikisha kwamba kila uwekezaji kwenye viwanda, miundombinu na teknolojia unajenga mnepo, unalinda mazingira na unafungua fursa kwa watu,” alisema.

Ruto ameongeza kuwa uchumi na ulinzi wa mazingira lazima visonge pamoja.

“Hatuwezi kutenganisha ukuaji wa uchumi na uzalishaji wa hewa ukaa na uchafuzi,” alisema. “Tunaweza kuunda ajira mpya, viwanda vipya na masoko mapya. Lakini mabadiliko haya lazima yawe ya haki, ya kupatikana kwa wote na ya gharama nafuu.”

Uchafuzi wa hewa kutoka kwa viwanda unachangia katika kuongeza nyuzi joto.

Unsplash/Maxim Tolchinskiy

Uchafuzi wa hewa kutoka kwa viwanda unachangia katika kuongeza nyuzi joto.

Mjadala watafuta suluhu halisi kwa changamoto halisi

UNEA-7, iliyoanza Desemba 8 inafunga pazia leo 12 Desemba, na inalenga kuharakisha hatua duniani kwa kusaidia mataifa kubuni sera zinazoweza kutekelezwa kwa ufanisi ili kuyakinga mazingira na mustakabali wa vizazi vijavyo.

Kauli mbiu ya mkutano wa mwaka huu ni kutafuta “suluhu halisi kwa changamoto halisi za ulimwengu”  imekuwa wito kwa mataifa wakati yakikabiliana na tishio linaloongezeka kwa kasi dhidi ya mifumo ya asili ya dunia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *