
Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, amesema moja ya ahadi kubwa iliyobaki kuitimiza katika klabu hiyo ni kukamilisha ujenzi wa uwanja katika eneo la Twiga na Jangwani, jijini Dar es Salaam.
Hersi ametoa kauli hiyo leo Jumamosi, Julai 4, 2026, wakati wa sherehe za ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambao Yanga imechukua kwa mara ya tano mfululizo.
Akizungumza katika makao makuu ya klabu hiyo, Jangwani, Dar es Salaam, Hersi amesema ahadi ambayo anaendelea kukumbushwa na mashabiki na wanachama ni kuhakikisha mradi wa ujenzi wa uwanja unakamilika kama alivyowahi kuahidi.
“Paredi la msimu ujao tutakalofanya tutatafuta sehemu nyingine na si hapa tena Jangwani, kwa sababu mwakani ujenzi wa uwanja utakuwa unaendelea katika kipindi hicho,” alisema Hersi.
Aidha, Hersi alieleza kuwa mchakato mwingine uliosalia ni kuhakikisha ardhi waliyopewa na Serikali inabadilishwa kutoka mfumo wa umiliki wa wanachama kwenda katika mfumo wa kampuni itakayohusika moja kwa moja na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa uwanja huo.
“Serikali imetutaka mfumo wa ujenzi uwe wa kampuni na si wa wanachama kama tunavyojiendesha sasa. Ninaamini hilo litakuwa jambo rahisi kwa wanachama kuridhia mabadiliko haya ya kimuundo na uwekezaji,” amesema.
Hersi, ambaye anagombea tena nafasi ya urais wa klabu hiyo, amesema mchakato wa kuridhia ombi la Serikali utakamilika katika uchaguzi mkuu wa Yanga utakaofanyika Agosti 2, 2026.
Mbali na suala la uwanja, Hersi amewahakikishia mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kuwa Yanga itaendelea kupigania mataji mbalimbali katika msimu wa 2026/2027.