Leo Ijumaa, mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika mkutano wa kujadili hali DRC, mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa ameonya kuhusu hatari zinazotokana na mashambulizi haya mapya kwa umoja wa nchi na uthabiti wa kikanda.

“Matukio ya hivi karibuni yanaweka hatari kubwa ya kusambaratika hatua kwa hatua kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,” ameonya Jean-Pierre Lacroix, akirejelea upanuzi wa unyakuaji wa maeneo unaofanywa na kundi hilo lenye silaha, kuanzishwa kwa mamlaka mbadala, na kudhoofika kwa uwepo wa Serikali ya Congo katika maeneo kadhaa ya mashariki.

Jean-Pierre Lacroix, Naibu Katibu Mkuu wa Operesheni za Amani, akitoa maelezo kwa mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali inayoihusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

UN Photo/Eskinder Debebe

Jean-Pierre Lacroix, Naibu Katibu Mkuu wa Operesheni za Amani, akitoa maelezo kwa mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali inayoihusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mamlaka ya DRC mashakani

Mwelekeo huu, amesema, “unatishia moja kwa moja umoja, uhuru na mamlaka kamili ya nchi, na unafufua hofu ya mlipuko wa mzozo wa kikanda wenye madhara yasiyotabirika.”

AFC/M23 imezindua mashambulizi mapya katika jimbo la Kivu Kusini siku za karibuni, ikiteka miji kadhaa, ukiwemo Uvira, ulioanguka Desemba 9 baada ya mapigano makali.

Jiji hili la kimkakati, lililoko mwambao wa Ziwa Tanganyika, lilikuwa limekuwa makao makuu ya mkoa baada ya waasi kuteka Bukavu mwezi Februari, kama sehemu ya mashambulizi ya kasi ya kijeshi yaliyoanza mwanzoni mwa mwaka.

Mikakati ya waasi ya upanuzi

Mikakati ya upanuzi wa eneo la harakati hizo za waasi imeiwezesha kudhibiti miji mingi katika jimbo la Kivu Kusini, pamoja na ile ya jimbo jirani la Kivu Kaskazini, hasa Goma, ambayo zamani ilikuwa makao makuu ya jimbo na sasa inashikiliwa na M23, kundi lenye silaha linalodai kuitetea jamii ya Watutsi wa Congo.

Maendeleo haya ya kimkakati yanabadilisha mistari ya mapigano na kudhoofisha zaidi mamlaka ya Serikali ya Congo katika eneo ambalo tayari limeharibiwa na miongo kadhaa ya mizozo.

Kwa mujibu wa Jean-Pierre Lacroix, kutekwa kwa Uvira kumeambatana na “kuongezeka kwa kiwango kikubwa cha mashambulizi ya kijeshi, ambapo kwa upande mmoja ni wapiganaji wa M23 wanaodaiwa kupata msaada kutoka kwa jeshi la Rwanda, na kwa upande mwingine ni jeshi la Congo likisaidiwa na wanajeshi wa Burundi na makundi ya kujilinda ya Wazalendo yaliyo upande wa serikali ya Kinshasa.”

Mtazamo mpana wa mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali inayoihusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

UN Photo/Eskinder Debebe

Mtazamo mpana wa mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali inayoihusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kutokuwepo kwa utulivu wa kudumu

Kutokuwepo kwa uthabiti wa kudumu kunachochewa na asili ya eneo la Mashariki mwa Congo. Eneo hilo ni miongoni mwa maeneo yenye utajiri mkubwa wa rasilimali za madini nchini, hasa dhahabu na koltani, madini muhimu kwa utengenezaji wa betri na simu za mkononi au za rununu.

Pia limegawanyika kutokana na migogoro ya kijamii iliyojaa kina, urithi wa miongo ya vita na watu kufurushwa makwao.

Katika mazingira haya, Lacroix amesema makundi mengi yenye silaha, ya Congo na ya kigeni, ambayo mara nyingi yanatumiwa na nchi jirani, yanagombania udhibiti wa maeneo, migodi na njia za magendo, na hivyo kuendeleza mzunguko wa vurugu ambao mara nyingi unakwepa juhudi za kisiasa za kuleta suluhu.

Pengo kati ya diplomasia na uhalisia wa hali

Kurejea kwa mapigano kunatokea licha ya hatua kadhaa za kidiplomasia, zikiwemo kutiwa saini kwa makubaliano ya amani mjini Washington Desemba 4 kati ya Rais wa Congo Félix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame. Makubaliano hayo, yaliyosimamiwa na Rais wa Marekani Donald Trump, yalifuata makubaliano ya mfumo yaliyotiwa saini Novemba 15 Doha kati ya DRC na AFC/M23, pamoja na kuanzishwa, mwezi Oktoba, kwa mekanismi ya pamoja ya ufuatiliaji wa usitishaji vita kati ya Kinshasa na waasi.

Hatua hizi zilionekana kuashiria matumaini ya kupungua kwa mivutano.

Lakini “matukio ya hivi karibuni Kivu Kusini yanaonesha wazi pengo kati ya jitihada za kidiplomasia na hali halisi inayowakumba raia,” amesisitiza Lacroix. Kwa mujibu wake, ukiukaji wa mara kwa mara wa usitishaji vita na kurejelewa kwa mapigano kunahatarisha “kuanguka kwa juhudi za kidiplomasia zinazoendelea, kukidhoofisha uaminifu wa michakato ya amani na kuongeza hisia ya kutelekezwa kwa raia.”

Mwanamke na mtoto wakisubiri katika kituo cha matibabu ya kipindupindu katika jimbo la Kivu Kusini, DR Congo.

© UNICEF/Jospin Benekire

Mwanamke na mtoto wakisubiri katika kituo cha matibabu ya kipindupindu katika jimbo la Kivu Kusini, DR Congo.

Kuenea kwa makundi yenye silaha

Wakati huohuo, pamoja na ongezeko la mapigano Kivu Kusini, vurugu bado zimekita mizizi katika majimbo jirani mawili.

Katika eneo la Lubero, Kivu Kaskazini, kundi la Allied Democratic Forces (ADF), waasi wenye asili ya Uganda wanaohusishwa na ISIS, liliwaua angalau raia 132 mwezi Novemba pekee.

Huko Ituri, makundi yenye silaha yanaendelea kufanya operesheni karibu kabisa na kambi za wakimbizi wa ndani, ambako walinda amani wa MONUSCO ndio pekee wanaotoa ulinzi wa moja kwa moja kwa zaidi ya watu 100,000.

Lacroix ameongeza kuwa “Wanawake na watoto ndiyo wanaoathirika zaidi”, akitaja ukatili wa kingono unaohusiana na vita, uhamishaji wa kulazimishwa, mauaji ya kiholela na utekaji.

Katika maeneo yanayodhibitiwa na AFC/M23, vizuizi vinavyowekwa dhidi ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa vinazuia kazi yake ya ufuatiliaji na udhibiti.

Kuzorota kwa hali ya kibinadamu

Kando na mzunguko huu wa ukosefu wa usalama, kuna janga kubwa la kibinadamu, watu milioni 5.3 wamekimbia makazi yao ndani ya nchi na zaidi ya milioni 24 wanakabiliwa na uhaba wa chakula, huku mpango wa misaada ya kibinadamu kwa DRC ukiwa umefadhiliwa kwa asilimia 22 pekee. Kufungwa kwa muda mrefu kwa viwanja vya ndege vya Goma na Kavumu na kupungua kwa upatikanaji wa misaada kunafanya hali kuwa ngumu zaidi.

Licha ya uhaba wa fedha unaoathiri operesheni zote za ulinzi wa amani, MONUSCO inajaribu kudumisha uwepo wa kuzuia mashambulizi.

“Kupunguzwa kwa wafanyakazi kutaathiri uwezo wake wa kutoa hatua za msaada wa haraka na kufikia maeneo mengi,” amekiri Jean-Pierre Lacroix.

Katika kukabiliana na mwelekeo huu hatari, mkuu huyo wa operesheni za ulinzi wa amani anatoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuchukua hatua.

“Katika kipindi hiki hatari, jukumu la Baraza la Usalama ni muhimu zaidi kuliko wakati mwingine wowote,” amesisitiza. Kwani, zaidi ya makubaliano yaliyosainiwa, “mafanikio ya kidiplomasia sasa lazima yageuzwe kuwa maboresho halisi uwanjani, la sivyo vita vitaendelea kubadili ramani ya Congo kwa nguvu na kwa kasi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *