Dodoma. Ni simulizi ya majonzi ya jinsi lori lililofeli breki lilivyowaparamia vijana watano waendesha bodaboda wakiwa kijiweni eneo la Dodoma Makulu, mkoani hapa.
Ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia leo Desemba 12, 2025 wakati lori hilo aina ya FAW likitokea barabara ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) lilipofeli breki na kuparamia kijiwe cha bodaboda cha Amani, kilichopo kando mwa barabara hiyo.
Tayari miili miwili kati ya mitano ya madereva hao waliokufa papo hapo imetambuliwa.
Miongoni mwa miili iliyotambuliwa ni wa Ijumaa Ndafu (27), ambao umezikwa leo katika Kata ya Dodoma Makulu.
Mwili mwingine ambao umetambuliwa kwa jina moja la Ishadi, umesafirishwa kwenda mkoani Arusha.
Picha ya marehemu Ijumaa Ndafu (27) enzi za uhai wake.
William Mathias, baba mdogo wa Ndafu, amesema ajali ilipotokea hawakujua kama mtoto wao ni miongoni wa waliokuwapo, kwani takribani dakika 10 kabla ya ajali, alikuwa maeneo ya nyumbani akifanya shughuli zake.
”Tuliposikia kuna ajali imetokea hatukuhisi kama Ijumaa angekuwepo kule, kwani nilikuwa naye dakika 10 zilizopita tukirekebisha fremu za duka langu, alinisaidia ngazi ya kurahisisha kazi yangu,” amesema.
Mathias amesema aliposikia barabarani kuna ajali hakwenda kwa sababu ni mwoga na alijua ni watu wengine tu ndio waliopata ajali hiyo, hakujua kuwa hata kijana wake ni miongoni mwa waliofariki.
”Mimi ni mwoga wa kuangalia ajali, hivyo niliwaacha wengine waende nikabaki nyumbani. Nashanga kuja kuambiwa Ijumaa amefariki kwenye ile ajali,” amesema akieleza kijana wao ameacha mke na mtoto mmoja.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mtaa wa Msangalalee Magharibi, Lenard Ndama, amesema tukio hilo limeacha majonzi mtaani kwake kwani limetokea kipindi ambacho hakikutarajiwa, akieleza vijana hawakuwa barabarani bali walikuwa wametulia nje kabisa ya barabara.
Amesema kijiwe cha vijana hao kiko umbali wa takribani mita 20 kutoka barabarani, lakini walifuatwa waliko na kugongwa na lori.
”Mpaka sasa tuna misiba miwili ya watu waliotambulika, mmoja anazikwa leo na mwingine anasafirishwa kwenda Arusha. Wengine watatu bado hawajatambuliwa,” amesema.
Renatha Mzanje, Ofisa Mawasiliano na Uhusiano wa Umma wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma, amesema walipokea miili ya watu watano na mpaka mchana wa Desemba 12, miwili imetambulika na kuchukuliwa na ndugu zao, huku mingine mitatu ikiwa bado haijatambuliwa.
”Kuna mmoja yupo wodini alijeruhiwa anaendelea vizuri na matibabu,” amesema.
Ajali ilivyotokea
Akizungumzia ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera amesema tukio hilo lilitokea Desemba 11, 2025 saa 2:30 usiku.
Amesema mbali ya watu watano waliofariki dunia, utingo wa lori lililosababisha ajali amejruhiwa, huku dereva akitoroka na anaendelea kutafutwa.
Kamanda Hyera amesema athari nyingine iliyotokana na ajali hiyo ni uharibifu wa pikipiki na uzio wa nyumba iliyo jirani na barabara ambao uligongwa na lori hilo.
“Eneo hilo la barabara lina mteremko mkali, hivyo madereva ni lazima waendeshe mwendo wa tahadhari ili inapotokea changamoto yoyote waweze kuepusha maafa yanayoweza kuzuilika, tofauti na wanavyokuwa kwenye mwendo mkali,” amesema.
Hyera amesema kutokana na eneo hilo kuwa la hatari kwa waendesha vyombo vya moto na watembea kwa miguu, Jeshi la Polisi litaimarisha usalama, wakati mamlaka nyingine ikiwamo Tanroads zikifanya jitihada za kuepusha ajali.
James Tusiime, aliyeshuhudia ajali hiyo amesema alisikia kishindo kikubwa ambacho hakikuwa cha kawaida kutokea maeneo ya barabarani, kilichoashiria kuna tatizo.
Alipofika kujua kinachoendelea amesema alikuta ajali hiyo.
“Wote waliofariki walikuwa ni vijana wetu ambao huwa wanatuwahisha tunapokwenda, leo ajali imekatisha uhai wao, kwa kweli tunasikitika,” amesema.
Shuhuda mwingine, Happiness Richard, amesema lori hilo lilikuwa linapiga honi mfululizo barabarani kuashiria kuna tatizo lakini lilipofika kwenye kona lilishindwa kukata, hivyo liliacha njia na kwenda kuwagonga madereva wa bodaboda ambao walikuwa wakisubiri abiria kwenye kijiwe chao.
Akizungumza akiwa eneo la tukio, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabir Shekimweri, amesema watazungumza na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ili waweke matuta katika eneo hilo kuwawezesha madereva kupunguza mwendo kutokana na uwepo wa ajali za mara kwa mara.
Waombolezaji wakiwa wamekusanyika kwenye msiba wa Ijumaa Ndafu kwenye Kata ya Dodoma Makulu Jijini Dodoma leo Desemba 12, 2025.
“Inaonekana gari hili lilipata hitilafu kwa hiyo dereva alishindwa kulimudu ndiyo maana liliacha njia na kwenda kuwaparamia vijana wetu na kusababisha maafa. Inabidi tuweke matuta katika eneo hili ili kudhibiti mwendo kwa wanaopandisha na wale wanaoshuka kwa ajili ya usalama wetu,” amesema.
Shekimweri amesema madereva hao walikuwa wamepaki pikipiki nje ya barabara lakini kutokana na lori hilo kufeli breki liliwafuata na kusababisha maafa yaliyotokea.
Ajali hiyo ni ya tatu kutokea katika eneo hilo ambazo zimegharimu maisha ya watu, wakiwamo madereva na watembea kwa miguu.