WAKALA wa maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Nyang’hwale mkoa wa Geita imefanikiwa kufikisha huduma ya maji safi katika vijiji 48 ambayo ni sawa na asilimia 77.4 ya vijiji vyote 62 vya wilaya hiyo.

Kwa mjibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 Wilaya ya Nyang’hwale ina wakazi wapatao 225,803 katika Vijiji 62 huku kati yao 174,772 kwenye vijiji 48 ndio wamefikiwa na huduma ya Maji safi na salama.

SOMA: Ruwasa wajipanga kupunguza adha ya maji Geita

Meneja wa RUWASA wilayani Nyang’hwale, Suzana Mabula amewasilisha taarifa hiyo katika kikao cha nusu ya mwaka wa fedha 2025/26 cha wadau wa maji na vyombo vya watoa huduma ngazi ya jamii wilayani humo.

Suzana amesema mbali na hatua hiyo jitihada zinaendelea ili kupanua uwigo wa upatikanaji wa huduma hiyo muhimu ambapo kwa mwaka wa fedha 2025/2026 wametenga Sh Bilioni 1.8 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji.

Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Grace Kingalame.

“Kwa sasa tuna miradi mitatu ambayo tunaendelea na utekelezaji wake, mradi wa kwanza ni wa visima vya jimbo, ambao unatekelezwa katika vijiji vitano hadi sasa shilingi milioni 137 zimekwishalipwa kwa ajili ya mradi huo.

“Mradi mwingine ni wa Iseni-Nyangalamila ambao unatekelezwa kwenye vijiji sita na hadi sasa serikali imekwishalipa zaidi ya milioni 300”, amesema Suzana.

Ametaja mradi mwingine ni wa Nyijundu unaohusisha ujenzi wa tenki la maji, vituo 18 vya kuchotea maji pamoja na mtandao wa mabomba ya maji wenye urefu wa kilomita 15 na tayari mkandarasi ameshalipwa sh milioni 536.

Wadau wa huduma ya maji wilayani Nyang’hwale.

Mwenyekiti wa CCM wilayani Nyang’hwale Adam Mtore ameshauri RUWASA kuhakikisha inapunguza upotevu wa maji na malalamiko ya bili kwa kufunga mita za wateja majumbani na siyo mbali na makazi yao.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, John Izack amezitaka taasisi za serikali zilizokatiwa huduma ya maji kutokana na madeni kuhakikisha zinalipa kwa wakati ili kurejeshewa huduma na Ruwasa iweze kujiendesha kwa tija.

Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Grace Kingalame ametoa onyo kali kwa watumishi wa Idara ya maji wanaojihusisha na udanganyifu kuacha mara moja kwani serikali haitawavumilia hivvo wazingatie nidhamu ya kazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *