Akizungumza mjini Baghdad katika hafla maalum ya kufunga mpango huo miaka 22 baada ya kuanzishwa mwaka 2003, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema kufungwa kwa ujumbe huo “kunafunga sura moja na kufungua nyingine,” akisisitiza kwamba maendeleo ya Iraq ndiyo habari kuu ya siku hiyo.
Ujasiri wa watu wa Iraq
Guterres amesifu mabadiliko makubwa ya Iraq tangu 2003, akisema uimara wa nchi hiyo “ni chanzo cha msukumo mkubwa.”
Aliwaambia viongozi waliohudhuria hafla hiyo kwamba “Mmevuka miongo ya vurugu, ukandamizaji, vita, ugaidi, misuguano ya kimadhehebu na kuingiliwa kwa kigeni. Kinyume na matarajio, watu wa Iraq hamkuwahi kuyumba katika dhamira yenu ya kujenga jamii ya amani na jumuishi, inayotegemea sheria na taasisi madhubuti.”
Ameongeza kuwa Iraq ya leo “haitambuliki na ni ya kushangaza ikilinganishwa na miaka yake ya mwanzo yenye machafuko.”
Urithi wa UNAMI
Katibu Mkuu amebainisha mchango wa UNAMI katika kuimarisha utawala, haki za binadamu na mazungumzo ya kisiasa.
“UNAMI iliheshimiwa kutembea bega kwa bega na watu wa Iraq,” amesema, akitaja msaada kwa mageuzi ya kimahakama, nafasi ya kiraia kwa wanawake na wachache, na juhudi za maridhiano ya kitaifa.
Pia amekumbusha jinsi ujumbe huo ulivyoongoza uratibu wakati wa mapambano dhidi ya Da’esh, akisema ulitoa mchango muhimu katika kuwalinda raia na kuwezesha kurejea kwa mamilioni ya watu waliokimbia makazi yao.
Kuheshimu ujasiri na kujitolea
Guterres amewakumbuka watumishi wa Umoja wa Mataifa waliohudumu nchini Iraq, wakiwemo waliouawa katika shambulio la 2003 katika Hoteli ya Canal. “Tunaiheshimu kumbukumbu na urithi wao wote wakiwemo Sérgio Vieira de Mello,” amesema, akibainisha kuwa tarehe 19 Agosti sasa ni Siku ya Kimataifa ya Wahudumu wa Kibinadamu.
Ametoa shukrani maalum kwa wafanyakazi wa kitaifa wa Iraq, akiwaelezea kama “Wairaqi ambao wamefanya kazi mwaka baada ya mwaka kujenga upya na kuimarisha nchi yao.”
Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres akiwa kwenye Makao Makuu ya UNAMI Baghdad Iraq (Kutoka Maktaba)
Ushirikiano wa UN kuendelea
Ingawa UNAMI inamaliza jukumu lake, Guterres amesisitiza kuwa ushirikiano wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq utaendelea.
Alisema Umoja wa Mataifa utaendelea kusaidia mageuzi ya taasisi, kuboresha utawala na utoaji huduma, pamoja na kuimarisha uchumi kupitia mashirika na programu mbalimbali.
Amesema “Ingawa ujumbe unaweza kuhitimishwa, Umoja wa Mataifa utaendelea kutembea na watu wa Iraq kuelekea amani, maendeleo endelevu na haki za binadamu.”
Kuanza kwa ukurasa mpya
Guterres amekaribisha uamuzi wa serikali wa kuupa barabara moja jijini Baghdad jina la “Barabara ya UN,” akisema ni “ishara yenye nguvu ya ushirikiano wetu wa kudumu.”
Akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa Iraq Mohammed Shia’ al-Sudani, amehitimisha kwa ahadi, “Mnaweza kuwa na uhakika kwamba Umoja wa Mataifa utakuwa nanyi katika kila hatua ya safari.”
TAGS: Masuala ya UM, Iraq, UNAMI, kufungwa kwa opereshen, Baghdad