Ameonya kuwa dunia imejikita sana katika masuala ya usalama kiasi cha kusahau umuhimu wa kufikia amani.
Kabla ya kufanyika kwa Jukwaa la 11 la Kimataifa la Muungano huo wa Ustaarabu mjini Riyadh, Saudi Arabia, kuanzia kesho tarehe 14–15 Desemba, UN News imezungumza na Moratinos ambapo amewahimiza vijana kote duniani kuifanya amani kuwa kipaumbele cha juu.
Amesema mustakabali wa dunia unategemea kizazi kipya kilicho tayari kuchagua mazungumzo badala ya migawanyiko, na ubinadamu badala ya chuki.
Katika maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Muungano wa Ustaarabu, Moratinos amezungumza kuhusu jinsi dunia ilivyobadilika katika miongo miwili iliyopita.
Kuanzak wa UNAOC
Muungano huo ulipoanzishwa mwaka 2005 kwa mpango wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, wakati huo Kofi Annan, mpangilio wa kimataifa ulikuwa wa upande mmoja.
Leo hii, dunia ni ya pande nyingi huku nguvu mpya zikijitokeza katika ulimwengu wa Kiarabu, Asia, Afrika na Amerika ya Kusini, zikidai sauti zao zisikike na nafasi zao zitambuliwe.
Moratinos amesisitiza kuwa Muungano huo uko katika nafasi ya kipekee ya kuwakutanisha wadau wote mezani.
Amesema dunia imekuwa tata zaidi, jambo ambalo ni changamoto inayohitaji dhamira ya kina zaidi ya kusikiliza, kufanya mazungumzo na kuelewana.
Miguel Ángel Moratinos mkuu wa UNAOC
Akili mnemba: Fursa na changamoto
Miongoni mwa masuala muhimu yanayotarajiwa kuangaziwa katika jukwaa hilo ni akili unde au akili mnemba, ambayo Mwakilishi wa UNAOC amesema inatoa fursa na itaunda mustakabali kwa namna kubwa, lakini pia akatahadharisha kuhusu changamoto zake.
“Teknolojia haijihusishi na dini, imani au maadili, mambo haya yote ni muhimu kwa binadamu,” amesema. Amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa akili unde inabaki kumlenga binadamu, na kuongozwa na maadili na maamuzi ya kibinadamu.
Ameonya kuhusu hatari ya watu kuachia uhuru na majukumu yao kwa mashine. “Ikiwa ubinadamu utasahau dira yake ya maadili, teknolojia haitarekebisha mwelekeo,” amesema.
Ameongeza kuwa Muungano wa Ustaarabu upo mahsusi kulinda maadili na misingi hiyo ya kimaadili.
Onyo kuhusu kurejea kwa chuki
Akizungumzia moja ya masuala muhimu zaidi yanayohusu Muungano huo, Moratinos amezungumzia kauli za chuki, hususan mitandaoni.
“Chuki imerudi,” amesema. “Inamfanya mtu amtenge mwingine. Chuki huanza kwa maneno, lakini husababisha kutengwa, vurugu na migogoro.” Ili kukabiliana nayo, amesema Muungano unawekeza katika programu zinazohamasisha simulizi mbadala na kukuza uelewano. Amesisitiza kuwa vijana ni nguzo muhimu katika juhudi hizi.
Amesema vijana wa leo wanaishi sehemu kubwa ya maisha yao katika “nafasi za mtandaoni”, na akaonya kuwa hali hiyo inaweza kuwanyima mawasiliano halisi ya kibinadamu.
“Tunahitaji kuwarejeshea vijana uhalisia,” amesema, akitoa wito wa kuwepo uwiano bora kati ya ulimwengu wa kidijitali na maisha halisi ambako mahusiano, tamaduni na jamii hujengwa kwa kweli.
Mitandao ya kijamii inaweza kuwezesha unyanyasaji mtandaoni.
Amani lazima iwe kipaumbele
Moratinos amesema dunia imezama katika mtazamo wa kupindukia wa usalama, na katika mchakato huo imesahau thamani ya amani. “Kila mtu anavutiwa zaidi na usalama kuliko amani. Lakini usalama hauwezi kupatikana bila amani.”
Amerejelea gharama kubwa ya kibinadamu inayosababishwa na migogoro na vita huko Gaza, Ukraine na Sudan, na kusisitiza haja ya dunia kujikita upya katika lililo muhimu zaidi, kuokoa ubinadamu.
Amani lazima iwe ujumbe mkuu wa Jukwaa la Riyadh na kanuni inayowaongoza vizazi vijavyo.
Amesisitiza kuwa ni vijana pekee ndio walio na uwezo wa kutimiza dira hii. Ni wao, amesema, wanaoweza kuamua kwamba karne ya 21 iwe karne ya mwisho ya vita.