Katika siku mbili zijazo, washiriki waliokusanyika katika mji mkuu wa Saudi Arabia wanatarajiwa kusisitiza kuwa ushirikiano baina ya tamaduni, dini na jamii mbalimbali unaendelea kuwa njia pekee inayowezekana ya kukabiliana na enzi inayokabiliwa na kuongezeka kwa migawanyiko na migogoro.
Akizungumza katika kikao cha ufunguzi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amepinga wazo kwamba dhamira ya Muungano huo si ya kweli au, kama wakosoaji wengine wanavyodai, “ni laini mno kwa dunia yetu ngumu.”
Amewaonya wanaodharau mazungumzo kama jambo la kijinga kuwa wamekosea. Diplomasia na ushirikiano, alisema, si hiari ni muhimu sana.
Miaka ishirini imepita tangu aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, alipoanzisha mpango huo mwaka 2005 kwa msaada wa Hispania na Uturuki.
Dunia imebadilika
Tangu wakati huo, mazingira ya kijiografia na kisiasa duniani yamebadilika kwa kiasi kikubwa, lakini lengo kuu la Muungano limebaki lilelile, kukabiliana na misimamo mikali na kutovumiliana, na kusaidia jamii za tamaduni na imani tofauti kuishi pamoja kwa heshima.
Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa ameeleza kitendawili cha zama ambazo ubinadamu “umeunganishwa zaidi, lakini haujawahi kugawanyika zaidi,” na akabainisha mistakabali miwili inayokinzana, mmoja unaoongozwa na hofu, kuta na vita vinavyozidi na mwingine unaojengwa juu ya madaraja ya uelewano kati ya tamaduni.
Amesisitiza kuwa ni njia ya pili pekee inayoweza kuleta amani ya kudumu: “Hakuna tena tarehe 7 Oktoba. Hakuna tena Gaza zinazoharibiwa. Hakuna tena El-Fasher zinazoachwa na njaa. Hakuna tena jamii zinazouawa, kufukuzwa au kufanywa mbuzi wa kafara.”
Katibu Mkuu ametaja nguvu tatu zenye uwezo wa kuleta mabadiliko chanya duniani ambazo ni vijana, wanawake na wasichana, pamoja na watu wa imani. Amewahimiza wajumbe kuendeleza dhamira ya Muungano “kwa ujasiri, uwazi na matumaini.”
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiwa jukwaani kwenye mkutano wa UNAOC Riyadhi Saudia
Tamko la Riyadh: Wito wa kuishi pamoja
Nchi zilizoshiriki katika Jukwaa hilo zimeidhinisha Tamko la Riyadh, linalotoa wito wa kupambana na aina zote za kutovumiliana kwa misingi ya dini kama kipaumbele cha kimataifa.
Hati hiyo inasisitiza nafasi muhimu ya elimu katika kukuza mazungumzo, haki za binadamu na jamii zenye amani, na kuthibitisha tena lengo la msingi la Muungano: kuimarisha ushirikiano kati ya tamaduni na dini huku ukihamasisha heshima, uelewano wa pamoja na ujumuishaji.
Sauti sawa, wajibu wa pamoja
Mwakilishi Mkuu wa UNAOC Miguel Moratinos, ambaye pia ni Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na chuki dhidi ya Uislam, amefungua kikao hicho kwa kusisitiza kuwa kila utamaduni lazima uwe na sauti sawa katika kuunda mustakabali wa dunia.
Amesema Hakuna mtazamo mmoja unaopaswa kutawala, badala yake, jamii ya kimataifa yenye amani na ujumuishaji wa kweli lazima ichote hekima na maadili ya ustaarabu wote.
Bwana. Moratinos ameonya kuhusu “kurejea kwa chuki,” na kutoa wito wa kuwa macho dhidi ya kuongezeka kwa ubaguzi.
Akinukuu Aya kutoka Suratul Hujurat katika Qur’ani Tukufu, amesisitiza kuwa utofauti wa binadamu ni chanzo cha nguvu, si mgawanyiko.
Amebainisha kuwa Uislamu ni dini ya amani na akasisitiza tena kuwa chuki dhidi ya Uislam haina nafasi popote. Wakati huo huo, amesisitiza kuwa chuki dhidi ya Wayahudi lazima ikomeshwe, akiongeza “Ukosoaji halali wa serikali haupaswi kuchukuliwa kuwa chuki dhidi ya Wayahudi wala kutumiwa kama kisingizio cha kuwatuhumu au kuchafua jamii nzima.”
Saudi Arabia: Zingatia mazungumzo, usijiondoe
Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Faisal bin Farhan Al Saud, amethibitisha tena “dhamira ya muda mrefu ya Ufalme huo katika mazungumzo ya kitamaduni.”
Amesema uungaji mkono wa Saudi kwa Muungano unatokana na imani thabiti kwamba ushirikiano kati ya tamaduni na ustaarabu ni msingi wa amani, ushirikiano na kuzuia migogoro.
Ameangazia mipango kadhaa ya Saudi inayolenga kukuza mazungumzo na kukabiliana na misimamo mikali, na akaonya kuhusu kuenea kwa harakati za misimamo mikali zinazoendeshwa kwa misingi ya dini au utaifa, pamoja na ongezeko la kutia wasiwasi la kauli za chuki na chki dhidi ya Uislam katika miongo miwili iliyopita.
Badala ya kusababisha kujiondoa, amesema changamoto hizi zinapaswa kuisukuma dunia kuimarisha si kuacha maadili ya mazungumzo, mawasiliano na kuishi pamoja.
Wawakilishi kutoka Hispania na Uturuki, ambao ni wafadhili waanzilishi wa Muungano huo, pia wamezungumza, wakithibitisha tena umuhimu wa kudumu wa ujumuishaji, heshima ya pande zote na mazungumzo endelevu.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiwa jukwaani kwenye mkutano wa UNAOC Riyadhi Saudia
Deepfakes, kauli za chuki na juhudi za udhibiti
Siku ya ufunguzi wa jukwaa hilo pia imeelekeza kipaumbele chake kwa moja ya changamoto zinazokua kwa kasi zaidi zinazounda mazingira ya taarifa leo, habari potofu zinazotokana na akili mnemba AI.
Washiriki wa jukwaa wamesema kuwa taarifa zilizobadilishwa au deepfakes, kauli za chuki zinazoongezwa na algoriti, na mifumo isiyo na udhibiti tayari vinabadilisha mjadala wa umma na si kwa njia nzuri.
Ismail Serageldin, mwenyekiti mwenza wa Kituo cha Kimataifa cha Nizami Ganjavi na aliyekuwa Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, amesema matumizi ya akili mnemba sasa hayazuiliki.
Ameahimiza umma kutoogopa teknolojia mpya, akilinganisha wakati huu na uvumbuzi wa kalkuleta, wakati wengi walitabiri kwamba ajira za uhasibu zingekoma.
“Badala yake,” amebainisha, “walibadilika na akahoji jamii itaweza kufanya vivyo hivyo leo”.
AI inaweza kuwa msaada wa kuleta haki
Kwa kuzingatia tahadhari sahihi, ameongeza kuwa, AI inaweza hata kusaidia watu kupata usawa bora kati ya kazi na maisha binafsi.
Bwana. Serageldin pia amesisitiza kuwa AI haitachukua nafasi ya binadamu, lakini watu wanaojua jinsi ya kuitumia watapata faida kubwa. Udhibiti makini lazima ulinde umma bila kuzuia ubunifu au uundaji.
Achraf Tasfaout, mtaalamu wa data anayefanya kazi katika sekta ya benki, ameonya kuwa AI inakuza kasi ya kuenea kwa kauli za chuki na kufanya iwe ngumu kwa watu kutofautisha kati ya yaliyo halisi na yaliyobadilishwa au deepfakes.
Sheria lazima ziwe bayana
Ametoa wito wa kuweka sheria wazi zinazoweka mipaka ya matumizi salama huku zikiruhusu mawazo mapya kuendeleza.
Amesema kuwa watunga sera na wanahabari wana jukumu muhimu katika kulinda jamii. Aidha, vijana, kama watumiaji wa AI walio hai zaidi, watakuwa muhimu katika kuunda suluhisho. Ameongeza kuwa AI yenyewe inaweza kutumika kukabiliana na changamoto nyingi inazosababisha.
Atif Rashid, Mhariri Mkuu wa Analyst News, ameonya kuwa mifumo ya AI inatolewa “kwa haraka sana,” mara nyingi bila hatua muhimu za usalama. Alisema inaweza kuonekana kana kwamba “binadamu ni panya wa majaribio” katika jaribio la kimataifa, huku udhibiti ukifika tu baada ya kuenea kwa upana kwa umma.
Bwana. Rashid amebainisha mifano ambapo AI imesababisha tabia hatarishi, aliyoielezea kama ‘AI psychosis,’ na akasisitiza kuwa mifumo mipya lazima iundwe kwa ajili ya ustawi wa binadamu wote, ikitegemea thamani za kibinadamu.