
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, katika ujumbe wake aliotuma kwa njia ya video kwa sababu yuko katika ziara nyingine nchini Oman amesema, “rushwa si kosa lisilo na waathirika. Inachochea migogoro, inaendeleza ukosefu wa usawa, na inanyonya rasilimali zinazohitajika kulinda watu na sayari. Kila dola inayopotea kutokana na uhalifu wa kiuchumi ni dola iliyoibwa kutoka kwa wale wanaotafuta mustakabali bora.”
Ameongeza kwamba, “teknolojia zinazoibukia kama akili unde au Akili Mnemba zina uwezo wa kuongeza kasi ya rushwa, lakini pia zinaweza kutusaidia kuigundua na kuizuia. Hata hivyo, hili linahitaji kanuni na uwajibikaji.”
Naye Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Annalena Baerbock, katika ujumbe wake wa video katika ufunguzi wa kikao hicho ambacho ni cha kumi na moja cha Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Rushwa, COSP10 amesema, “kuzuia na hatimaye kutokomeza rushwa ni wajibu wa pamoja. Tunawajibika kwa watu tunaowahudumia.”
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), John Brandolino, yeye amesema, “rushwa hutoa miundombinu haramu inayoruhusu makundi ya kihalifu kufanya kazi na kujipatia faida bila kuadhibiwa kote duniani. Kuna haja ya mbinu jumuishi na iliyoratibiwa, ambapo taasisi zinafanya kazi kwa pamoja katika sekta na mipaka mbalimbali, kwa kushirikiana na wadau wote husika, ili kuvunja mitandao ya uhalifu na ushirikiano haramu kwa wakati mmoja.”
Mkutano huo wa wiki nzima unafanyika chini ya kaulimbiu “Kuchagiza Uadilifu wa Kesho”, na unawaleta pamoja zaidi ya washiriki 2,500 kutoka Nchi Wanachama 170 wa Mkataba.
Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al Thani, amehudhuria ufunguzi wa mkutano huo. Waliohutubia katika ufunguzi huo ni pamoja na Rais anayemaliza muda wake wa kikao cha kumi, Christine Cline kutoka Marekani, Rais mpya wa kikao cha kumi na moja, Hamad bin Nasser Al-Misnad kutoka Qatar, pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa UNODC, John Brandolino.
Maazimio yanayozingatiwa na Nchi Wanachama wa Mkataba yanajikita katika kushughulikia jukumu la akili unde katika kuzuia na kupambana na rushwa, kuimarisha uadilifu wa watoto na vijana, kuongeza uwazi katika ufadhili wa vyama vya siasa na kampeni za uchaguzi, pamoja na kuchunguza nafasi ya rushwa katika kuwezesha uhalifu mwingine, kama vile usafirishaji haramu wa wahamiaji na uhalifu unaoathiri mazingira, miongoni mwa mengine.
Kuhusu Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Rushwa na Mkutano wa Nchi Wanachama
Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Rushwa ni chombo pekee cha kimataifa chenye nguvu ya kisheria kinachopambana na kosa hili. Ulianza kutumika Desemba 2005 na karibu ni wa ulimwengu mzima, ukiwa na Nchi Wanachama 192. Chini ya Mkataba huo, Nchi Wanachama zinawajibika kisheria kuzuia na kuhalalisha adhabu dhidi ya rushwa; kukuza ushirikiano wa kimataifa; kurejesha na kurudisha mali zilizoibwa; na kuboresha misaada ya kiufundi na ubadilishanaji wa taarifa katika sekta binafsi na ya umma.
Kupitia Mfumo wa Mapitio ya Utekelezaji wa Mkataba (IRM), Nchi Wanachama zimekubaliana kushiriki katika mchakato unaotathmini jinsi zinavyotekeleza wajibu wao chini ya Mkataba. Tangu 2010, IRM imesaidia nchi 146 kusasisha au kuanzisha sheria na sera mpya za kupambana na rushwa.
UNODC inawezesha nchi kubadilisha ahadi za kimataifa za kupambana na rushwa kuwa mageuzi halisi yanayolinda rasilimali za umma huku yakikuza uwazi, uadilifu na ustawi. Kupitia uwepo wake katika uwanja wa utekelezaji, UNODC inaunga mkono nchi katika kujenga taasisi zenye uwajibikaji na kupunguza fursa za rushwa kushika mizizi.
Mkutano wa Nchi Wanachama (COSP) ndio chombo kikuu cha kufanya maamuzi cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Rushwa. Hukutana kila baada ya miaka miwili na kusaidia Nchi Wanachama kutekeleza Mkataba na kupitisha maamuzi ya sera yanayoelekeza juhudi za kimataifa za kupambana na rushwa.