
Mamia ya wakazi, wanaharakati wa haki za binadamu na wawakilishi wa mashirika ya kijamii walifanya matembezi ya amani katika mji wa pwani wa Mombasa, wakitoa wito wa kusitishwa mara moja kwa vita vinavyoendelea katika mataifa kadhaa ya Afrika, yakiwemo Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Matembezi hayo, ambayo waandaaji walisema ni ya kwanza ya aina yake jijini humo, yalilenga kuangazia kile walichokitaja kuwa ukimya wa jumuiya ya kimataifa huku vifo vya raia na maafa ya kibinadamu vikiendelea kuongezeka katika maeneo yenye migogoro.
Waandamanaji waliobeba mabango na kuimba kaulimbiu za amani walisema sauti ya Afrika lazima isikike kwa nguvu zaidi katika juhudi za kumaliza vita vinavyochochewa na mapambano ya kudhibiti rasilimali za asili.
“Kile kinachotokea leo Congo au Sudan kinaweza kutokea kwetu kesho, kwa sababu sisi pia tuna rasilimali,” alisema Mwaivu Kaluka, mwanaharakati wa Chama cha Kikomunisti Kenya. “Hivi sio vita vya kikabila tu, bali ni migogoro inayochochewa na watu wenye nguvu wanaopigania rasilimali za Afrika,” aliongeza.
Kaluka alisema mataifa kama Congo na Sudan yana utajiri mkubwa wa rasilimali, lakini wananchi wa kawaida hawafaidiki, akiongeza kuwa uingiliaji wa kigeni umechangia kuendeleza migogoro hiyo.
“Rasilimali za Afrika lazima ziwanufaishe Waafrika,” alisema.
Wito kwa hatua za Kiafrika na kimataifa
Washiriki waliitaka Umoja wa Afrika, jumuiya za kikanda na serikali zenye ushawishi kuongeza juhudi za kidiplomasia na kibinadamu ili kuzuia kupotea kwa maisha zaidi na kuyumba kwa usalama wa kikanda.
Rafik Rauf, muandaaji wa matembezi hayo kutoka shirika la kibinadamu la Marafiki Relief Aid Africa, alisema lengo lilikuwa kuhamasisha uungwaji mkono wa umma na taasisi.