Akilihutubia Bunge la Ulaya mjini Strasbourg, Von der Leyen amesema suala la usalama sio mbadala bali ni la lazima. Ameongeza kuwa Ulaya haiwezi ikawaruhusu watu walio nje ya bara hilo kuweka masharti ya namna bara hilo litakavyoangaliwa.

Rais huyo wa Halmshauri Kuu ya Ulaya amesema licha ya Marekani kuwa sahihi kwamba pato la mataifa ya Ulaya linashuka, amesisitiza kuwa hali pia nchini Marekani iko vivyo hivyo.

Kando na hayo amesema bara hilo lazima lichukue hatua ya namna ya kuifadhili Ukraine na kutoa kipaumbele kwa amani ya taifa hilo katika mkutano utakaofanyika wiki hii.

“Tutaendelea kufanya kazi kwa karibu na Rais Zelensky na Rais Trump kufikia kile sote tunachokitaka, amani ya kudumu ambayo inalinda uhuru wa Ukraine na kuimarisha usalama wake. Mbinu yetu iko wazi kabisa na tunafanya kazi kwa nguvu zetu zote ili kusitisha umwagaji damu. Hatua ya kwanza ni usitishaji mapigano na njia ya kufika huko inajulikana. Urusi lazima ishinikizwe kuja katika meza ya mazungumzo sio kwa kujionesha tu, bali kwa vitendo na matokeo.”

Viongozi wa Ulaya wapo katika shinikizo la kutumia mali ya Urusi iliyozuiliwa kuifadhili Ukraine na kuishinikiza nchi hiyo kuingia katika meza ya mazungumzo na kumaliza vita vyake Ukraine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *