
Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa, Kiswahili kinaendelea kupata umaarufu duniani na kutambulika kuwa ndiyo lugha itakayoleta mshikamano wa Bara la Afrika.
Hayo yameelezwa leo Jumatano, Desemba 17, 2025 na Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Kampuni ya Alaf Limited, Hawa Bayumi wakati akitangaza ufadhili wa masomo kwa wanafunzi watatu wanaofanya Programu ya Shahada ya Uzamili ya Lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki).
Akizungumza wakati akikabidhi hundi kwa wanufaika hao watatu, Bayumi amesema hatua hiyo ni muendelezo wa juhudi za kampuni hiyo kukuza Kiswahili katika ukanda wa Afrika Mashariki, Afrika na duniani kote.
“Kiswahili ni moja ya tunu kubwa tuliyorithi kutoka kwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ni lugha inayozidi kuenea na kupata umaarufu duniani na hatimaye kutambulika kuwa ndiyo lugha itakayoleta mshikamano wa bara la Afrika.
“Hivyo, tumeona hatuna budi kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuikuza lugha hii adhimu,” amesema Bayumi.
Pia, amesema Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimekuwa na jukumu kubwa na muhimu katika kuandaa na kutekeleza Tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi ya Afrika, ambazo Alaf inadhamini pamoja na kampuni yake dada ya nchini Kenya na Uganda inayowaunganisha waandishi kutoka ukanda wa Afrika Mashariki.
“Sisi kama moja wapo wa kampuni zilizopata mafanikio makubwa na kutambua umuhimu wa Lugha ya Kiswahili kama zana muhimu ya maendeleo ya kitamaduni, kijamii na kiuchumi, tumeona umuhimu wa kukuza Fasihi ya Kiswahili na ndiyo maana tutaendelea kuunga mkono juhudi zote zinazolenga kuikuza lugha hii,”amesema.
Pia, amewataja wanufaika wa ufadhili huo wa Alaf wa Sh11, 700,000 kuwa ni Frank John Kaswahili, Yasenta Emanuel Dagati, na Veromina Boazi Kerato.
Ameitoa wito kwa wanufaika kutumia ufadhili walioupata vyema kwa kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye masomo yao ili wawe na mchango mkubwa katika kuikuza lugha adhimu ya Kiswahili kupitia elimu watakayoipata.
Uongozi wa UDSM umeishukuru Alaf kwa ufadhili huo, ukisema ni sehemu ya maombi mengi yaliyofanywa na wanafunzi wengi.
“Kwa kawaida huwa kuna maombi mengi kutoka kwa wanafunzi kuhusiana na ufadhili huu, lakini ni wanafunzi watatu pekee ndio wanaonufaika; kwa hili tunawashukuru sana ila tunaomba mfikirie jinsi ya kuongeza idadi ya wanufaika ili Lugha ya Kiswahili iweze kukua zaidi”, amesema Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (Taaluma) Profesa Baraka Maiseli.