Dar es Salaam. Nikiwa msanii wa muziki nchini Tanzania kwa zaidi ya miaka 50, nimejionea matukio mengi muhimu katika historia ya Tanzania ambayo yamebadilisha kabisa mwelekeo wa muziki wa rhumba.

Historia ya muziki huu wa mijini, ambao sasa unaitwa muziki wa dansi ilianza zama za Wajerumani. Wajerumani waliingia nchini kwanza kama ‘wafanyabiashara’ chini ya kampuni waliyoiita Germany East africa Company. 

Muda si mrefu baada ya hapo, baada ya kuwatapeli machifu kadhaa, walianzisha serikali ya kwanza katika nusu ya pili ya karne ya 19, na kuliita koloni lao jipya Germany East Africa, na ili kulinda serikali hiyo mpya, jeshi lilianzishwa. 

Hapo ndipo Wajerumani walipoleta ala za kwanza za muziki kutoka nje ya nchi. Ala hizo zilikuwa za kutumiwa na bendi zao za kijeshi. Ala kama saksofoni, tarumbeta, na ngoma ambazo zilitengenezwa katika nchi yao. 

Muziki wa bendi za kijeshi siku hizo huitwa kwa jina la brass band, ndio uliochochea kuanzishwa kwa muziki wa kwanza wa mijini.

Nchi yetu imekuwa na makabila mengi tangu zamani, na kila kabila lilikuwa na ‘ngoma’ zake. Na ngoma hizo zilikuwa na jina tofauti kutokana na sababu ya ngoma. Kulikuwa na jina kwa ajili ya ngoma za mavuno, kulikuwa na jina kwa jili ya ngoma za matambiko na kadhalika. 

Baada ya wenyeji kuona aina ya muziki uliokuwa ukichezwa na wanajeshi wa Kijerumani, waliiga na kuanza aina mpya ya muziki waliyoiita ‘Beni Ngoma’.

Badala ya saksafoni na tarumbeta, ala za asili za kupulizia zilibuniwa, na muziki mpya ukazaliwa. Pamoja na kuiga vifaa pia, muziki huo ukawa na viongozi kama wa kijeshi, na kuiga kutoa amri za kijeshi ili kucheza huo muziki kama askari walikatika paredi, na wanamuziki wa Beni ngoma wakawa wanavaa sare kama ilivyo kwa wanajeshi.

Muziki huu ukawa maarufu sana miongoni mwa vijana wa mijini wa wakati huo na ulisaidia sana pia kueneza Kiswahili nchini kwetu. Hata neno muziki lilianza kutumika wakati huo kwani Wajerumani ndio waliokuja na jina ‘muzik’. 

Mwisho wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia ulileta mwisho wa utawala wa Wajerumani na nchi, ambayo hadi wakati huo ilijulikana kama Afrika Mashariki ya Kijerumani, ikakabidhiwa kwa Waingereza.

Waingereza hawakuikubali Beni Ngoma, kwani waliona muziki huo kama aina ya dhihaka kwa jeshi, na walijaribu kuupiga marufuku. Lakini umeendelea kuwepo katika makabila mengine na umekuwa moja ya ngoma zao. 

Kwa mfano, Wanyakyusa na Malipenenga, na Wamanda na Mganda.
Wakati huohuo, Waingereza walianzisha utamaduni wa kuwa na vilabu, ambapo ‘Waafrika waliostaarabika’ walianzisha vilabu vya kucheza dansi. 

Vilabu vya dansi vilinakumbukwa ni Novelty Dancing Club ya Tanga na New Generation Dancing Club ya Dar es Salaam. Vilabu hata vilifanya mashindano, vikicheza muziki wa dansi wa nchi za Magharibi, na muziki huu ulikuwa ule walioupiga kwenye gramafoni. 

Muda si mrefu, vilabu hivi vikaanzisha bendi za muziki zilizokuwa zikipiga muziki ule waliyousikia kwenye gramafoni. Muziki huu mpya ulikuwa msumari mwingine kwenye jeneza la umaarufu wa Beni Ngoma.

Wakati huohuo, kukaingia santuri kutoka Cuba, santuri zilizoleta muziki wa rumba, chacha, borelo, samba, merenge na aina nyingine za muziki ambazo zinadumu mpaka leo.

Bendi hizo mpya za vilabu zikaanza kupiga muziki wa ki Cuba kwa kuiga santuri hizo mpya huo ukwa mwanzo wa muziki wa rumba.

Miongoni mwa makundi makubwa ya muziki ya kwanza kurekodiwa wakati wa utawala wa Waingereza yalikuwa ni  YMCA Social Orchestra na Dar es Salaam Social Orchestra. 

Inasemekana kwamba kundi hilo la pili ndilo lililozaa bendi maarufu ya Dar es Salaam Jazz Band. 

Kwenye mwaka 1948, kampuni ya kwanza ya kurekodi ilianzishwa Nairobi, Kenya. Kuanzia hapo wanamuziki waliotaka kutoa rekodi, kutoka Afrika Mashariki nzima, walimiminika Nairobi. 

Akiwemo kijana wa Kichaga Adam Salim, ambaye ndie mtunzi wa wimbo maarufu Malaika. Lakini hiyo ni hadithi ya siku nyingine. 

Nyota wakubwa walizaliwa, majina makubwa kutoka Tanzania yakiwemo Frank na Dada zake, Dk Hosea Macha, Salum Abdallah wa Cuban Marimba Band, Morogoro Jazz Band na kadhalika. Na kwa miaka mingi, Kenya ikawa kitovu muhimu sana cha muziki wa Afrika Mashariki na Kati.

Baada ya Uhuru wa Tanganyika, karibu kila mji mkubwa ulikuwa na angalau bendi moja au zaidi. Kuna bendi nyingi zilimilikiwa na TANU Youth League, bendi hizo zilicheza aina mbalimbali za muziki; nyingine zilicheza muziki kulingana na kabila lililokuwa na bendi hiyo. Huku bendi nyingine nyingi zikicheza muziki kwa kuiga muziki kutoka Cuba. 
Lakini pia kulikuwa na makundi mengi yaliyocheza muziki kwa kuiga muziki kutoka nchi za Magharibi, kwa kupiga muziki wa aina ya rock n roll.
 
Tanganyika ilipata uhuru wake mwaka 1961, na takriban wakati huo, Wakongo waliokimbia nchi yao walianza kuifanya Tanganyika makazi yao. Wanamuziki kutoka huko walikaa katika baadhi ya miji mikubwa, kama Dar es Salaam, Songea, Tabora, Kigoma, Mwanza na Moshi, na wakaanza kushawishi na kwa kweli kubadilisha mandhari ya muziki wa rhumba nchini.

Wanamuziki wa ndani ambao walicheza muziki katika vilabu vyao kama burudani waliona Wakongo wanaowasili wakijipatia riziki kutokana na muziki tu. 

Makundi ya hapa nyumbani yakaanza kuiga makundi ya Kongo. Waliiga muziki wao, mtindo wa maisha, na baadhi ya wanamuziki walienda mbali hadi kubadilisha majina yao kuwa ya ‘Kikongo’.

Miaka kadhaa baada ya Uhuru, Tanzania ilianza kufuata Sera ya Ujamaa. Mashirika ya umma na taasisi za serikali zilihimizwa kuwa na makundi ya utamaduni; bendi nyingi zilianzishwa kote nchini, na kazi ziliyofanywa na bendi hizo bado zinaheshimiwa sana hadi leo. 

Na hakika kilikuwa kipindi ambacho muziki wa Tanzania ulipata utambulisho wake.
UKIMWI ulipoingia uliwaathiri wanamuziki wengi, na hivyo kuunda pengo kubwa lililosababisha wanamuziki wa zamani kutokukabidhi ujuzi kwa wanamuziki wa kizazi kilichofuata. 

Jambo ambalo limeleta pengo kati ya wanamuziki wa sasa na wale wa zamani. Ni kama vile wanamuziki wa sasa wa rhumba wanapapasa, wakijaribu kupata rhumba ni nini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *